Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
LICHA ya kufumuliwa mabao 3-0 katika mechi iliyopita dhidi ya Misri, uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umeendelea kumvumilia kocha mkuu wa Taifa Stars , Mdachi Martinus Nooij.
Juzi Stars ililala kwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mafarao katika mechi ya kwanza ya Kundi G kuwania kufuzu fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017.
Hata hivyo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, amesema shirikisho hilo litaachana na Nooij ikiwa atashindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu fainali zijazo za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Taifa Stars kwa mara ya tatu katika misimu mitano ya CHAN imepangwa kuanza hatua ya awali ya dhidi ya timu ya taifa ya Uganda (Cranes) katika michuano hiyo itakayofanyika Rwanda mwakani.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mchana, Malinzi amesema mechi ya kwanza ya Stars dhidi ya Cranes itachezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar kabla ya kurudiana Julai 3-5 nchini Uganda na endapo Tanzania ikishindwa kufuzu, ajira na Nooij nayo itafikia kikomo.
"Suala la ajira ya kocha mkuu wa Taifa Stars lilishajadiliwa na Kamati ya Utendaji ambayo ilishatoa tamko kwamba anatakiwa aiwezeshe timu kushiriki CHAN nchini Rwanda mwakani," amesema Malinzi na kueleza zaidi:
"Taifa Stars itacheza na Uganda visiwani Zanzibar Jumamosi, tunawakaribisha sana. Tusipofuzu, maana yake ajira ya Nooij nayo itasitishwa. Suala hilo liko wazi. Hakuna kikao kingine cha Kamati ya Utendaji ya TFF kuhusu suala hilo."
Taifa Stars ilishinda kwa jumla ya mabao 3-2 dhidi ya Uganda katika msimu wa kwanza 2009, ikishinda 2-1 nyumbani na kutoka sare ya 1-1 jijini Kampala.
Uganda ilikuwa shujaa mbele ya Tanzania mwaka jana katika kufuzu baada ya kushinda 1-0 ugenini na kushinda tena 3-1 kufuzu fainali zilizopita zilizofanyika Afrika Kusini.
Stars chini ya Nooij imekuwa na matokeo mabaya huku Tanzania ikiporomoka kwa nafasi 20 katika viwango vya mwezi huu vya soka vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wiki iliyopita.
Ikiwa chini ya Mholanzi huyo, Stars imechezxa mechi 17 ikishinda tatu, sare sita na kupoteza nane.
Katika mechi nne zilizopita Stars imefungwa mabao 7-0 ikiwa ni: 1-0 dhidi ya Swaziland, 2-0 dhidi ya Madagascar, 1-0 dhidi ya Lesotho na 3-0 dhidi ya Misri.
0 comments:
Post a Comment