Na
Oswald Ngonyani
Hatimaye shirikisho lenye dhamana ya mpira wa
miguu nchini (TFF) limetoa maamuzi yake kuhusu sintofahamu ya kimkataba baina
ya klabu ya Simba dhidi ya mchezaji wake Ramadhani Singano maarufu kwa jina la
Messi.
Hayakuwa maamuzi yaliyotegemewa na wengi,
yamekuwa ni maamuzi yanayoenda sawia na dhana ya ‘Funika kombe mwanaharamu
apite’.TFF hawajawapa mashabiki haja yao ya kumjua mtuhumiwa halali wa sakata
hilo, wengi wetu tumejikuta tukibaki na labda.
Pamoja na suala hilo kuhitimishwa na
Uongozi wa juu wa TFF chini ya Katibu wake Bw. Celestin Mwesigwa bado kumekuwa
na minong’ono ya wazi miongoni mwa wanafamilia ya mchezo wa soka nchini huku
wengi wao wakiyaona maamuzi ya shirikisho hilo kama ya kupepesa macho ama
kutikisa masikio.
Binafsi nililifuatilia kwa umakini
mkubwa sakata hilo tangu lilipoanza kuchipuka wiki kadhaa zilizopita mpaka jana
(Jumanne) lilipohusisha wahusika wa pande zote mbili kwa lengo la kufikia
maafikiano.
Juu ya maamuzi hayo ya TFF kumeonekana
kuwa na utata wa wazi kabisa huku Katibu mkuu huyo akionekana kushindwa kulifafanua vema sula hilo la
kimkataba na hata kushindwa kutoa majibu
stahiki kuhusu tamati ya mikataba miwili iliyokuwa inakinzana ule unaoisha
mwaka 2015 na ule wa mwaka 2016.
Wanahabari wengi walitaka kujua tatizo
lililokuwa kwenye mkataba lilikuwa ni lipi hasa. Lakini bado kulionekana kuwa
na ugumu kwa watoa ufafanuzi akiwemo Mwenyekiti wa Spotanza, Mussa Kisoki
ambaye alionekana kuridhia maamuzi ya TFF kirahisi sana na hata kuwashangaza
wengi akiwemo Singano mwenyewe.
Ninakumbuka wakati sakata hilo
likipangiwa siku ya kutolewa maamuzi Bw. Kisoki alionekana kuzungumza mengi
kuhusu haki stahiki za mchezaji husika lakini kauli yake baada ya maamuzi hayo
imeonekana kukiuka kile ambacho alikuwa anakisimamia kabla.
Kimsingi wengi tulitegemea makubwa
kutoka kwa Kisoki ambaye alikwenda katika kikao hicho kama Mwenyekiti wa chama
cha wacheza soka Tanzania (Spotanza) na wengi tulitegemea kuona akimsimamia
Ramadhani Singano kinaganaga na hata ikiwezekana kuhoji maswali magumu kwa Simba lakini pia kwa
TFF kwa lengo la kuziondoa sintofahamu zote zilizokuwa zimejitokeza, lakini
hakufanya hivyo.
Katika kikao hicho cha jana TFF wamegundua
kuwa mikataba yote miwili yaani ule alionao mchezaji lakini pia ule walionao Simba, ina matatizo na hivyo Katibu
huyo wa TFF amewataka wahusika wa pande zote mbili wakubaliane upya.
Maamuzi hayo kwa kiasi fulani yameonekana kumweka babaikoni hata
Singano mwenyewe kwani kilichoamriwa katika kikao hicho kwake kimeshindwa kumpa
uhuru wa kujua kama yupo huru au bado ni mchezaji wa Simba.
Kwa wiki kadhaa sasa Simba imekuwa
ikisisitiza kuwa ina mkataba na Messi wa miaka mitatu unaoisha mwaka 2016
lakini yeye mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa alikuwa na mkataba wa miaka
miwili na klabu hiyo na unaisha Julai mwaka huu 2015.
