Monday, June 15, 2015

'Winga Simon Msuva wa Yanga ndiye aliyeibuka Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa msimu uliopita.'
 
MSIMU wa 2014/15 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ulimalizika Mei 9 Yanga wakitwaa ubingwa huku Ruvu Shooting Stars ikiungana na Police Moro FC kuporomoka daraja.

Kuna wachezaji wengi waliofanya vizuri katika msimu huo. Katika mfululizo wa makala za kuangalia wachezaji wa VPL waliong'ara msimu mliopita, leo tunawaangalia mawinga 10 waliofunika zaidi. Karibu...

1. EMMANUEL OKWI - SIMBA
Kwa mtazamo wangu, huyu ndiye anastahili kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa 2014/15 kutokana na mchango mkubwa alioutoa kukiwezesha kikosi cha Mserbia Goran Kopunovic kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Okwi, mchezaji wa zamani wa SC Villa ya kwao Uganda, Etoile Sportive du Sahel (ESS) ya Tunisia na Yanga, amefunga mabao 10 ambayo yalikuwa na maana kubwa kwa kikosi cha Wanamsimbazi.

Kila goli la Okwi aidha lilizaa ushindi au sare kwa mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara. Goli lake dhidi ya Yanga na lile la dakika za majeruhi dhidi ya Mtibwa Sugar (yote kwenye Uwanja wa Taifa) ni miongoni mwa mabao bora ya msimu. Kwa kifupi, ukiondoa magoli yote ya Mganda huyo, Simba inakuwa miongoni mwa timu mbili ambazo zilipaswa kurejea Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kuporomoka daraja.

Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alipiga 'hat-trick' yake ya kwanza katika misimu yake mitano aliyokaa Tanzania, ameitendea haki nafasi ya winga wa kushoto aliyokuwa akichezeshwa katika kikosi cha Simba msimu uliopita na anaingia katika orodha hii ya mawinga hatari wa msimu.
   
2. BRIAN MAJWEGA - AZAM FC
Alitua Azam FC katika usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana akitokea kwa mabingwa wa Uganda, KCCA FC. 

Licha ya Azam FC kung'olewa katika hatua ya robo fainali dhidi ya Mtibwa, Majwega aling'ara katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari mwaka huu akiibuka kinara wa pasi za mwisho.

Winga huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza katika nafasi ya beki wa pembeni, alifanya kazi nzuri msimu uliopita na kuisaidia Azam kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi akipika mabao mengi. 

Azam wamekuwa wakimtumia katika nafasi ya winga wa pembeni kulia huku wingi ya kushoto ikisimamiwa na mchezaji bora wa msimu wa 2013/14 wa VPL, Muivory Coast Kipre Tchetche.

3. SIMON MSUVA - YANGA
Alikosa mechi mbili za mwisho ambazo Yanga ililala 2-1 dhidi ya Azam na 1-0 dhidi ya Ndanda FC. Pengine ndiyo sababu kuntu ya kushindwa kuifikia rekodi ya mabao 19 iliyowekwa na mfungaji bora wa VPL 2013/14, Mrundi Amissi Tambwe.

Msuva pia hakuwa na uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha Yanga kilichocheza mechi saba za mwanzo msimu uliopita kikiwa chini ya Mrazil Marcio Maximo.

Mbali na kuibuka mfungaji bora wa msimu akifunga mabao 17 ikiwa ni sawa na idadi ya mabao yaliyofungwa na mfungaji bora wa ligi hiyo msimu wa 2012/13, Tchetche, Msuva amefanya kazi kubwa kuipa Yanga taji la 25 la Tanzania Bara.

Akitumika katika nafasi ya winga wa kulia katika kikosi cha Mdachi Hans van der Pluijm, Msuva aliyekulia Azam FC, alifunga mabao muhimu katika mechi ambazo Yanga ingeambulia sare au kipigo. 

