Muwania nafasi ya kuteuliwa kugombea nafasi ya Urais ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Mh. January Makamba ameahidi kukuza mchezo wa soka katika mkoa wa Tanga endapo atachaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano ili kuleta heshima kwenye mkoa huo kama ilivyokuwa kwenye miaka ya 70.
Makamba anataka kurejesha heshima ya mkoa wa Tanga kwenye soka ambayo imetetereka kwa kipindi kirefu, ameongeza kuwa atahakikisha hamasa inakuwepo kwa wale wote wanaopenda michezo na kusisitiza kuwa, timu zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania kutoka mkoa huo inabidi zinyakue taji la ligi hiyo.
“Tanga ilikuwa inaheshimika, timu za hapa zilikuwa zinashinda zinashiriki ligi kuu ya Tanzania na kuwa mabingwa, zinashiriki michezo ya Afrika. Tanga tulikuwa tunaona timu kutoka nje, sasa tutarudidha hadhi na heshma ya mkoa wa Tanga kwenye michezo”, amesema Makamba.
“Tumeanza kwa kuzipandisha timu zetu mbili za Coastal Union na African Sports lakini tuna timu ya tatu ya Mgambo tutahakikisha kwamba hamasa inakuwepo”, amesisitiza.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Bumbuli ametangaza nia ya kuwania urais kupitia chama chake cha CCM na sasa yupo kwenye ziara akizunguka mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kutafuta wadhamini.
0 comments:
Post a Comment