*Atauweza mfupa uliowashinda Wabrazil, Waserbia?
KOCHA Dylan Kerr ameweka rekodi ya kuwa Muingereza wa kwanza kuinoa Simba tangu vurugu za kutimua ovyo makocha zilipoanza katika klabu hiyo ya Msimbazi mwaka 1998.
Aidha, beki huyo wa zamani wa klabu za Leeds United na Reading za England pamoja na Arcadia Shepherds FC ya Afrika Kusini, amekuwa Muingereza wa pili kuzinoa klabu kongwe nchini Simba na Yanga katika miongo miwili iliyopita. 1997 Steve McLennan aliinoa Yanga.
McLennan, kocha mzungu wa kwanza Yanga, alitimuliwa na nafasi yake akakaimu kwa muda aliyekuwa msaidizi wake, Juma Pondamali ‘Mensah’, kabla ya Tito Oswald Mwaluvanda kuajiriwa 1998.
Kerr (48) pia amekuwa kocha mkuu wa pili kutoka Uingereza atakayeongoza timu ya Tanzania katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2015/16 utakaoanza Agosti 22 baada ya Azam FC kumrejesha kwa mara pili Stewart Hall.
Takwimu za NIPASHE zinaonyesha kuwa Kerr anakuwa kocha wa 20 kuinoa Simba tangu 1998 timuatimua ya makocha (makocha wakuu) ilipoanza ikiwa ni wastani wa kocha mmoja kila mwaka.
Kerr pia anakuwa kocha mkuu wa 10 kuinoa Simba katika miaka mitano iliyopita. Achilia mbali Jamhuri Kihwelo 'Julio' na Selemani Matola ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiinoa timu hiyo wakiwa makocha wakuu wa muda.
Tangu 2010 timu hiyo ilipita chini ya mikono ya makocha wakuu: Mzambia Patrick Phiri (2010), Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Mganda Mosses Basena (2012), Mserbia Milovan Cirkovic (2012), Mfaransa Patrick Liewig (2013), mzawa Abdallah 'King' Kibadeni (2013), Mcroatia Zdravko Logarusic (2013-2014), Phiri tena (2014), Mserbia Goran Kopunovic (Januari - Mei 2015) na sasa Kerr.
Makocha walioinoa timu hiyo tangu 1998 ni: Mohamed Kajole (1998), David Mwamaja (1999), Mrundi Nzoyisaba Tauzany (1999-2000), Kibadeni (2000), Syllersaid Mziray (2000), Mkenya James Siang'a (2001-2004), Phiri (2005), Mbrazil Neider dos Santos (2006), Talib Hilal raia wa Oman (2007), Cirkovic (2009), Phiri (2010), Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Basena (2012), Cirkovic (2012), Mfaransa Patrick Liewig (2013), Kibadeni (2013), Logarusic (2013-2014), Phiri (2014), Kopunovic (Januari Mosi - Mei 2015) na sasa Kerr.
Imeelezwa kuwa Kerr Kerr ataigharimu Simba kiasi cha dola 9,000 (Sh. milioni 20) kila mwezi, dola 6,000 (Sh. milioni 13.2) ikiwa ni mshahara kwa mwezi na kiasi kinachobaki kitatumika kumlipia gharama mbalimbali zikiwamo za nyumba na usafiri.
Binafsi sitarajii mambo mapya katika klabu ya Simba kutoka kwa Kerr kutokana na historia ya klabu hiyo na soka la Tanzania kwa ujumla.
Klabu ya Simba, kama ilivyo kwa watani wao wa jadi Yanga, haina tatizo la wataalam wa ufundi. Mfumo wa uendeshaji wa soka nchini unaotawaliwa na upangaji matokeo na fitna ndiyo umekuwa kikwazo kwa maendelezo ya klabu hizo na soka la Tanzania kwa ujumla.
Makocha wengi wanatemwa na Simba na Yanga kutokana na ama kuwa wakweli kupita kiasi kwa kuanika changamoto za muda mrefu zilizopo katika klabu hizo au kwa kushindwa tu kupata ushindi katika mechi za watani wa jadi kati ya timu hizo.
Je, Kerr ana kitu gani cha ziada ambacho makocha waliopita Simba hawakuwa nacho kiasi kwamba ajihakikishie ajira ya mwaka mzima aliopewa na hata kuongezwa muda katika klabu hiyo ya Msimbazi?
