WEKUNDU wa Msimbazi Simba, siku chache zijazo wanatarajia kumtangaza kocha mkuu mpya anayerithi mikoba ya Goran Kopunovic aliyemaliza mkataba klabuni hapo na kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya.
Afisa habari wa Simba, Hajji Sunday Manara amesema tayari wameshapata kocha wa uhakika kutoka Uingereza ambaye atakata kiu ya mashabiki wa Simba wanaotaka kujua nani atakinoa kikosi chao.
"Suala la kocha limeshakamilika, nadhani ndani ya siku mbili, tatu nitatangaza. Anatoka Uingereza, hakuna haraka, kocha wa Simba atajulikana". Amesema Manara.
Aidha, Manara amesema wanaanza kambi mwezi ujao kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara unaotarajia kuanza Agosti 22 mwaka huu.
"Sisi tunaanza kambi tarehe moja Julai, kocha tumeshampata, jina tutawatajia, haitazidi wiki hii. Tuna utaratibu wetu wa kutangaza mambo yetu ya Simba" Ameongeza Manara na kusisitiza: "Tumepata kocha mzuri, kocha wa uhakika, Simba ni klabu kubwa, makocha wengi waliomba kazi, ilibidi tufanye uchaguzi sahihi na tumeshampata".
0 comments:
Post a Comment