Na Mwandishi wetu
Katika sehemu ya nne ya habari hii kuhusu upangaji matokeo unavyolitafuna soka la Tanzania jana, tuliona jinsi mbinu za kupanga marefa zinavyotumika kusaidia timu kushinda.
Leo tunawaletea sehemu ya tano ya mfululizo wa habari hii ya kiuchunguzi juu ya kadhia ya kupanga matokeo katika soka la Tanzania. Sasa endelea.
WACHEZAJI KUPANGA MATOKEO
Kashfa ya upangaji wa matokeo ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliwakumba kipa Shaaban Kado na mshambuliaji Ulimboka Mwakingwe (2010/11).
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Pius Kisambale, pia alikumbwa na kashfa hiyo katika msimu wa 2011/2012 wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Wachezaji hao watatu walihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
KADO
Kado, kipa wa zamani wa Mtibwa na Yanga, naye aliwahi kuhusishwa na kashfa za rushwa na kupanga matokeo katika msimu wa 2010/11 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tukio hilo lilitokea wakati mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe (kwa wakati huo hakuwa na timu), alipokamatwa Turiani na walinzi wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa akituhumiwa alikwenda huko ili amkabidhi Kado 'kitu kidogo' kabla ya mechi ili aachie mabao wakati wa mechi ya Mtibwa dhidi ya Simba katika msimu huo. Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani mkoani Morogoro.
Kipa huyo ambaye msimu uliopita alikuwa anakitumikia kikosi cha mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union, hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo alipotafutwa na NIPASHE.
"Ninaomba tuongelee mambo mengine kuliko kuzungumzia mambo na vitu ambavyo kwa sasa havipo kwangu," alisema Kado.
KISAMBALE
Kisambale alihojiwa na Takukuru baada ya kunaswa na viongozi wa Yanga akizungumza kwa simu na mmoja wa 'vigogo' wa Simba kwa madai kuwa na lengo la kukihujumu kikosi cha Wanajangwani katika mechi ya watani wa jadi iliyochezwa Oktoba 29, 2011 kwenye Uwanja wa Taifa. Simba ililala kwa bao 1-0 lililofungwa na Mzambia Davies Mwape.
Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, alikiri suala hilo lilifikishwa katika meza za taasisi hiyo nyeti nchini.
Kiongozi huyo wa Simba alidaiwa kumpigia simu Kisambale wakati Yanga ilipokuwa imeweka kambi kwenye moja ya hoteli za jiji la Dar es Salaam.
Ilielezwa kuwa kigogo huyo wa Simba alimwomba Kisambale akipangwa katika mchezo huo, acheze chini ya kiwango na kumwahidi kumpa pesa na ikiwezekana aongee na wachezaji wengine wa Yanga juu ya mpango huo mchafu.
Katika mahojiano na NIPASHE kwa simu baada ya kurejea nchini kwa mapumziko akitoka Nepal anakoichezea klabu ya Saraswoti Youth, Kisambale alisema kesi yake ilimalizwa kimya kimya.
"Nani kayaleta tena mambo hayo? Zilikuwa hisia tu za baadhi ya watu. Ni kweli nilihojiwa na Takukuru, suala hilo halikuwa la kweli ndiyo maana likamalizwa kimya kimya," alisema Kisambale.
NSA JOB
Mshambuliaji Nsa Job alikiri mwaka juzi kupewa shilingi milioni mbili na mmoja wa vigogo wa moja ya timu kubwa nchini ili acheze chini ya kiwango katika mechi dhidi ya timu hiyo.
Katika mahojiano na kituo cha redio cha Clouds FM Aprili 3, 2013, Job alikiri kupewa kiasi hicho cha fedha na kiongozi wa timu husika ili asiifunge katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini alipokea fedha hizo na kuifunga timu hiyo.
Kutokana na kwenda kinyume cha makubaliano yao, Job alilalamika kuwa kigogo huyo alikuwa akimsumbua kwa kumtaka arejeshe kiasi cha fedha alichopewa.
Hata hivyo, pamoja na taarifa za wachezaji na wapangaji wengine wa matokeo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, hakuna hatua zaidi zilizowahi kuchukuliwa.
