Shirika la
utangazajia BBC limeripoti kuwa aliyekuwa makamu wa rais wa shirikisho la Soka
Duniani FIFA, Jack Warner ameituhumu Marekani kwamba inafuatilia mashtaka ya rushwa dhidi
ya maafisa waandamizi wa shirika hilo kwa sababu imeshindwa kuwa mwenyeji wa
kombe la dunia la mwaka 2022.
Akiandika katika gazeti ambalo analolimiliki huko Trinidad
na Tobago, bwana Warner amesema tuhuma hizo dhidi yake na wengine kumi na tatu
zinaonyesha kwamba Marekani inaegemea upande mmoja.
Warner amekana tuhuma hizo. Shirikisho hilo la Soka Duniani
limegubikwa na tuhuma za rushwa kwa kipindi cha wiki mbili mfululizo. Akiandika
katika gazeti lake linaloitwa Sunshine, Warner anaelezea mashtaka ya Marekani
dhidi yake kuwa ni uonevu na yaliyoegemea upande mmoja.
Warner amesema Marekani ambayo inajifanya kuwa ni polisi wa
dunia, imehamasika kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa kuwa mwenyeji wa
mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2022.Warner, mwenye umri wa miaka 72
amekana tuhuma za kupokea rushwa ya dola milioni kumi za kimarekani kutoka
Afrika Kusini baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia
ya mwaka 2010.
Katika makala yake, Warner ameendelea kujitetea kwa kusema
kuwa, kuishutumu Afrika Kusini kunachafua hadhi ya hayati Nelson Mandela ambaye
ameisaidia Afrika Kusini kupata nafasi hiyo.
Gazeti hilo limeonyesha picha za Jack Warner akikutana na
Prince William, David Beckham, Barack Obama na Vladimir Putin ambao amesema
wote walikuwa na ushawishi pindi nchi zao zilipokuwa zikifanya kampeni ya kuwa
mwenyeji wa Kombe la Dunia.Jack Warner amemalizia kwa kuuliza iwapo walikuwa
wanatumia takrima kama rushwa?
Jack Warner ni mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa bodi ya
shirikisho la soka duniani FIFA, ambao wanatuhumiwa kwa kashfa ya rushwa na
mpaka sasa Warner amekana tuhuma zote zinazomkabili.
0 comments:
Post a Comment