Nyota wa Brazil na klabu ya Barcelona Neymar hatocheza tena michuano ya Copa America inayoendelea huko Chile baada ya kufungiwa kucheza mechi nne kutokana na kitendo chake cha utovu wa nidhamu alichokifanya wakati Brazi ikicheza dhidi ya Colombia mchezo ambao ulimalizika kwa Brazil kufungwa kwa goli 1-0.
Nahodha huyo wa Brazil alioneshwa kadi nyekundu baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi kupulizwa kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Santiago Jumatano iliyopita. Neymar alimpiga na mpira mgongoni kwa makusudi mchezaji Pablo Armero wa Colombia mara baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya mwisho kumaliza mchezo huo.
Mshikemshike baada ya Neymar kuzua tafran kwa kupiga mpira ulio ‘mbabua’ mgongoni mchezaji wa Colombia
Awali alifungiwa kucheza mechi moja, lakini baadae shirikisho la soka la Amerika ya Kusini (South America Football Confederation) liliongeza kifungo na faini ya dola 10,000 za Kimarekani baada ya Neymar kugundulika kuwa alimtolea maneno machafu mwamuzi Enrique Osses raia wa Chile. Kwahiyo sasa adhabu ya Neymar ni kifungo cha kutocheza mechi nne pamoja na faini ya dola 10,000 za kimarekani
Naye Carlos Bacca wa Colombia amefungiwa kucheza mechi mbili na faini ya dola 5,000 za kimarekani baada ya kuhusika kwenye vurugu zilizotokea kwenye mchezo huo ambapo yeye alimsukuma Neymar mara baada ya kumpiga Armero kwa mpira.
Lakini shirikisho hilo la mpira la America ya Kusini limesema, rufaa ikowazi wa wote waliopewa adhabu na Brazil wanaweza kupinga maamuzi hayo yaliyotolewa kabla ya mchezo wao wa mwisho wa kundi C dhidi ya Venezuela utakaopigwa leo (Jumamosi) usiku kuamkia kesho (Jumapili).
Kwasasa Brazil wanaoongoza kundi C na wanakutana na Venezuela ambao wametoka kupoteza mchezo wao dhidi ya Peru lakini wakiwa wameshinda mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Colombia.
Awali Neymar alianza kuonesha vitendo ambavyo si vya kiungwana kwenye soka pale alipojaribu kufunga goli kwa kutumia mkono lakini baadae ‘akambabua’ na mpira Pablo Armero na kutaka kumpiga kichwa Jeison Murillo.
Kukosekana kwa Neymar kutamfanya kocha wa Brazil Carlos Dunga amtumie Robinho kama mbadala wa Neymar kwenye mechi ijayo dhidi ya Venezuela.
Dunga amekuwa akiwatumia Robinho na Douglas Costa kwenye mazoezi ili kujaribu kutengeneza uwiano mzuri kati yao wakati pia kiungo wa Liverpool Philipe Coutinho anatarajiwa kuanza kwenye mchezo huo ambao utakuwa ni wa kwanza kwake tangu kuanza kwa mashindano.
Robinho amejumuishwa kwenye kikosi cha Dunga mwaka jana baada ya kuikosa michuano ya kombe la dunia wakati huo kocha akiwa Scolari. Robinho ambaye alishawahi kukipiga Real Madrid, Manchester City na AC Milan kwasasa anacheza kwenye klabu ya Santos ya Brazil.
0 comments:
Post a Comment