Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Nooij amepewa sharti gumu na TFF kuhakikisha Taifa Stars inaifunga Misri ili kufuzu fainali zijazo za AFCON vinginevyo atatimuliwa.'
KOCHA mkuu wa Taifa Stars, Martinus Nooij, amesema kikosi chake kitaibuka na ushindi dhidi ya Misri katika mechi ijayo ikiwa kitafanikiwa kumiliki zaidi mpira dhidi ya Mafarao hao.
Stars itakuwa na kibarua kigumu mbele ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika wakati timu hizo zitakapochuana katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwenye Uwanja wa Borg El Arab uliopo pembeni kidogo mwa mji wa Alexandria, Misri Juni 14, mwaka huu.
Katika mahojiano na mtandao huu jijini hapa leo, Nooij amesema ana matumaini ya kuifunga Misri kutokana na kujiunga kwa washambuliaji wa kimataifa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaokipiga katika kikosi cha TP Mazembe ya DRC.
"Tuna kikosi kipana kwa sasa kinachoundwa na timu mbili. Moja itaenda Kigali, Rwanda kushiriki michuano maalum wakati ya pili ikitangulia Ethiopia kujiandaa dhidi ya Misri.
"Nina matumaini tutaifunga Misri ikiwa tutacheza kwa mfumo wa kumiliki zaidi mpira kama tulivyocheza mechi ya mwisho ya COSAFA (Michuano ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika) dhidi ya Lesotho.
"(Mrisho) Ngasa pia atajiunga nasi muda wowote kuanzia leo akitokea Afrika Kusini," amesema kocha huyo.
MANYIJA Jr, SAID MOHAMED KUONGOZA KIGALI
Mdachi huyo amesema kuwa kikosi kitakachokwenda Kigali kitakuwa na makipa Said Mohamed wa Mtibwa Sugar na Peter Manyika Jr wa Simba.
Kocha huyo amesema atafafanua zaidi kuhusu mipango yake katika mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika muda mfupi kabla ya Stars kulihama jiji la Dar es Salaam kwenda Rwanda na Ethiopia kesho.
0 comments:
Post a Comment