Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda (kulia) akiongozana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, kuelekea kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 50 tangu shirikisho hilo la soka nchini lipate uanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) iliyofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. Mtanda alikemea vitendo vya rushwa na upangaji wa matokeo katika mechi za soka nchini.
Na Mwandishi wetu aliyekuwa Turiani
WAKATI Tanzania imeendelea kufanya vibaya katika soka la kimataifa, upangaji wa matokeo katika ligi za soka nchini umetajwa kuchangia kuligharimu taifa kimaendeleo.
Aidha, baadhi ya maofisa wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) wamekuwa wakishiriki katika vitendo hivyo haramu kwa lengo la kuzibeba baadhi ya timu, hasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE, ulibaini michuano mbalimbali ya soka nchini, hasa Ligi Kuu Tanzania Bara, imekumbwa na changamoto ya upangaji wa matokeo unaofanywa na baadhi ya viongozi na wadau wa soka wasio waaminifu.
Gazeti hili pia lilibaini ni mara chache TFF imejitokeza kupambana na upangaji matokeo. Mwaka 1987 kulibainika upangaji mkubwa wa matokeo katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini timu zilizohusika na kashfa hiyo ziliishia kupigwa faini ilhali hukumu ya kosa hilo ni kushushwa daraja.
Simba na Tukuyu Stars ndizo timu zilizobainika kupanga matokeo zilipofungana mabao 5-5 katika kipindi hicho.
Msimu wa 2008/9 TFF ilimwaadhibu refa wa kati aliyekuwa na beji ya uamuzi ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Othmani Kazi, kwa kumfungia maisha (baadaye alipunguziwa adhabu hadi kifungo cha miezi mitatu) baada ya kubainika kupokea rushwa ya Sh. 200,000 ili kuipendelea Majimaji FC ilipocheza dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mfano wa adhabu kali na stahiki kwa wapangaji matokeo ni tukio lililowahi kutikisa soka la Tanzania mwaka 1984 wakati viongozi wawili wa Yanga, Julius Rutainulwa na Issa Makongoro walipofungiwa maisha na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) baada ya kujaribu kuwahonga waamuzi wa Ethiopia wakati wa mechi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya timu yao na Gor Mahia ya Kenya.
Miongoni mwa athari zinazosababishwa na upangaji matokeo ni kuteuliwa kwa wachezaji wabovu kuingia katika kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) kutoka klabu zinazofanya vizuri kwa kupanga matokeo.
Mwezi uliopita Taifa Stars ilitolewa kwa aibu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (Cosafa) nchini Afrika Kusini ilipopoteza mechi zote za Kundi B dhidi ya Swaziland (1-0), Madagascar (2-0) na Lesotho (1-0).
Kabla ya michuano hiyo kuanza Mei 17, nchi zote tatu zilizoing'oa Taifa Stars, zilikuwa chini katika ubora wa soka kulinganishwa na Tanzania iliyokuwa nafasi ya 107 kwa mujibu wa viwango vya soka vya Mei 2015 vilivyotolewa na Fifa.
Katika kipindi hicho Lesotho ilikuwa nafasi ya 121, Madagascar (150) na Swaziland (176), lakini katika viwango vya mwezi huu Swaziland imepanda kwa nafasi 14 hadi nafasi ya 162 wakati Madagascar imepanda kwa nafasi 37 hadi nafasi ya 113 huku Lesotho ikishuka kwa nafasi moja hadi 122. Tanzania imeporomoka kwa nafasi 20 hadi nafasi ya 127.
Kikosi cha Taifa Stars kilichokwenda Afrika Kusini kwa ajili ya michuano hiyo kiliundwa na wachezaji 19 huku 14 (74%) wakitoka timu zilizomaliza nafasi tatu za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/15, Yanga, Azam na Simba.
Yanga, mabingwa wa msimu uliopita, walitoa wachezaji sita (32%): kipa Deogratius Munishi, beki wa pembeni Oscar Joshua, viungo Said Juma na Hassan Dilunga pamoja na mawinga Mrisho Ngasa na Simon Msuva.
Stars ya Cosafa 2015 pia iliundwa na wachezaji watano (26%) kutoka Azam FC iliyomaliza nafasi ya pili. Wachezaji hao ni kipa Mwadini Ali, mabeki Shomari Kapombe na Aggrey Morris, kiungo mkabaji Erasto Nyoni na mshambuliaji John Bocco.
Simba iliyokamata nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ilitoa wachezaji watatu (16%) ambao ni viungo washambuliaji Said Ndemla na Abdi Banda pamoja na mshambuliaji Ibrahim Ajibu.
Wachezaji wengine watano (26%) waliounda kikosi cha Stars na klabu wanazotoka kwenye mabano ni beki wa pembeni Mwinyi Mngwali (KMKM), beki wa kati Salim Mbonde (Mtibwa), beki wa kati Joram Mgeveke (Mwadui FC), kiungo Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar) na mshambuliaji wa kati Juma Luizio (Zesco, Zambia).