Mechi zote mbili dhidi ya Mgambo Shooting Stars ni mfano kuntu kwa hili. Alifunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kufunga  la kwanza katika ushindi wa 2-0 jijini Tanga. Goli la pili lilifungwa na Tambwe.

Uwezo wake wa kukimbia kwa kasi, kupiga pasi za mwisho, kufunga mabao na jukumu jingine alilopewa msimu uliopita la kuwa mpiga penalti mkuu wa Yanga, unamuingiza moja kwa moja kwenye orodha ya mawinga wakali wa msimu.

4. JACOB MASAWE - NDANDA
Kutoporomoka daraja kwa Ndanda FC kumechagizwa kwa kiasi kikubwa na mchezaji huyu wa zamani wa Toto Africans, African Lyon na Oljoro JKT.

Masawe, mchezaji bora wa VPL 2011/12 akiwa na Toto Africans, alifunga mabao matano msimu uliopita yaliyoipatia Ndanda pointi 15 (kila alipofunga bao, Ndanda iliibuka na ushindi). Ukiondoa mabao yake, Ndanda inakuwa miongoni mwa timu mbili ambazo zilipaswa kurejea FDL.

Winga huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji wa kati (Na. 8), ana uwezo mkubwa wa kukimbia, kupiga chenga na kufunga mabao. Kumbuka goli alilowafunga Yanga wakati Oljoro JKT ikilala 2-1 jijini Arusha Aprili 12 mwaka jana. 

Nidhamu ya hali ya juu aliyonayo iliyompa taji la mchezaji bora wa VPL misimu mitatu ni miongoni mwa sababu nyingine kuntu za kumfanya aingiee katika orodha hii.

5. MALIMI BUSUNGU - MGAMBO
Amefunga mabao tisa ikiwa ni nusu ya mabao yote ambayo Mgambo Shooting Stars imefunga. Anawaniwa vikali na Simba ili atue Msimbazi kwa ajili ya msimu ujao.  

Busungu ana kasi na ni mchezaji hatari anapokuwa karibu na lango la wapinzani kwani miguu yake inalijua vyema lango. Kumbuka mechi ya Yanga dhidi ya Mgambo ambayo refa wa kati Ngole Mwangole alionekana kuibeba Yanga katika matukio mbalimbali. 

Ikumbuke pia mechi ambayo winga huyo wa kushoto aliiongoza Mgambo kuiua Simba 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga Machi 18. Hakika, benchi la ufundi la Taifa Stars halijafanya makosa kumjumuisha mkali huyo katika kikosi kinachojiandaa kuikabili Misri mwezi huu. 

6. DEUS KASEKE - MBEYA CITY 
Ametua Yanga kwa mkataba wa miaka miwili uliochagizwa na donge la Sh. milioni 40. Ingawa amefunga mabao mawili tu msimu uliopita, Kaseke ni miongoni mwa mawinga bora wa VPL na amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya kikosi cha City.

Kaseke ni winga mwenye akili nyingi ya mpira, ana uwezo mkubwa wa kukimbia na kupiga chenga. Hakika, Yanga wamelamba dume!
 
7. KIPRE TCHETCHE - AZAM
Mafanikio ya Azam FC katika misimu mitatu iliyopita kwa kiasi kikubwa yamechagizwa na raia huyu wa Ivory Coast.

Katika mechi ambazo Tchetche hakuwamo kikosini, Azam aidha ilifungwa au kuambulia sare. Hakuwapo nchini wakati Azam ilipopoteza mechi mbili mfululizo 1-0 dhidi ya JKT Ruvu Stars na Ndanda FC.

Kama ilivyodokezwa hapo awali, Tchetche alifunga mabao 17 msimu wa 2012/13 na kuibuka  mfungaji bora, msimu wa 2013/14 aliibuka mchezaji bora wa ligi kutokana na kutoa pasi nyingi za mabao na kufunga pia. 

Ingawa kiwango chake kilionekana kushuka katika msimu uliopita, kiungo mshambuliaji huyo ameitendea haki wingi ya kushoto msimu uliopita akipika mabao muhimu yaliyofungwa na mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu.
 
8. MRISHO NGASA - YANGA
Ameiacha Yanga na kujiunga na klabu ya Free State ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL). Alifunga magoli manne msimu uliopita, ikiwa ni rekodi mbovu kwake ikilinganishwa na misimu iliyopita aliyokuwa Azam FC na Simba.

Ngasa hakuwa na mwanzo mzuri msimu uliopita kutokana na kile alichoeleza kuwa ni deni la zaidi ya Sh. milioni 45 alilokuwa anadaiwa na moja ya benki nchini iliyomkopesha fedha kuilipa Simba, likiwa ni agizo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kubainika alisaini mikataba miwili ya klabu mbili tofuati.

Ngasa amefanya vizuri mzunguko wa pili akipika mabao mengi, hususan yaliyofungwa na Msuva na Tambwe. Kwa mfano, katika mechi waliyoshinda 4-1 dhidi ya Police Moro FC na kutwaa ubingwa, Ngasa alipika mabao yote matatu ya mwisho. Bao la kwanza lililofungwa na Tambwe katika dakika ya 41 ambalo binafsi ndilo goli bora la Yanga la msimu, lilipikwa na Msuva.

Ngasa ana uwezo mkubwa wa kukimbia kwa kasi, kupiga chenga na ni mchezaji hatari katika kufungua nafasi kwa wachezaji wenzake ambazo zinakuwa na madhara makubwa kwa wapinzani.

Katika msimu wa 2013/14 ambao Azam FC ilitwaa ubingwa, Ngasa aliibuka kinara wa mabao katika klabu ya Yanga (katika mshindano yote) akifunga mabao 13 na pasi za mwisho 17 VPL). Pia alitwaa kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika baada ya kufunga mabao sita.

Ngasa pia alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi (Aprili) 2015 akilamba Sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa VPL, Vodacom Tanzania.

9.  HAMIS MAINGO - PRISONS
Kutokana na kucheza katika kikosi dhaifu cha timu inayopigania kulinda kutoporomoka daraja karibu kila msimu, winga huyu hatari hajulikani kwa wapenmzi wengi wa soka nchini.

Kama ulikuwa hujui, huyu ndiye aliyesababisha kiungo Amri Kiemba na winga Haroun Chanongo waungane na kiungo Shaban Kisiga kusimamishwa Simba alipofunga goli la ajabu la dakika ya 89 katika mechi yao ya sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya Oktoba 25.

Maingo ni winga wa kulia mwenye kasi na hakabiki kirahisi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga za fedheha. 

Akiwa na kikosi cha Tanzania Prisons, Maingo hushirikiana vyema na beki wa pembeni kulia, Salum Kimenya ambaye pia anapaswa kuwekwa mbali na watoto. 

10. SALUM AZIZI GILA - MGAMBO
Kwa wanaofuatilia kwa kina VPL, watakubalina na mimi kwamba Busungu na Gila ndiyo mawinga hatari zaidi katika kikosi cha Bakari Shime cha Mgambo Shooting.

Mgambo ilifunga mabao 18 katika mechi zote 26 za msimu wa 2014/15, lakini ukichukua mabao ya Busungu ukajumlisha na mabao ya Gila, utapata mabao 12. Kwa mantiki hiyo mabao sita pekee ndiyo yamefungwa na wachezaji wengine wa timu hiyo msimu mzima.

Kama ilivyo kwa Busungu,  Gila ana kasi, nguvu na miguu inayolijua lango lilipo. Kucheza katika kikosi ambacho hakina washambuliaji wazuri, kumewagharimu wawili hao kiasi cha majina yao kutofahamika kwa wapenzi wengi wa soka nchini.

*Imeandikwa na Sanula Athanas, Mwandishi wa Michezo Mwandamizi wa gazeti la NIPASHE. CHANZO: GAZETI LA NIPASHE

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video