Rasmi sasa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm,
ametangaza rasmi kwamba, hana mpango wa kumsajili kiungo aliyekuwa akifanya
majaribio kikosini hapo, Msierra Leone, Lansana Kamara, ila akatamka kauli ya
kishujaa kuwa ndani ya wiki hii atakamilisha usajili wa wachezaji wawili wa
kimataifa.
Mchezaji huyo alipewa taarifa hiyo rasmi na kocha huyo jana
ambapo alimuweka wazi kuwa katika mechi hiyo ya kwanza ya mazoezini hakuonyesha
kitu, hivyo anapaswa kuchagua mawili, aidha kuendelea kujifua na Yanga bila
matumaini yoyote ya kuichezea timu hiyo msimu ujao au aangalie maisha sehemu
nyingine.
Imeelezwa kuwa kauli hiyo ilimchefua mchezaji huyo na kuamua
kukacha mazoezi ya Yanga yaliyoendelea jana Karume kwa ajili ya maandalizi ya
mchezo wao wa kirafiki dhidi ya SC Villa ya Uganda, utakaopigwa kesho kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar.
Kamara aliyekuwa akijifua Yanga kwa wiki
tatu mfululizo, ametemwa kikosini hapo baada ya majaribio ya mechi ya kwanza ya
kirafiki waliyocheza na Friends Rangers ya Magomeni kwenye Uwanja wa Karume,
juzi Jumatano.
“Kamara nimemwambia kwamba kwa kiwango alichonionyesha
mazoezini na kwenye mechi ya juzi ni cha kawaida sana kwa mchezaji profesheno
kama yeye, halafu pia kiwango chake hakikuweza kuzidi viungo nilionao hapa. Kwa
staili hiyo sitaweza kumsajili mchezaji wa kiwango kama chake.
“Kwa hiyo nikamwambia anaweza kuja kuendelea kufanya mazoezi
na sisi kama kawaida lakini sitamchukua, sasa sijajua imekuwaje kama ameacha
kufanya mazoezi au ni vipi kwa sababu leo (jana) sijamuona hapa, hata hivyo
hainisumbui kitu kwa sababu nilishamweleza ukweli wake,” alisema Pluijm.
Alipoulizwa kama timu pinzani za ligi kuu zikimnasa Kamara
itakuwaje, alisema: “Wamnase tu (anacheka kuonyesha hajali), kwa mpira alionao
sidhani kama ataweza kusumbua safu ya viungo wangu, aende tu hata Simba, Azam
au timu nyingine yoyote hakuna tatizo.”
Katika mazungumzo hayo, Pluijm hakuishia hapo tu, bali
aliongeza kuwa kuanzia leo Ijumaa, ndani ya siku tatu lazima asajili wachezaji
wawili wenye viwango vya juu kutoka nje.
“Kuna wachezaji wawili wanakuja, nikuhakikishie tu kwamba
wiki hii haiishi yaani haifiki Jumapili, kuna wachezaji profesheno tunamalizana
nao na wana viwango vizuri tu, sikutajii nchi gani wala wanacheza nafasi gani
ila utawaona tu. Nakuhakikishia tena kwamba kabla ya wiki hii kuisha,” alimalizia
Pluijm.
Wiki iliyopita gazeti hili liliweka wazi kuwa Kamara hana
nafasi ya kuichezea Yanga kutokana na kuonyesha uwezo wa kawaida licha ya
baadhi ya wadau walio karibu na timu hiyo kuonekana kumpigia debe, hivyo neno
limetimia.
0 comments:
Post a Comment