Mara ya mwisho Tanzania kufanya vizuri katika mashindano ya soka ya kimataifa ilikuwa mwaka 1980 wakati Taifa Stars ilipofuzu kwa mara ya kwanza kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
MAREFA KUPANGA MATOKEO
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda (pichani), alisema jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa rushwa katika soka la Tanzania inafanyika waziwazi, jambo ambalo limekuwa linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo huo nchini.
Mtanda (34) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga (CCM), aliitaka TFF kuhakikisha inapiga vita rushwa na upangaji matokeo kwa vitendo badala ya kuishia kukemea jambo hilo mikutanoni.
Alisema kitendo cha mamlaka ya soka nchini kufumbia macho rushwa iendelee kutawala soka la Tanzania, kutasababisha timu husika kutopata maendeleo huku Tanzania siku zote ikibaki kuwa msindikizaji kwenye mashindano ya kimataifa.
"Waamuzi wanapanga matokeo na kusababisha timu isiyostahili kushinda, kuibuka na ushindi. Tuwe na waamuzi wenye ubora wa juu ambao watasaidia nchi yetu kusonga mbele.
"Ninaamini hatua zinachukuliwa, lakini ni lazima zionekane wazi. Wale ambao wanaonekana wanataka kuchafua taswira ya TFF, uamuzi uchukuliwe na uonekane," alisema Mtanda bila kutawataja marefa wanaojihusisha na vitendo hivyo haramu.
Mbali na rushwa na upangaji matokeo, Mtanda alisema maendeleo ya soka la Tanzania pia yamekuwa yakikwamishwa na changamoto ya kuwa na miundombinu mibovu katika viwanja vingi vya soka nchini.
Fredrick Mwakalebela, katibu mkuu wa zamani wa TFF, alisema tatizo la rushwa na upangaji matokeo michezoni lipo hususani mwishoni mwa ligi.
Alisema kuna watu wachache wanaotia doa soka la Tanzania kutokana na mazoea ya kucheza mchezo mchafu na kupanga matokeo katika mechi muhimu, jambo ambalo litasababisha taifa kukosa wachezaji wazuri.
"Kuna mambo mengi yalijitokeza miaka ya nyuma, unakumbuaka suala la wachezaji waliowahi kukamatwa na fedha za kupanga matokeo? Halikuchukuliwa hatua stahiki, na ndiyo maana mambo haya yanaendelea kujitokeza chini kwa chini," alisema Mwakalebela na kueleza zaidi:
"Suala la waamuzi pia linatakiwa lichukuliwe kwa uzito wa juu, kuna mambo fulani yanajitokeza katika michezo, hakika yanatia hofu kubwa. Ukifuatilia ripoti za waamuzi huwa zinafanana sana, lakini ukishuhudia mchezo unaweza kugundua kuwa kuna uhuni umefanyika."
TAMKO WIZARA YA MICHEZO
Aidha, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, aliliambia Bunge la Tanzania mjini Dodoma Juni 4 mwaka huu kuwa kuna baadhi ya klabu zimekuwa zikijihusisha na vitendo vya rushwa na upangaji matokeo.
"Suala la rushwa si jambo jema, kamwe hatuwezi kuliunga mkono. Rushwa zimekuwa zikitokea katika michezo mbalimbali nchini hasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Serikali inalaani vikali vitendo hivyo na inawataka wale wanaojihusisha navyo, kuacha mara moja," alisema Nkamia.
Takwimu za NIPASHE zinaonesha kuwa tangu 2011 asilimia kubwa ya marefa wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliowahi kuadhibiwa na TFF kwa kutomudu mechi au kutoa ripoti za uongo za mchezo, walichezesha mechi zinazohusisha timu kongwe nchini, Simba na Yanga. Baadhi yao ni mwamuzi wa kati Mathew Akrama wa Mwanza (Yanga vs Simba 2012/13), mwamuzi msaidizi mwenye beji ya Fifa, Ferdinand Chacha (African Lyon vs Simba 2012/13), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba 2012/13), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar 2012/13) na Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu 2012/13).
Wengine ni Mwamuzi Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2011/12, Martin Saanya wa Morogoro aliyefungiwa msimu mzima baada ya kutoa penalti kwa Coastal Union iliyozaa bao la kusawazisha katika mechi ya kwanza ya msimu uliofuata wa ligi hiyo kati ya Yanga na 'Wagosi wa Kaya' iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa Agosti 24, 2013 na refa wa kati Mohammed Teofile (Yanga vs Ruvu Shooting).
Wapo marefa wachache wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliowahi kufungiwa na TFF kwa madai ya kuchezesha chini ya kiwango mechi zisizohusisha timu za Simba na Yanga. Waamuzi hao ni Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar). Marefa hao waliadhibiwa msimu wa 2012/13 wa ligi hiyo.
Wengine ni mwamuzi wa kati Stephen Makuka na mwamuzi msaidizi Said Mnonga (Azam FC vs Kagera Sugar 2014/15).
ITAENDELEA KESHO
CHANZO: MTANDAO WA IPP MEDIA
0 comments:
Post a Comment