Na Mwandishi wetu, Moshi
MWAKA huu ni sheeedah! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya baadhi ya wakazi wa Moshi kumwangukia aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha ili awanie ubunge katika jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wakizungumza katika kikao maalum kilichoandaliwa na wakazi hao mjini hapa leo, wakazi hao wamesema wanamkubali Mosha kutokana na kusaidia mambo mengi ya kijamii mjini na wanaamini atasaidia kuinua michezo na kutengeneza timu itakayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Wamedai kuwa Mosha amekuwa akifanya mambo mengi mjini hapa katika jamii na makundi mbalimbali na ni mkereketwa mkubwa wa michezo, hivyo ni vyema akawa mbunge wao.
"Miaka mingi sana hapa Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla hatuna timu ambayo inawakilisha mkoa wetu, ni imani yetu kuwa endapo atakuwa mbunge wetu, ataweza kusimamia michezo kikamilifu pamoja na uchumi wetu ndani ya Moshi," amesema Steve Mgaya, mkazi wa Moshi ambaye ndiye alikuwa katibu wa kikao hicho.
Amesema kikao chao kilipata baraka kutoa kwa Baraza la Wazee wa Moshi ambao kwa pamoja wamemtaka Mosha achukue fomu na wao watamsapoti.
Amesema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kufuata kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kuhakikisha wanampata mtu ambaye hatakisumbua chama katika kumuuza.
Ameongeza kuwa wazo wa kumuomba Mosha kugombea Ubunge Moshi mjini halina shinikizo kutoka kwa mtu yeyote ndani ya CCM na wala hawamzuii mtu yoyote kutangaza nia.
MOSHA AFUNGUKA
Alipotafutwa na mtandao huu, Mosha amekiri kufuatwa na kundi la wakazi mjini hapa wakiwamo vijana na wazee pamoja na viongozi wa dini ambao walimtaka kuchukua fomu ya ubunge kupitia CCM.
"Ni kweli nilifuatwa na kundi la wakazi wa Moshi na kunitaka nigombee ubunge, hivyo nimekaa na kutafakari, pia ninaheshimu uamuzi wao. Mimi sitawaangusha kwa vyovyote vile," amesema Mosha.
Kuhusu suala la mkoa wa Kilimanjaro kutokuwa na timu ya ligi kuu, Mosha amesema hata yeye huwa linamuuma kuona mkoa huo uko nyuma kisoka, hivyo anao wajibu wa kuitafutia ufumbuzi kadhia hiyo.
Kujitosa kwa Mosha katika siasa kumetokea ikiwa ni muda mfupi baada ya Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kutangaza nia ya kuwania ubunge wa Viti Maalum (CCM) mkoani Singida.
Akiwa Singida jana, Wema alitangaza nia ya kuwania ubunge kupitia chama hicho tawala katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment