Na Shaffih Dauda
UCHAGUZI wa FIFA umefanyika mwishoni mwa juma lililopita
mjini Zurich, Uswizi, huku dunia nzima ikishuhudia Sepp Blatter akitetea kiti
chake cha urais kwa muhula wa tano mfululizo.
Stori ya uchaguzi mkuu wa FIFA iligonga vichwa vya
wanamichezo duniani na ikapata uzito wa juu zaidi siku moja kabla ya kupiga
kura ambapo maafisa sita wa ngazi za juu wa Shirikisho hilo walikamatwa na FBI
kwa tuhuma za rushwa ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 100.
Kashifa hii nzito ilitikisa dunia na mashinikizo yakaanza
kutolewa yakimtaka Rais Blatter ajiuzulu na baadaye aahirishe uchaguzi mkuu kwasababu
ya tuhumu hizo.
Msimamo wa Blatter , mwenye uwezo mkubwa wa kuongoza soka
ulibaki palepale, uchaguzi ukafanyika mei 29 mwaka huu na yeye kushinda.
Kukaa madarakani kwa muda mrefu, ni sababu inayowafanya
watu wengi waamini Blatter hafai, lakini kashifa hii ya rushwa ambayo ni
propaganda ya nchi za Magharibi iliwaongezea nguvu watu wasiompenda Blatter
akiwemo rais wa Uefa, Michel Platini.
Kimsingi, hizi kelele za Blatter hafai, ni propaganda za
mataifa ya magharibi hususani Marekani. Kwa wale wote wanaompiga vita Blatter, wafanye
uchunguzi, waje hapa watuambie ufisadi
upi umefanyika ndani ya FIFA. Dhahiri hakuna
tuhuma za rushwa ndani ya FIFA kama taasisi , ila hizi tuhuma tunazozisikia
zimetokea kwenye vyama vingine.
Wanachama wa FIFA ni
vyama vya soka vya nchi na siyo vyama vya mabara kama wengi wanavyodhania,
mfano tuhuma za rushwa zinazozungumzwa kuihusisha FIFA zinatokana na chama cha
soka cha America ya kaskazini (CONCACAF ).
Concacaf si mwananchama wa FIFA , ndio maana FBI imewakamata kina Jack
WARNER pamoja na Jeffrey WEBB
kwasababu wao ndio walikuwa viongozi waliohusika kwenye madili hewa
yaliyotokana na haki za matangazo ya televisheni pamoja na kuingia mikataba
kibao ya kifisadi.
Ukifuatilia kwa undani, mataifa ya
magharibi hususani Marekani wanaamini kuwa wao ndio wenye nguvu zaidi duniani ‘Super
Power’. Hawafurahii kuona nchi nyingine duniani inawazidi kiuchumi, kibiashara,
kiasa n.k
Inapotokea taasisi kama FIFA ambayo
si ya kiserikali inakuwa na nguvu kubwa, wafuasi wengi na wanaongezeka kadri siku
zinavyokwenda, Marekani hawafurahii hali hii.
Rais wa FIFA, Sepp
Blatter anaonekana ndiye rais mwenye nguvu kuliko rais yeyote duniani, anaweza
kumzidi hata rais wa Marekani, Barack Obama.
Blatter ni
rais wa dunia wakati Wamarekani wanaamini rais wao ndiye rais wa dunia, lakini
kutokana na nguvu ya mpira wa miguu, Blatter anamzidi nguvu Obama.
Kutokana na
hali hii, Taifa la Marekani linatafuta namna ya kuidhoofisha FIFA na wana tafuta
njia ya kuliweka Shirikisho hilo chini ya himaya yao.
Nikupe mfano
wa UN ambayo ni taasisi isiyo ya kiserikali yenye nguvu duniani. Wakati
wa utawala wa katibu mkuu, Boutros Boutros-Ghali kutoka Misri (1992-1996), UN
ilionekana inakua sana na kuwa na nguvu kupita maelezo.
