Na Shaffih Dauda
Namshukuru Mungu tumekutana tena Jumamosi ya pili
tangu nianze kuandika makala katika gazeti hili bora la michezo nchini!
Juma hili kuna mambo makubwa mawili yametokea ambayo
ni sakata la utata wa mkataba wa Ramadhan Singano ‘Messi’ na Simba, pamoja
na tuzo za ligi kuu Tanzania bara 2014/2015.
Sakata la Singano na Simba limedhihirisha ‘magumashi’
ya TFF yaliyohitimishwa na tuzo za VPL. Wamefanya tukio la ajabu kwa kuamua kuvunja mikataba ya pande mbili zinazoshindana
kisheria.
Hoja ya msingi katika sakata la Singano ni mkataba
mmoja kughushiwa, kila upande unadai
mkataba wake ni sahihi, lakini TFF wameamua kuvunja mikataba yote na kuwashauri
kuanza majadiliano ya mkataba mpya, ingawa Simba wamekaidi wakidai bado wana mkataba na Messi mpaka Julai
2016.
Mkataba wa miaka miwili alionao Messi alisaini Mei 1, 2013 na unatakiwa kumalizika
Julai 1, 2015, wakati mkataba
wa miaka mitatu walionao Simba na TFF ulisainiwa Mei 1, 2013 na utaisha Julai 1, 2016. Je, mkataba wa miaka mitatu uliopo Simba na TFF na
ule wa Singano wa miaka miwili umeandikwa na nani? Nani ameghushi? Kiu ya
Watanzania ni kujua hilo.
TFF wameshindwa
kuthibitisha mkataba upi ni sahihi, badala yake wanatumia busara kuifuta
mikataba yote kwa madai kuwa ina utata. Kwanini wasiweke wazi mkataba sahihi na
aliyeghushi afikishwe kwenye vyombo vya Sheria?. TFF wameogopa kuathiri
upande mmoja ambao labda wana maslahi nao, wanafunika kombe mwanaharamu apite.
Maamuzi haya ‘Bomu’ yamehitimishwa na tuzo za ligi kuu zilizofanyika juzi. Sitazungumzia
zawadi za mshindi wa kwanza mpaka wa nne, mwamuzi bora wala timu yenye nidhamu
bora, nitajikita katika vipengele viwili vya Golikipa bora na kocha bora.
Magolikipa watatu waliotajwa kuwania tuzo, Mohamed Yusuph (Tanzania Prisons), Said
Mohamed (Mtibwa Sugar) na Shaban Kado (Coastal Union) hawamo Taifa Stars
inayocheza dhidi ya Misri kesho kuwania
kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, AFCON 2017, hii ni dalili tosha kuonesha
kwamba tuzo hizi ni za kihuni tu!.
Kama TFF, bodi ya ligi na wadhamini Vodacom
wanatuaminisha kuwa Yusuph, Said na Kado ndio makipa watatu bora, basi wanathibitisha
kilio cha wadau wengi wa soka ambao wanasema uteuzi wa kocha Mart Nooij si
sahihi.
Wachezaji wanaoitwa timu ya taifa ndio bora ligi
kuu, lakini unataja magolikipa watatu ambao hawapo timu ya taifa, unamaanisha
nini? Kwanini Aishi Manula, Mwadini Ali na Deogratius Munish waitwe timu ya
taifa wakati wapo makipa wengine bora zaidi yao? . Ukiangalia kiundani, Ally
Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam)
wamecheza mechi nyingi za ligi kwa mafanikio, lakini hawakutajwa kabisa,
hii ni sahihi?
TUZO
YA KOCHA BORA
Makocha watatu waliowania tuzo, Goran Kopunovic
(Simba), Hans van der Pluijm (Yanga) na Mbwana Makata (Prisons) wote hawakuanza na timu, lakini najiuliza
swali, kocha bora ni yule anayeiongoza timu kuchukua ubingwa au anayeisaidia timu kutoshuka daraja?
Pluijm tangu awasili mwishoni mwa mwezi Desemba
mwaka jana, ameiongoza Yanga katika mechi 20 za ligi kuu na sita za kimataifa. Ameshinda
mechi 14 za ligi kuu, sare tatu na
kufungwa 3 na akafanikiwa kutwaa ubingwa, ukija mechi sita za kimataifa,
aliibuka kidedea kwenye mechi mbili, akatoa sare moja na kufungwa tatu.
Kopunovic aliyeanza kazi mwezi Januari mwaka huu,
ameingoza Simba katika mechi 18 za ligi kuu, akishinda mechi 12, sare mbili na
kupoteza mitanange minne, wakati kocha bora Mbwana Makata ameiongoza Prisons
katika mechi 8 pekee za ligi kuu akishinda tatu, sare tatu na kufungwa mbili.
Ukiangalia takwimu hizi bila kuzingatia vigezo
walivyoweka bodi ya ligi, Hans Van der
Pluijm ndiye kocha bora wa VPL. Cha ajabu kabisa! TFF wamebadilisha ligi ya
Tanzania kwamba, ili uwe bora unatakiwa kuisaidia timu
kutoshuka daraja na si kuipa timu ubingwa na kucheza kwa kiwango cha juu.
TUZO
YA MCHEZAJI BORA
Mlinzi wa kati wa Azam fc, Paschal Wawa, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi hawawezi
kukosekana kuwania tuzo, wametumia vigezo gani kuwaacha hawa?. Sina tatizo na Simon
Msuva kushinda tuzo ya Mfungaji na mchezaji bora kwasababu alistahili, lakini
nashangaa baadhi ya wachezaji kuachwa.
Tuzo hizi
zinaondoa heshima ya soka la Tanzania na hata mdhamini mwenyewe anachafuka
kwasababu anapenda kudhamini kitu kinachompa sifa.
Nawatakieni wikiendi njema! Tukipewa uzima tukutane
tena Jumamosi ijayo!
(MAKALA HII IMEHAMISHWA KUTOKA GAZETI LA MICHEZO LA CHAMPIONI
JUMAMOSI)
0 comments:
Post a Comment