Mathalani, Kopunovic ameiongoza Simba katika mechi 18 kati ya 26 za VPL msimu uliopita ikipoteza nne dhidi ya Stand United, Mgambo na Mbeya City (alifungwa mechi zote mbili dhidi ya City), ikashinda 12 na kutoka sare mara mbili. Simba chini yake ikamaliza nafasi ya tatu, moja zaidi ya msimu wa 2013/14, lakini hajaongezwa muda kutokana na kile kilichoelezwa kuwa alitaka fungu kubwa.
Mbali na mafanikio hayo VPL, Kopunovic pia aliiongoza Simba katika mechi tano kati ya sita za michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar ambako mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara walitwaa ubingwa.
Kocha huyo alikuwa jukwaani wakati Simba ikifungwa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan visiwani humo siku ya Mwaka Mpya, ikiwa ni saa chache baada ya kusaini mkataba mfupi wa miezi sita kuinoa timu hiyo ya Msimbazi.
Kwa mantiki hiyo, Kerr ni wa bei nafuu kuliko Kopunovic jambo ambalo linatoa taswira kwamba huenda Muingereza huyo hana uwezo mkubwa wa kufundisha soka kulinganishwa na Mserbia Kopunovic.
Ikumbukwe kuwa baada ya kuingia madarakani, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, aliamua kuvunja mkataba wa aliyekuwa kocha mkuu wa Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen, kwa kigezo hicho cha Simba (mshahara mkubwa ambao ulikuwa dola za Marekani 17,500) na kumleta kocha wa bei nafuu aliyechemsha, Mdachi Martinus Nooij.
Kama ilivyokuwa kwa Kopunovic, Simba imerudia kosa kwa kumpa Kerr mkataba mfupi wa mwaka mmoja, hali ambayo inaonyesha timu hiyo haijajiridhisha kikamilifu na uwezo wa kocha huyo na inamleta kumfanyia majaribio.
Hii ina maana kwamba, akifanya vizuri atapanda dau kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake na Simba itashindwa kumlipa na itamtimua na kuendeleza rekodi yake mbaya ya kuingia gharama za kusaka kocha mpya kila msimu.
Mfano, Mcroatia Logarusic alifukuzwa akiwa ametumikia mwezi mmoja tu katika mkataba wake wa mwaka mmoja na klabu ikalazimika kumlipa kwa kukiuka haki za kimkataba.
Mserbia Cirkovic alirejea nchini mwaka juzi akiidai Simba Dola za Marekani 32,000 (Sh. milioni 72.6) kutokana na kuvunjwa kwa mkataba wake na klabu hiyo. Hali hiyo pia iliwahi kumpata Mganda Basena ambaye alirudi kwa mara ya pili kuinoa Simba huku akiidai Sh. milioni 99 za mshahara wake. Hii ni mifano michache tu.
Ikumbukwe pia kuwa mabadiliko ya mara kwa mara ya wataalam wa benchi la ufundi yamekuwa yakiigharimu Simba kwani baadhi ya makocha wapya wamekuwa wakitoa ushauri usiofaa. Msimu uliopita Simba ilimtema mfungaji bora wa VPL msimu 2013/14, Mrundi Amissi Tambwe, kutokana na ushauri mbovu wa Phiri.
Usajili wa Simba kwa ajili ya msimu wa 2015/16 unatekelezwa kutokana na ripoti ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo msimu uliopita, Kopunovic. Hii inamaanisha kwamba Kerr anakuja kufundisha kikosi kilichosajiliwa kutokana na mfumo wa Kopunovic. Je, makocha hao wawili wana mfumo sawa wa ufundishaji?
Hiki ndicho kiliigharimu Simba katika misimu mitatu iliyopita kutokana na kunolewa idadi kubwa ya makocha. Kila kocha anakuja na mfumo wake, jambo ambalo katika misingi ya ufundishaji ya michezo (Principles of Sport Training) ni hatari kwani husabisha kuwachanganya wachezaji.
Ninafikiri kulikuwa na haja Simba kumbakisha Kopunovic au kuajiri kocha atakayedumu kwa muda mrefu ili kuepuka gharama za usajili wa makocha kila mwaka na changamoto nyingine zitokanazo na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha nilizoziorodhesha hapo juu.
*Imeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi wa michezo mwandamizi wa gazeti la NIPASHE.
CHANZO: MTANDAO WA IPP
0 comments:
Post a Comment