Marekani chini ya
Rais Bill Clinton (1993-2001) hawakufurahishwa na nguvu iliyoonekana UN. Walitafuta namna ya
kumdhoofisha Boutros ili asiendelee kuwa katibu mkuu katika uchaguzi uliofuata
kwasababu alikuwa na mitazamo iliyoikuza taasisi hiyo.
Waliona UN inakuwa na ushawishi na umaarufu kuliko serikali
ya Marekani, hivyo wakatafuta kila njia ya kumuangusha Boutros ili taasisi hiyo
iwe chini ya himaya yao.
Hii ni sawasawa na sasa ambapo Marekani wanaingia kwenye
vita ya kulidhoofisha shirikisho la soka ulimwenguni FIFA linaloonekana kuwa na nguvu kubwa. Kutokana na ukubwa wa sasa wa FIFA,
inawezekana rais wake, Sepp Blatter akawa na nguvu kuliko hata rais Obama.
Jambo la pili; watu kama Uingereza pamoja na Uefa kwa ujumla
ni wabaguzi. Wao wanaamini waanzilishi wa FIFA ni Uefa. Ukiangalia historia ya
FIFA iliyozaliwa mjini Paris Ufaransa, iliundwa na mataifa ya bara la ulaya kama
vile Ubelgiji, Denmark, Uholanzi, Hispania, Sweden na Switzerland.
Uefa wao wanadai FIFA ni Shirikisho ambalo chanzo chake
ni wao, hivyo sio haki kwa mataifa mengine wanachama wa FIFA kutoka mabara
mengine kuwa na nguvu sawa na mataifa ya ulaya.
Ukinukuu kauli ya rais wa Uefa, Michel Platini kwamba; “Ni
jambo la aibu kwa nchi kama Ufaransa
kuwa na nguvu sawa na ki-nchi kama Vanuatu”.
Hii ni kauli ya kibaguzi kwasababu katika mchakato wa
kupiga kura popote duniani, hakuna kura yenye nguvu kuliko nyingine. Hata wakati
Michel Platini anachaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la soka Ufaransa,
hakukuwepo na kura ambayo inasema matajiri wana nafasi ya ziada ya kupiga kura
10 kuliko maskini. Inapokuja ishu ya
uchaguzi kura ya tajiri na kura ya mtu yeyote mwenye sifa zinafanana.
Kauli ya Platini kwamba nchi kama Ufaransa sio haki kuwa
na kura sawasawa na nchi ndogo kama Vanuatu ni ya kibaguzi moja kwa moja.
Vanuatu ni nchi ndogo ambayo inawakilisha nchi nyingi maskini
hususani kutoka bara la Afrika na Asia ambako kuna mataifa mengi masikini,
lakini kuna kura nyingi za FIFA.
Uefa wanataka rais wa FIFA atokee kwao, wanataka mtu wao
akiingia madarakani wabadilishe katiba kwa mfano kipengele cha timu
zinazoshiriki kombe la dunia.
Wakati wa nyuma, nafasi nyingi walipewa Uefa na nafasi
chache walitoa barani Afrika na mabara mengine. Blatter ndiye aliyeongeza nchi
za Afrika kushiriki kombe la dunia na hayo ni moja ya mafanikio yake katika
utawala wake. Amesababisha mataifa kama Togo, Angola, China yapate nafasi ya
kushiriki kombe la dunia tofauti na huko nyuma .
Falsafa ya Blatter ya kuendeleza mpira duniani kote na kusambaza misaada bila upendeleo, imemfanya
awe na nguvu zaidi na kuyakera mataifa makubwa hususani ya Uefa pamoja na
Marekani. Wanaona kama vile wanakuwa na haki sawa na mataifa madogo kutoka
Afrika na mabara mengine.
TAASISI
YA FIFA KUHUSISHWA NA RUSHWA
Kashifa ya
rushwa wanayohusishwa FIFA ni hila iliyoanzishwa kuharibu uchaguzi wa FIFA.
