Saturday, June 13, 2015

Na Mwandishi wetu

Katika sehemu ya tatu ya habari hii kuhusu upangaji matokeo unavyolitafuna soka la Tanzania jana, tuliona jinsi mbinu za kutokuadhibu wachezaji zinavyotumika kusaidia timu kushinda.
 
Leo tunawaletea sehemu ya nne ya mfululizo wa habari hii ya kiuchunguzi juu ya kadhia ya kupanga matokeo katika soka la Tanzania. Sasa endelea.
 
UBINGWA WA MTIBWA 1999, 2000
 Mtibwa Sugar FC ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo 1999 na katika mwaka wa mabadiliko ya millennia, 2000.
 
Licha ya kuwa na kikosi kizuri kilichosheheni nyota akiwamo kocha wa sasa wa timu hiyo, Mecky Mexime, mmoja wa maofisa wa juu wa TFF (jina tunalihifadhi) aliiambia NIPASHE kuwa ubingwa huo ulichagizwa na kitendo cha shirikisho kupanga marefa maalum kwa ajili ya mechi za 'Wakatamiwa wa Manungu'.
 
Ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa shirikisho, alisema Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), kilipanga marefa wawili wa kati kuchezesha mechi za Mtibwa kipindi hicho.
 
"Ilikuwa ukimkosa refa Issaro Chacha katika mechi za Mtibwa, basi Nassoro Hamdoun alikuwa katikati. Marefa hao walipangwa kutokana na makubaliano maalum kati ya uongozi wa Mtibwa na FAT," alisema kigogo huyo wa TFF.
 
Alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo, Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser, alisema: "Mambo yalifanyika 2000 inakuwaje leo baada ya miaka 15 yanafuatiliwa? Huyo ofisa wa TFF ina maana na yeye pia kashiriki kupanga matokeo kwa sababu analijua jambo toka 1999, amekaa kimya mpaka leo 2015.
 
"Kama mtu anakuwa nazo habari, za uhakika anazo, halafu anakaa nazo. Maana yake mtu akiiba, na mtu mwingine akamuona anaiba na kumwangalia tu hasemi, wote wezi hao. Huyu naye (ofisa wa TFF) kwenye kushiriki kupanga matokeo yumo vile vile."
 
CHACHA, HAMDOUN WALONGA
Gazeti hili lilizungumza marefa hao wawili wanaoishi Pwani na Kigoma wakakiri kuchezesha mechi zilizoihusisha Mtibwa Sugar, lakini wakakana kupanga matokeo kuibeba timu hiyo.
 
“Ni kweli nilichezesha mechi nyingi za Mtibwa kipindi hicho kwa sababu nilikuwa mwamuzi bora. Mtibwa ilikuwa timu kubwa na mechi zake zilikuwa ngumu. FAT walihitaji mwamuzi bora kwa ajili ya mechi hizo,” alisema Hamdoun na kueleza zaidi:
“Mimi nilikuwa mwamuzi bora kipindi hicho, nilichezesha mechi za Simba dhidi ya Yanga, Simba dhidi ya Mtibwa na Yanga dhidi ya Mtibwa. Hadi ninastaafu jina langu ni jeupe. Sikuwahi kupanga matokeo.
 
“Ukitafuta mwamuzi aliyefanya vizuri kuanzia mwaka 1962 hadi 2000, hutaacha kulitaja jina la Hamdoun. Mimi nilikuwa mwamuzi pekee niliyekuwa ninapandishwa ndege kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam na Mbeya kuchezesha mechi kubwa.”
 
Naye refa mstaafu Chacha alisema ubora aliokuwa nao katika kuchezesha soka kipindi hicho ndiyo uliombeba kuchezesha mechi nyingi zilizoihusisha Mtibwa. 
 
“Takwimu zipo na huwezi kuzipinga, FAT walipanga marefa kulingana na ukubwa wa mechi. Mimi na Hamdoun kipindi hicho tulikuwa marefa bora,” alisema Chacha na kueleza zaidi:
 
“Mimi na Hamdoun tulikuwa miongoni mwa marefa 10 waliochaguliwa kuchezesha Ligi ya Muungano mwaka 2000. Katika orodha hiyo kulikuwa na marefa watano kutoka Tanzania Bara, lakini tuliingia.
 
“Pili, Mtibwa ilikuwa timu bora kipindi hicho, ninakumbuka katika mechi nne za Yanga dhidi ya Mtibwa nilizowahi kuchezesha, Mtibwa ilifunga Yanga tatu bila (mabao 3-0) kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Hii haikuwa timu ya kubeza. Sikuwahi kujihusisha na upangaji wa matokeo na ninachukia suala hilo."

CHANZO: MTANDAO WA IPP MEDIA 

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video