KANUNI FIFA KUHUSU RUSHWA
Ibara ya sita ya Kununi za Nidhamu za Fifa inaainisha hukumu ya makosa yanayotokana na watoa rushwa na upangaji matokeo kwenye soka.
Vifungu (a), (b) na (c) vya kanuni hizo vinaeleza kuwa mtu anayebainika kujihusisha na rushwa anaweza kuadhibiwa kwa kufungiwa maisha, kupigwa faini, au kutoruhusiwa kabisa kuingia katikia kiwanja chochote cha soka.
Fifa pia inaweza kuandaa utaratibu wa kufilisi mali za mtuhumiwa na mali zake kutumika kuendeleza soka ikiwa atahusishwa na masuala ya kutoa rushwa kwa marefa.
UPANGAJI MATOKEO KIMATAIFA
Mwaka 1994 soka la Ufaransa lilighubikwa na kashfa ya rushwa baada ya Rais wa Olympique de Marseille, Bernard Tapie, kutuhumiwa kuhonga timu pinzani na matokeo yake timu yake ikashushwa daraja kutoka Ligi Kuu.
Olympique de Marseille ilivuliwa ubingwa wa msimu wa 1992/93 wa Ligi Kuu ya Ufaransa na kupokwa haki ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, 'Super Cup' na Kombe la Klabu Bingwa za Dunia baada ya kuhusishwa na kashfa ya kununua mechi.
Ilibainika kuwa klabu hiyo iliwahonga wachezaji wa Valenciennes FC, Jacques Glassmann, Jorge Burruchaga na Christophe Robert ili wacheze chini ya kiwango.
Nyota hao watatu walipigiwa simu na mchezaji wa Marseille, Jean-Jacques Eydelie, wakiahidiwa fedha ili wacheze chini ya kiwango na pia wahakikishe hawachezi rafu ili wachezaji wa Marseille wasiumie kwani walikuwa wanakabiliwa na mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1993.
Kutokana na kashfa hiyo ya rushwa, Tapie, ambaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya Ufaransa, alifungwa miaka miwili jela kwa kuhusika na makosa hayo.
Tukio jingine ambalo lilitikisa soka la kimataifa ni lile la kashfa ya rushwa na upangaji wa matokeo ya mechi za ligi nchini Italia 2006.
Kashfa hiyo ilihusisha timu za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na zile za Daraja la Kwanza. Timu zilizohusishwa na kashfa hiyo ni Juventus, AC Milan, Fiorentina, Lazio na Reggina baada ya mawasiliano ya simu kati ya viongozi wa timu hizo na waamuzi kunaswa wakati wakipanga mikakati ya kuhongana.
Juventus iliyokuwa bingwa wakati huo ilituhumiwa kutoa rushwa ili kupangiwa waamuzi inaowataka. Kutokana na makosa hayo, klabu hiyo ilishushwa daraja huku Fiorentina na Lazio, AC Millan na Reggina zikipokwa pointi na kupigwa faini.
Aidha, mkurugenzi wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi, alifunguliwa mashtaka ya makosa ya jinai kwa makosa ya rushwa na baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka mitano na miezi minne jela.
Mmiliki wa Fiorentina, Diego Della Valle na Rais wa Lazio, Claudio Lotito alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela na faini ya Euro 25,000 kila mmoja. Mtendaji mkuu wa zamani wa AC Milan, Leonardo Meani alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.
Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Italia, Innocenzo Mazzini alihukumiwa kifungo cha miezi 26 jela wakati refa mstaafu Massimo De Santis alitupwa jela ya miezi 23 kutokana na ushiriki wao katika vitendo hivyo viovu.
Kashfa za watu kununua mechi zimewahi pia kuikumba Brazil mwaka 2005 baada ya refa Edilson Pereira de Carvalho kufungiwa maisha wakati refa Paulo Jose Danelon aliondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya nchi hiyo kutokana na kupokea rushwa ya kampuni za kamari ili kupanga matokeo ya mechi.
CHANZO: MTANDAO WA IPP MEDIA
0 comments:
Post a Comment