Kama nilivyoeleza
kwa ufupi mwanzoni mwa makala hii ni kwamba; waliotuhumiwa na rushwa ni vyama
vya soka vya mabara mengine hasa CONCACAF ambao sio wanachama wa FIFA.
Wanachama wa
FIFA ni yale mataifa 209. Zile dili za kupiga dola zaidi ya milioni 100
zilitokana na mikataba ya udhamini mbalimbali pamoja na hela za haki za
matangazo ya televisheni ambayo vyama vya mabara ya Amerika kaskazini na kusini waliingia.
Hiyo kesi inawahusu
waliokamatwa kama vile Jeffrey Webb ambaye alikuwa rais wa CONCACAF. Mtu kama Webb anaishi Miami Marekani na makao
makuu ya CONCACAF yapo mjini humo. Kwanini FBI baada ya kufanya uchanguzi wao
hawakumkata akiwa Miami na wakasubiri wakati wa uchaguzi wa FIFA?
CONCACAF
ndio wenye hatia ya hizo fedha, kwanini wasikamatwe huko huko mpaka wasubiri
siku moja kabla ya uchaguzi wa FIFA mjini Zurich?
Lengo la
Marekani lilikuwa ni kuhamisha malengo ya uchaguzi na kutengeneza mazingira
kuwa FIFA ni chombo cha wahuni na wala rushwa, lakini FIFA kama taasisi
haihusiki kwa chochote na ndio maana Blatter hajakamatwa.
Jack WARNER wakati anaingia FIFA alikuwa makamu wa rais wa CONCACAF, huyu Jeffrey Webb ni makamu wa rais wa sasa wa CONCACAF. Kumbuka hawa wanaingia moja kwa moja kwenye kamati ya
utendaji ya FIFA wakiwa makamu wa Rais.
Katiba ya FIFA inasema kwamba marais wa vyama vyote vya mabara kama
CAF, UEFA, CONCACAF wanaingia moja kwa moja kama makamu wa rais wa FIFA. Wajumbe
wa kamati ya utendaji wanachaguliwa kutoka kwenye vyama hivyo hivyo kutokana na
idadi ya nafasi iliyotengwa kutoka kila chama cha bara.
Maana yake ni kwamba wale wajumbe wanaoingia kwenye kamati ya utendaji
ya FIFA wanachanguliwa na mabara yenyewe. Makamu wa rais wa FIFA anachaguliwa
na nchi wanachama wa vyama vya mabara husika.
Blatter hajakamatwa kwasababu zile fedha hazikupigwa moja kwa moja
kutoka makao makuu ya FIFA, zilizopigwa
kwenye vyama na ndio maana wamekamatwa hao viongozi.
Propaganda za mataifa ya magharibi ilikuwa ni kupotosha umma kwamba
FIFA kama taasisi imehusika na rushwa na
kumchafua Blatter ili wapiga kura waogope kumchagua, bahati nzuri, wajumbe
walibaki kwenye misimamo yao na mwisho wa siku Blatter akashinda na kubaki kuwa
rais wa FIFA.
UKIRUDI KWENYE KIPENGELE CHA KUKAA MUDA MREFU MADARAKANI
Toka Blatter alivyoingia madarakani
mwaka 1973 akiwa kama kalani tu ‘Development Officer’ alifanya kazi nzuri.
Baadaye akateuliwa na rais wa wakati huo wa FIFA, Mbrazil João Havelange kuwa katibu mkuu baada ya kugundua kuwa Blatter
amesomea shahada ya biashara na amebobea kwenye mambo ya masoko.
Blatter alikuja na mbinu mbalimbali za kuiingizia fedha FIFA na moja ya mafanikio yake ya mwanzoni ni
kuwezesha kampuni ya Adidas kuwa mdhamini wa FIFA. Pia akawezesha kampuni ya Cocacola
kuwa mdhamini wa FIFA.
Zaidi ndiye aliyetengezea timu kabambe ya wataalamu
mbalimbali ambao wameliendesha shirikisho kiuweledi na kufungua mianya ya
kupata hela zinazosababisha kuwa taasisi yenye nguvu kubwa duniani.
