Na Ramadhani Ngoda
Kinara
wa mabao katika ligi kuu soka nchini Ufaransa Alexandre Lacazette
amekiri kuwa itakuwa vigumu kwake kuzipiga chini ofa kutoka Barcelona au Real
Madrid pindi atakapohitajika na wababe hao wa Hispania na kuzikata maini
Manchester City na Liverpool zinazomuwania kwa udi na uvumba katika kipindi
hiki cha usajili.
Lacazette(24) ameibuka kinara katika upachikaji mabao nchini
humo baada ya kuifungia Olympic Lyon mabao 27 na kuwawezesha mabingwa hao wa
zamani wa Ufaransa kushika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Paris Saint Germain
(PSG).
Alexandre Lacazette akishangilia moja ya mabao aliyoifungia Olympic Lyon. |
Licha ya klabu nyingi kumuhitaji mfumania nyavu huyo,
Liverpool na Manchester City zimekuwa viongozi wa riadha ya kupata sahihi yake
lakini kauli yake inaonekana kuzivunja moyo klabu hizo za nchini Uingereza.
“Sijafanya maamuzi bado. Lakini ni vigumu kusema hapana kwa
Barcelona au Real Madrid japo kwa sasa sifikirii kuhusu hilo,” Lacazetter
aliliambia gazeti la ‘Le Parisien’ la Ufaransa.
Hali ya Arsenal kumuhitaji Kareem Benzema inaweza kuwafanya
Madrid wahamishie akili kwa Lacazettee na kuua kabisa ndoto za Liverpool ama
matajiri wa jiji la Manchester, Manchester City kupata huduma ya mshambuliaji
huyo.
Pamoja na hayo, Lacazette amemtupia mzigo wakala wake
kujadiliana na timu yoyote inayomuhitaji na yeye atakuwa tayari kwa lolote
ambalo wakala wake ataona lina manufaa kwake na hatasita kufanya maamuzi.
“Nitaendelea na likizo yangu, nitamuacha wakala wangu
alijadili hili na kujiridhisha. Sitakuwa na wasiwasi nalo,” alisisitiza
Lacazette.
Lakini nyota huyo bado hajafuta kabisa uwezekano wa kubaki
kwa mabingwa hao mara saba wa ufaransa
kwa msimu mwingine licha ya vilabu kadha wa kadha barani Ulaya kufanya jitihada
za kumuondoa ‘Stade De Gerland’ akisisitiza kuwa anaweza kubaki na kuwa na
msimu mbaya au mzuri.
“Naweza kubaki Lyon na nikawa na msimu mbaya kama
ninavyoweza kuondoka na kuwa namsimu mzuri (aendako). Inategemea na mafikio
yangu, kama nakwenda kwenye timu ambayo ina washambuliaji sita, si sawa na hapa
nilipo(Lyon) ambapo ni chaguo la kwanza,” aliongeza mpachika mabao huyo.
Alexandre Lacazette aliyelelewa katika kituo cha kukuzia
vipaji cha ELCS Lyon na kupandishwa katika timu ya
wakubwa ya Lyon mwaka 2010,
ameshaichezea klabu hiyo michezo 139 na kufanikiwa kupachika wavuni mabao 51
ndani ya miaka mitano aliyoitumikia Lyon almaarufu kama ‘The Kids’ inayomilikiwa
na mfanya biashara maarufu Jean-Michel Aulas.
0 comments:
Post a Comment