*Sputanza wawasilisha TFF nyaraka za Singano
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Kumekuwa na mvutano mkali kati ya Messi na Simba kuhusu madai ya kughushiwa kwa mkataba wa winga huyo.'
CHAMA cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza) kimesema kimewasilisha katika Shiriksho la Soka Tanzania (TFF) nyaraka muhimu kuhusu mkataba wa winga Ramadhani Singano 'Messi' na klabu yake ya Simba ili kumaliza mvutano uliojitokeza.
Kumekuwa na mvutano kati ya Messi na uongozi wa Simba baada ya winga huyo kudai kutoutambua mkataba wa miaka mitatu kati yake na klabu hiyo ya Msimbazi uliopo TFF.
Akihojiwa kwenye moja ya vituo vya redio jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Mwenyekiti wa Sputanza, Mussa Kisoky, amesema wamelazimika kuwasilisha TFF nyaraka muhimu za mikataba miwili ya Messi na Simba baada ya kubaini kuna utata katika mkataba wa miaka mitatu ambao mchezaji huyo amedai kutoutambua.
"Messi alifika ofisini kwetu na kutueleza kila kitu kilichotokea kati yake na klabu ya Simba. Kikumbwa ambacho Messi anataka ni ufafanuzi wa mkataba wa miaka mitatu uliopelekwa na Simba TFF ilhali yeye alisaini mkataba wa miaka miwili mbele ya uongozi wa klabu hiyo.
"Baada ya kutupatia nyaraka za mikataba yote miwili, tulibaini kuna utata ndiyo maana tukaamua kuliwasilisha suala hili TFF ili mwanachama wetu (Messi) apate haki yake. Jana nilikaa TFF kwa saa nane tukizungumza nao kuhusu utata wa mkataba wa mchezaji huyu," amesema Kisoky.
Kiongozi huyo wa Sputanza amefafanua pia mbinu ambazo Messi alizitumia kuingia TFF na kupatiwa nyaraka za mkataba unaodaiwa kughushiwa na Simba.
Amesema kuwa winga huyo alilazimika kumdanganya aliyekuwa Meneja Utawala wa TFF (Wanachama wa Shirikisho), Evodius Mtawala, ili ampatie nakala ya mkataba wake na Simba, jambo ambalo Messi alililifanikisha na kupatiwa nakala inayoonyesha ana mkataba wa miaka mitatu na Simba unaomalizika mwishoni mwa msimu ujao.
Lakini,Messi anadai alisaini mkataba wa miaka miwili na Simba unaomalizika Julai Mosi mwaka huu, jambo ambalo linapingwa vikali na uongozi wa Simba.
Baada ya maelezo hayo yaliyoonekana kuuumiza uongozi wa Simba, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope, alijiunga moja kwa moja na kipindi hicho cha redio huku akipinga vikali kitengo cha Sputanza kufafanua kuhusu usajili wa Messi redioni kwa madai kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Simba ni siri.
"Hayo mambo yote unayoyasema kuhusu kughushiwa kwa mkataba wa Messi bado ni madai. Unayaongea vipi kwenye redio ilhali bado hayajathibitika? Utafanya nini kwa Simba pale itakapothibitika kwamba mkataba wa miaka mitatu uliopo ni halali?" Amehoji Hanspope.
Baada ya kuibuka kwa mvutano huyo redioni, Kisoky amesema: "Sijaja hapa kuikandamiza klabu ya Simba, lakini kesi hii itakapoanza TFF, patachimbika mbele ya kamati husika ya TFF."
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, baada ya kutafutwa na mtandao huu, alikiri kuzungumza na uongozi wa Sputanza kuhusu sakata hilo, lakini hajapokea rasmi malalamiko yao.
"Ni kweli jana tulikuwa na watu wa Sputanza katika ofisi za TFF na tuliwaambia wawasilishe suala hilo kimaandishi, lakini hadi ninaondoka leo nilikuwa sijaona nyaraka hizo. Huenda wamewasilisha, lakini bado hazijanifikia," amesema Mwesigwa.
Mvutano wa Messi dhidi ya Simba ni wa kikatiba, hivyo ni wazi utafikishwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
0 comments:
Post a Comment