Ukiangalia maendeleo mengi ya mpira yamekuja kipindi cha
utawala wake na kauli ya kusema amekaa sana madarakani hivyo atoke na waje watu wengine wenye mawazo ya kileo
sio sahihi.
Ni vitu gani vya kileo ambavyo havijafanyika kwenye
utawala wa Blatter? Kupitia teknolojia, ni watu wangapi wameshuhudia fainali za
kombe la dunia kupitia kiganjani?
Ni makampuni mangapi ya kibiashara yameingia mikataba na
FIFA kwa ajili ya kudhamini michezo mbalimbali? Unaposema Blatter atolewe kwasababu amekaa sana madarakani,
sidhani kama ni kigezo sahihi.
Kwa mfano hapa Tanzania tuchukulie Rais wa TFF, Jamal Malinzi
ameingia madarakani, ametengeneza mifumo bora ya soka la vijana, mifumo mizuri
ya ligi na vilabu vya Tanzania inayozalisha wachezaji wengi wanaoweza
kushindana na mataifa mengine yanayoendelea, lakini amekaa kwa muda mrefu
madarakani.
Katika kipindi chake, timu zote za taifa zinashinda na
kufuzu kombe la Mataifa ya Afrika na dunia, lakini wanakuja watu wanasema
Malinzi atoke kwasababu amekaa madarakani kwa mihula minne, hivyo aje mtu
mwingine katika muhula wa tano.
Kigezo cha kumtoa mtu madarakani ni kukaa kwa muda mrefu
au kwasababu ameshindwa kufanya kazi? Kama mtu amefanya kazi kwa muda mrefu na imeonekana,
kwanini aondolewe?
Katika utawala wa Sepp Blatter vimejengwa viwanja vya
kisasa zaidi ya 200. Mataifa madogo kama Haiti, Vietnam, wanacheza mpira kwenye
viwanja bora. Unataka mafanikio gani?
Alichotaka kufanyiwa Blatter ni sawa na alichofanyiwa
Muammar Gaddafi na mataifa ya magharibi hususani Marekani.
Gaddafi alikaa madarakani kwa muda mrefu, lakini alifanya
kazi nzuri, aliboresha miundombinu ya kijamii, wananchi wake walitibiwa bure,
walisoma bure, walipewa fedha za kujenga nyumba, alisaidia kwa kiasi kikubwa
bajeti ya umoja wa Afrika AU, alitoa michango mingi kwa nchi za Afrika, hata
Tanzania aliijengea msikiti mkubwa pale Dodoma.
Kiongozi huyu alifanya mambo makubwa kuliko mtu yeyote
Afrika na pengine dunia yote. Nchi yake ni tajiri na alikuwa na uwezo wa
kufanya lolote lile analota kwa waanchi wake, lakini mataifa ya magharibi yalimezea
mate utajiri wa Libya.
Baadaye wakatafuta namna ya
kumdhoofisha Gaddafi, wakipandikiza
chuki na hatimaye akaondolewa madarakani na kuuwawa kabisa.
Hata katika historia ya Iraq
, nchi yenye utajiri wa mafuta, Marekani walikuwa wanautaka utajiri huo,
walipandikiza chuki miongoni mwa watu, wakapigana na baadaye Rais Saddam
Hussein akauawa na wakafanikisha jambo
lao.
Viongozi wazuri
wanaondolewa kwasababu tu ya kukaa kwa muda mrefu madarakini, inawezekana baadhi
yao wakawa na matatizo kweli, lakini waliowengi ni propaganda za watu wa
magharibi hususani wanapotaka jambo lao litimie.
Kwa mifano hiyo, Sepp
Blatter sio mtu mbaya, Wamarekani wanatafuta njia ya kumuangusha wakitaka
taasisi ya FIFA iwe kwenye himaya yao kama walivyofanya kwa UN, lakini nguvu ya
kura imeendelea kumuweka madarani.
Nawatakia siku njema!
0 comments:
Post a Comment