Tuesday, June 16, 2015

Na Sanula Athanas


Mtaalam wa masuala ya sheria, Frank Chacha, amekosoa uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwashauri Simba na mchezaji Ramadhani Singano 'Messi' kumaliza mgogoro wao kwa mazungumzo.
 
Baada ya kuibuka mvutano mkali kati ya Simba na Singano kuhusu utata wa kimkataba kati ya winga huyo na mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara, TFF ilizikutanisha pande zote jijini Dar es Salaam Jumanne Juni 9 mwaka huu na kubaini kuwapo kwa dosari katika mikataba yote miwili iliyowasilishwa mbele ya shirikisho hilo.
 
Singano anaamini alisaini mkataba wa miaka miwili na Simba unaomalizika mwezi huu wakati Simba wanaamini nyota huyo ana mkataba nao wa miaka mitatu utakaomalizika Julai Mosi mwakani.
 
Baada ya pande zote kukutanishwa na TFF, ilielezwa na shirikisho hilo kuwa pande zote mbili zilikubaliana kuanza mazungumzo ya makubaliano mapya na hatimaye mkataba mpya utakaoanza katika msimu mpya wa 2015/16.
 
Hata hivyo, katika mahojiano na NIPASHE jana, Chacha ambaye pia ni mwanasheria wa klabu ya Yanga, alisema TFF haikulitendea haki soka la Tanzania ilipotoa uamuzi huo wa kisiasa ilhali kulikuwa na kughushiwa kwa nyaraka za mikataba.
 
Alisema TFF ilipaswa kulifikisha suala hilo kwenye mamlaka husika ili lipatiwe ufumbuzi na kukomesha tabia ya baadhi ya wadau wa soka nchini kughushi nyaraka, hasa za mikataba ya wachezaji.
 
"Kwa kuwa TFF ilibaini mikataba yote miwili haiko hai, maana yake ni kwamba Singano si mwajiriwa wa Simba. 'He is a free agent' (yuko huru). Kwa kuwa kulikuwa na mikataba miwili inayokinzana, maana yake kulikuwa na kughushiwa kwa nyaraka hii ni kesi ya jinai," alisema Chacha na kueleza zaidi:
 
"TFF imebaki kuwa mbwa asiyekuwa na meno, haing'ati. Ukiangalia 'issues' (masuala) za kina (Amissi) Tambwe na (Haroun) Chanongo, wale wachezaji bado wanadai pesa zao, hawajalipwa na Simba. Ukiangalia kinachosababisha ni nini, utabaini ni usimba na siasa ndani ya shirikisho. 
 
"Inabidi tuwe na watu ambao ni 'independent' (huru) na 'professional' (wenye weledi). Inapokaa ile Kamati ya Sheria na Hadhi wa Wachezaji, badala kufanya uamuzi kwa misingi ya kisheria, kunatumika busara na siasa."
 
ADHABU KUGHUSHI NYARAKA
Akizungumzia kuhusu adhabu kwa watu wanaoghushi nyaraka, Chacha alisema adhabu kwa mtu anayepatikana na hati hiyo ni kifungo kuanzia miaka mitatu hadi saba na faini kulingana na uzito wa kosa na jinsi mtuhumiwa anavyojitetea mahakamani.
 
Alipotafutwa na NIPASHE jana alasiri, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, hakuwa tayari kuzungumza.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa Yanga, alisema: "I'm in a meeting' (niko kwenye kikao)."
 
CHANZO: MTANDAO WA IPP MEDIA

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video