Goli pekee la mshambuliaji Claudio Pizarro lilitosha kuwapa ushindi Peru kwenye mchezo wa kundi C dhidi ya timu ya Venezuela kwenye michuano ya Kombe la Amerika ya Kusini maarufu kama Copa America inayoendelea kutimua vumbi nchini Chile.
Goli hilo kutoka kwa straika wa Bayern Munich lililopachikwa kunako dakika ya 72 lilikuwa na maana kubwa kwa Peru usiku wa kuamkia leo kwenye michuano hiyo, kwasabu Peru wamepata ushindi wao wa kwanza hivyo kufufua matumaini ya kusonga mbele kwenye kundi hilo lenye timu ngumu za Brazil, Colombia pamoja Venezuela.
Peru walistahili kushinda mchezo huo kufuatia Venezuela kucheza pungufu muda mwingi wa mchezo kutokana na Fernando Amorebieta kulimwa kadi nyekundu dakika ya 26 na kuacha Venezuela ikicheza pungufu muda wote wa mchezo.
Dakika ya sita ya mchezo, Venezuela walifanya shambulizi kali ambapo mchezaji Salomon Rondon alipata nafasi ya kufunga ikiwa ni mita nane toka langoni lakini akaachia shuti ambalo liliishi mikononi mwa golipa wa Peru Pedro Gallese ambaye aliunyaka mpira huo kiulaini.
Nafasi peke kwa Peru kwenye kipindi cha kwanza ilikuwa ni dakika tano kabla ya kwenda mapumziko lakini mshambuliaji Guerrero alipoteza nafasi hiyo kwa kupiga shuti lilikwenda nje ya goli na kuikosesha Peru goli la kuongoza kwa kushindwa kuitumia nafasi hiyo adimu.
Kipindi cha pili timu zote zilifunguka na kucheza soka safi huku Peru wakijitahidi kutengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli.
Wakati mchezaji wa Venezuela Tomas Rincon akijitahidi kuokoa mpira uliopigwa na Cueva ndipo mpira huo ukamkuta Pizzaro kwenye njia nae bila ajizi akaukwambisha wavuni kwa shuti kali na kuipa timu yake ya Peru ushindi.
Ili Venezuela waweze kusonga mbele, wanahitaji ushindi mbele ya Brazil ili kujihakikishia wanafuzu kucheza hatua ya robo fainali. Peru wao watakutana na Colombia ambao hawana pointi hata moja siku ya Jumapili kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo.
0 comments:
Post a Comment