Busungu (wa kwanza kutoka kulia) akikabidhiwa jezi na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro (katikati) wakati winga huyo alipotambulishwa rasmi leo.
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Busungu aliifungia Mgambo Shooting Stars mabao 10 VPL 2014/15 akikamata nafasi ya nne katika orodha ya wafumania nyavu hatari zaidi wa msimu."
UONGOZI wa Yanga leo umemtambulisha rasmi mchezaji mpya uliyemsajili mwishoni mwa wiki, Malimi Busungu huku ukitamba kuhamia katika usajili wa nyota wa kimataifa.
Busungu, winga wa kushoto aliyefunga mabao 10 katika kikosi cha kocha mkuu mzawa Bakari Shime cha Mgambo Shooting msimu uliopita, alisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili usiku wa kuamkia Jumapili akiwa ni mchezaji huru.
Akizungumza na waandishi kwenye ofisi za makao makuu ya Yanga jijini Dar es Salaam leo, Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, amesema walivutiwa na kiwango cha Busungu msimu uliopita wakiamini atawasaidia katika mechi za kimataifa mwakani.
“Sisi (Yanga) tulivutiwa na kiwango cha Busungu, kazi tuliyopewa na kocha mkuu (Mdachi Hans van der Pluijm) tumeimaliza na tumempa jezi namba 16 ambayo aliichagua mwenyewe,” amesema.
Busungu amekabidhiwa jezi hiyo iliyokuwa inavaliwa na kiungo mshambuliaji Nizar Khalfan ambaye mkataba wake umekwisha huku uongozi wa Yanga kupitia kwa Muro ukisema kuwa: "Ukiona namba iliyokuwa inavaliwa na mchezaji wa Yanga anapewa mchezaji mpya, jiongeze kwamba aliyekuwa anaivaa ameachwa."
Nizar na mshambuliaji wa Yanga, Jeryson Tegete, wanadaiwa kujiunga na kikosi cha kocha mkuu mwenye maneno mengi, Jamhuri Kihwelo 'Julio' cha Mwadui FC.
Kusajiliwa kwa Busungu katika kikosi cha Yanga kumeifanya idadi ya waliosajiliwa msimu huu kufikia wanne baada ya kiungo mshambuliaji Deus Kaseke, kipa Benedikti Tinoko na beki wa pembeni Haji Mwinyi kumwaga wino kwa mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara.
YANGA YA KIMATAIFA
Katika hatua nyingine, Muro amesema kuwa baada ya kufanikiwa kuwanasa nyota wa Tanzania waliokuwa wamependekezwa na benchi lao la ufundi, sasa wanahamia katika usajili wa nyota wa kimataifa.
Miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kusajiliwa ni Donald Ngoma wa FC Platinum ya Ligi Kuu ya Zimbabwe.
"Yanga hii ni ya kimataifa, hata Busungu sasa ni mchezaji wa kimataifa. Kuanzia wiki ijayo tutaanza kutambulisha nyota wa kimataifa wenye viwango vya dunia," ametamba Muro.
0 comments:
Post a Comment