PAMOJA na
kumsaini winga , Deus Kaseke na straika Malimi Busungu, bado Yanga wamesema
hawajaridhika zaidi, hivyo wanataka kuongeza nguvu kwenye wingi zote- kulia na
kushoto.
Katika kufanikisha hilo, Kocha Mkuu, Hans van Der Pluijm, anatarajiwa
kushuka Bongo ndani ya wiki hii ambapo ataambatana na wachezaji wawili
wanaomudu wingi ya kulia na kushoto.
Habari kutoka
Yanga zinasema kuwa lilikuwa pendekezo la kocha mwenyewe, lakini taarifa nzuri
kwa Wanayanga ni kwamba nyota hao ni kama mapacha- wanajuana kwa kina, kwani
wote wanatokea timu moja inayoshiriki ligi kuu nchini Ghana.
Taarifa hizo
zimekwenda mbali na kufafanua kuwa mbali na Ghana, pia mitego imetegwa katika
nchi nyingine tano ambazo ni Rwanda, Benin, Sierra Leone, Zimbambwe na Nigeria.
Nafasi ambazo
zinatolewa macho zaidi ni beki wa kulia ambaye anategwa nchini Benin, huku nchi
nyingine wakiangalia zaidi kuimarisha safu ya ushambuliaji na kiungo wa kati.
“Tumeamua kuangalia zaidi kuimarisha winga zetu, ukiangalia Coutinho hana
msaidizi kama ilivyo kwa Kaseke. Na wote atakuja nao kocha akitoka kwenye
mapumziko huko Ghana, sijawajua majina ila wanatoka timu moja,” kilisema chanzo
hicho.
Katibu wa klabu
hiyo, Dk Jonas Tiboroha, amesema mpango wa kusaka wachezaji wa kimataifa,
lakini kikwazo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchelewa kutoa msimamo wao
juu ya ombi la kutaka idadi ya wachezaji wa kigeni kuongezeka kutoka watano
hadi nane.
“Ni kweli kuna
wachezaji wa kigeni tunawafuatilia kwa karibu lakini kama unavyojua tayari
tumejaza nafasi za wageni, kwa sasa tunasubiri tamko la TFF ili tuangalie cha
kufanya zaidi, lakini kuhusu ujio wa kocha na wachezaji hajaniambia,” alisema
Dk Tiboroha.
0 comments:
Post a Comment