Thursday, June 4, 2015



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda, amesema kuwa tatizo la rushwa katika mchezo wa soka nchini limekuwa likionekana kufanyika 'waziwazi' na kueleza kwamba jambo hilo linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo huo.
 
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mtanda ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa umefika wakati wale wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukemea kwa nguvu zote.
 
Mtanda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga (CCM) Mtwara, alisema kuendelea kuruhusu rushwa iendelee kutawala katika mchezo huo, timu hazitaendelea na matokeo yake kila siku Tanzania itabaki kuwa wasindikizaji kwenye mashindano mbalimbali.
 
Alisema pia tatizo jingine linalorudisha nyuma maendeleo ya soka Tanzania ni kitendo cha waamuzi kupanga matokeo na kusababisha timu isiyostahili kushinda kuibuka na ushindi.
 
"Waamuzi wanapanga matokeo. Tuwe na waamuzi wenye ubora wa juu ambao watasaidia nchi yetu kusonga mbele. Ninaamini hatua mnazichukua, lakini ni lazima zionekane wazi. Wale ambao wanaonekana wanataka kuchafua taswira ya TFF maamuzi yachukuliwe na yaonekane," alisema.
 
Kiongozi huyo aliitaka pia TFF kuhakikisha inaandaa programu ya mafunzo kwa ajili ya makocha wazalendo ili pale wale wageni watakapoondoka, makocha hao waweze kufundisha katika kiwango cha juu.
 
"Sikatai makocha wageni wanasaidia kwa sababu ni wataalam, ila mpango huo uwepo na uandaliwe utaratibu wa kuweka muda maalumu wa kuhakikisha makocha hao wa kigeni wanaondoka na wale wazalendo wanakuwa tayari kufanya kazi," aliongeza.
 
Alisema pia ili mchezo huo upate maendeleo, ni vyema mpango wa kuboresha viwanja vinavyotumika na akakubaliana na hoja hiyo iliyotolewa na mshambuliaji wa Taifa Stars, John Bocco, kwamba miundombinu haiko katika viwango vinavyotakiwa.
 
NDOLANGA AUNGURUMA
Aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo zamani likiitwa FAT, Muhiddin Ndolanga, ambaye alikuwa mmoja wa wadau 194 waliotunukiwa tuzo maalumu ikiwa ni ishara ya TFF kutimiza miaka 50 tangu ijiunge na FIFA, alimtaka Mtanda kupitia Kamati yake ya Maendeleo ya Jamii kutunga sheria ambazo zitawafanya wachezaji kukatwa kodi na kuweka akiba zao ili zije kuwasaidia uzeeni.
 
Ndolanga alisema kwa kufanya hivyo itawasaidia wachezaji hao baadaye na kwa utaratibu huo serikali itapata pato na uchumi wake kuongezeka kupitia wachezaji hao wa soka.
 
Aliitaka pia serikali kuchukua hatua kwa kusaidia maandalizi ya mchezo wa soka kuanzia ngazi ya chini.
Aliwashukuru pia viongozi wa TFF kwa kutambua na kuheshimu mchango wao na kuongeza kwamba kama kuna atakayebeza basi ni yule aliyekosa kunufaika na kakosa kwa sababu hastahili.
 
Leodegar Tenga, Rais wa zamani wa TFF na Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), alishukuru kwa kupata tuzo tatu lakini akaweka wazi kuwa ile aliyoifurahia zaidi ni ya kuwamo kwenye kikosi cha kwanza na cha mwisho hadi sasa cha Taifa Stars kilichoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1980.
 
Tuzo nyingine alizopata Tenga ni ya kuiongoza TFF kwa muda wa vipindi viwili na vilevile kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa. 


CHANZO: IPP MEDIA

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video