SIKU chache baada ya Bodi ya ligi (TPLB) kwa kushirikiana na wadhamini Vodacom kugawa zawadi za ligi kuu soka Tanzania bara (VPL) msimu wa 2014/2015, kocha mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Musa Kiwhelo 'Julio' amewajia juu wanaopinga Shaban Hassan Kado kuchaguliwa golikipa bora na Mbwana Makata kuwa kocha bora.
"Kuna watu wanapinga Kado kuchaguliwa kuwa kipa bora, wapo wengine wanapinga vilevile Mbwana Makata kuchaguliwa kuwa kocha bora, Watanzania tuondoe hizo dhana potofu, waliomchagua Makata na Kado wana akili, wameona vigezo ndio maana wamewachagua.Tuacheni chuki, mbona wengine hatukupata kama mimi Julio?, muda ukifika tutapata". Amesema Julio.
Kocha huyo wa zamani wa Simba na Coastal Union amewataka watu kukubali matokeo, lakini amefurahia kuona Kado aliyemsajili Mwadui akitokea Coastal Union amekuwa kipa bora.
"Binadamu tuwe na utaratibu wa kukubali matokeo kwa kile kinachofanywa, nimefurahi kwamba nimemchukua mchezaji kwenda naye Mwadui halafu amechaguliwa kuwa kipa bora, hii inaonesha kwamba timu yetu imepata mtu aliyestahili". Amesema Julio.
Kado alikuwa anawania tuzo ya Golikipa bora na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar na Mohamed Yusuph wa Tanzania Prisons, wakati Makata alichuana na Goran Kopunovic wa Simba na Hans van der Pluijm wa Yanga.
0 comments:
Post a Comment