Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
SERIKALI kwa kushirikiana na asasi za kimataifa WildAid na African Wildlife Foundation, viongozi wa dini, wasanii na wanamichezo nchini imezindua kampeni mpya ya kupiga vita tatizo sugu la ujangili linaloikabili Tanzania.
Msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya na mshindi wa tuzo sita za Muziki Tanzania 2015, Ali Kiba ameteuliwa kuwa balozi wa kampeni hiyo pamoja na Miss Tanzania wa zamani, Jacqueline Mengi, mwanamuziki Vanessa Mdee na Mtanzania aliyetikisa katika Ligi Kuu ya Kikapu Marekani (NBA), Hasheem Thabeet.
Watanzania hao wameungana na mabalozi wengine wa kimataifa wa kampeni hiyo Jackie Chan, Yao Ming, Edward Norton, Prince William na David Beckham ambao wanapinga vikali ujangili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini hapa leo asubuhi, Waziri wa Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyarandu, amesema kampeni hiyo imelenga kuongeza ufahamu na kuielimisha jamii kuhusu tatizo la ujangili ambalo linashusha hadhi ya Tanzania kimataifa.
Amesema serikali itaendelea kulinda tembo na wanyama wote waliopo kwenye hifadhi za taifa kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho cha Tanzania na dunia kwa ujumla huku akiwaomba wananchi na viongozi wa dini kuisaidia serikali katika kutekeleza jukumu hilo.
"Kwa niaba ya serikali, ninaipongeza serikali ya China kwa kutangaza kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu nchini China. Niwapongeze pia Ali Kiba na Jacqueline Mengi kwa kugushwa na kujitokeza kuwakumbusha Watanzania kuacha nia na matembo mabaya ya ujangili," amesema Nyalandu.
Naye Ali Kiba amesema ameupokea kwa mikono miwili ubalozi wa kampeni hiyo huku akiwaomba Watanzania kuacha vitendo vya ujangili ambavyo aliviita vya kinyama.
"Wanyama wanaipa nchi yetu thamani, lakini wanauawa kwa mateso na kikatili. Tembo unapomtoa meno yake ni kumuonea. Ni sawa na wewe uende hospitali halafu wakung'oe jino bila ngazi. Huu ni unyama. Nimelivalia njuga suala hili. Nitapaza sauti yangu nikiwa Balozi wa WildAid," amesema Ali Kiba.
Kwa upande wake Jacqueline alisema kuwa atadhamini matangazo ya kampeni hiyo katika vyombo vya habari vya IPP.
"Nimefurahi kuwa Balozi wa WildAid. Nilisononeka sana kuwaona watoto wa tembo walivyoathirika baada wazazi wao kuuawa kinyama nilipotembelea kituo cha kulelea watoto yatima wa tembo jijini Nairobi," amesema Jacqueline na kueleza zaidi:
"Ninapenda kuwahimiza Watanzania wenzangu kulinda urithi wetu. Tujenge kizazi kinachochukia ujangili. Tusikubali kuwa kizazi kinachokaa kimya ilhali wanyama wetu wanaangamia."
Mkurugenzi wa African Wildlife Foundation, Patrick Bergin, amesema idadi ya sasa ya tembo imepungua kwa asilimia sitini (60%) kulinganishwa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
"Mwaka 2005 Botswana ndiyo iliyokuwa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo ikiwa na jumla ya tembo 150,000. Tanzania ilikuwa ya pili ikiwa na tembo 136,000 ikifuatwa na Zimbabwe iliyokuwa na 90,000 na Kenya iliyoshika nafasi ya nne ikiwa na tembo 25,000," amesema Bergin na kuongeza:
"Utafiti uliofanyika hivi karibuni unaonyesha kuwa Botswana bado inaongoza ikiwa na idadi ile ile ya tembo 150,000. Hii ina maana kwamba tembo wamezaliana, lakini ujangili pia ulichukua nafasi.
"Nafasi ya pili inashikiliwa na Zimbabwe ambao wana tembo 75,000. Kwa maana hiyo tembo zaidi ya 15,000 wameuawa. Tanzania ni ya tatu ikiwa na idadi ya tembo ambao wamepungua kwa asilimia 60, na ya nne ni Kenya ambayo imeongeza tembo 1,000."
Mkurugenzi Mtendaji wa WildAid, Peter Knights, amesema utafiti walioufanya Aprili mwaka huu katika wilaya 138 za mikoa 30 nchini kuhusu mitazamo na uelewa wa Watanzania kuhusu wanyama pori hasa tembo na vifaru, ulionyesha kuwa asilimia 79.1 ya watu wote 2,030 waliohojiwa, walionyesha kuwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa tembo kutoweka Tanzania.
Mkurugenzi huyo pia amewapongeza Ali Kiba na Jacqueline kwa kujitokeza kupamba na ujangili huku akiunga na na Nyalandu kutambua jitihada za China kupiga vita tatizo hilo.
Video mpya inayomhusisha Ali Kiba na Jacqueline tayari imeshatengezwa na imeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mbali na Ali Kiba na Jacqueline, Nyalandu pia alikuwa amefuatana na viongozi wa dini katika hafla hiyo leo asubuhi.
0 comments:
Post a Comment