Baadhi ya wanachama wa klabu ya Simba wameridhishwa na zoezi la usajili linaloendelea ndani ya timu yao kwa ajili ya kutafuta wachezaji watakaoongeza nguvu kwenye kikosi hicho cha Msimbazi kujiandaa na patashika za ligi kuu msimu ujao
Katibu wa tawi la ’Mpira Pesa’ Magomeni jijini Dar es Salaam Ostadh Masoud amesema, wao kama wanachama wanafurahishwa na hilo na wachezaji wote waliojiunga na timu yao wana imani watakuwa na mchango mkubwa msimu ujao wa ligi kuu pale utakapoanza.
“Timu yetu kwa mara ya kwanza tulipochagua uongozi wa timu, timu iliyokuwepo ilikuwa ni timu ambayo hatujui nani anacheza wapi na nani anacheza pale. Mwisho wa siku mpaka tumemaliza ligi tumepata wachezaji wanne ambao wanatengeneza safu ya ulinzi, viungo wanne na tukapata ma-forward wawili lakini ilikuwa kama namba tisa hatuna na ikawa namba saba hatuna na hata golini napo kulikuwa kuna mashaka,” amesema Masoud.
“Sasa namba tisa amepatikana Mavugo ambaye anaonekana ni mzuri sana na tumemfuatilia tumeona anarekodi nzuri kikubwa tumuombee kwa Mungu aje a-perform na huku kwasababu mchezaji kumsajili kumtoa sehemu moja kumleta sehemu nyingine na kufika kucheza vilevile inabidi kumuombea Mungu. Lakini usajili tumeridhika nao,” amesema.
“Mavugo atakuja kucheza namba tisa kwasababu ndio nafasi ambayo sisi imetusumbua sana, Danny Sserunkuma tuliamini atakuja kuziba nafasi ya Tambwe afanye kama vile alivyofanya Tambwe lakini akashindwa. Maguri naye vilevile kashindwa akiwa kama mzawa wa ndani, kwahiyo tunaamini Mavugo ndiyo mchezaji sahihi wa klabu yetu na kwasababu amepatikana, akiwekwa pale yeye na Kiongera ambaye anarudi na watu wote tulimuona na amekuwa anafanya vizuri sana kwenye timu yetu ya Simba B,” amefafanua.
“Hata ujio wa Mussa Hassani ‘Mgosi’ vilevile sio mbaya kwasababu watu wanasema, kijiji kinachokosa wazee kinakuwa hakina hekima na busara, Mgosi kwa performance yake ya uwanjani akiwa Mtibwa kusema kweli ameturidhisha kwasababu amecheza vizuri sana tunaamini akiwa Simba atatusaidia. Peter Mwalyanzi ni moja ya wachezaji wachache watakaoweza kuunganisha timu kutengeneza kikosi cha kwanza kwasababu mwisho wa siku ni kupata kikosi cha kwanza na wachezaji ambao wanaweza kuja kuingia kuongezea nguvu kikosi,” amengeza.
“Kwahiyo mimi nawapongeza sana viongozi, wamesajili kikosi kidogo ambacho wametumia gharama ndogo lakini ambacho kinauwezo wa kucheza uwanjani,” alimaliza.
0 comments:
Post a Comment