Utata huo kwa kiasi fulani ulionekana
kujenga picha fulani katika vichwa vya wengi huku mtuhumiwa sahihi aliyegushi mkataba
akionekana kutafutwa kwa lengo la kuwajibishwa na mamlaka husika za kisheria
ili kutoa funzo kwa wengineo wenye unasaba na hulka hizo za kihuni lakini kwa
maamuzi haya yaliyotolewa ni wazi kuwa kuna upande ambao haujatendewa haki na
TFF.
Kuwaambia wahusika wakae chini na
kuzungumza upya suala hilo huku mikataba yao ya awali ikifutwa inaonyesha ni
namna gani TFF imeamua kutuzuga watanzania kwa kumficha mharifu.
Kilichokuwa kinalalamikiwa na kila
upande ni uhalali wa mkataba. Wakati Singano akiamini kuwa mkataba wake wa
miaka miwili ulikuwa sahihi, Simba nao walikuwa wameweka bayana kuwa mkataba
wao wa miaka mitatu ulikuwa sahihi pia.
Kwa mantiki hiyo, mkinzano huo wa hoja
za kimantiki kutoka kwa kila pande ziliwafanya wadadisi wengi wa masuala ya soka
kwenda mbali zaidi na kuamini kuwa kulikuwa na kila dalili ya upande fulani
kuhusika katika kugushi mkataba husika, na kilichokuwa kinasubiriwa na wengi ni
kuufahamu upande huo uliokuwa umehusika kuupotosha ukweli.
Kwa maamuzi haya ya TFF, ambayo yameonekana
kuwa kama ya busara kwa watu wac hache ni wazi kuwa sisi wapenda haki tumewekwa
katika mabano na hata kushindwa kujua kipi ni nini, hasa kuhusu mtuhumiwa wa
kitendo hicho cha kihuni.
Kuna mambo ambayo yalionekana
kutoeleweka na hata kuwafanya waandishi waonekane wakihoji sana hususan kuhusu Suala
la kuzingatia mkataba mama jambo ambalo limezidi kuwachanganya hata waandishi
lakini katibu huyo alipoulizwa, alionekana kuwa na majibu ya namna ile ile ya
kuzidi kuwaweka kwenye mabano waandishi hao.
“Hatujaja hapa kutangaza mshindi ni
nani, kwa kifupi ni vizuri waanze upya na kujadili kuhusiana na mkataba mpya,”
alisema.
Messi alikuwa na mkataba unaoisha mwaka
2015, wakati Simba wana mkataba unaoisha 2016 jambo lililozua tafrani kati yao.
Licha ya Mwesigwa kukiri kulikuwa na
mapungufu pande zote mbili baada ya kikao hicho cha pande zote pamoja na Spotanza,
bado alishindwa kuweka wazi kama Messi bado ni mchezaji wa Simba au makubaliano
yanamfanya awe huru.
“Siwezi kuweka hadharani masuala
yanayohusu mkataba, hiyo ni siri kati ya mchezaji na klabu,”alisisitiza.
Tangu kutolewa kwa maamuzi hayo, wadau
wengi wa mchezo wa soka wameonekana kutoridhishwa na kilichoamuriwa huku
wengine wakienda mbali zaidi kwa kuilaumu TFF hasa kutokana na kitendo chake
cha kuuficha ukweli kuhusu sakata hilo.
Binafsi nilitegemea upande fulani
kuwajibishwa kwa kosa la kukiuka sheria na taratibu za kimkataba ili kuwa somo
kwa wengine. Lakini kwa maamuzi haya yaliyotolewa ninajilaumu kwa kupoteza muda
wangu bure kuisubiri hatma ya sakata hili lililoonekana kuwagusa wengi.
Hii ndiyo soka ya Bongo Bwana…..
(0767 57 32 87)
0 comments:
Post a Comment