Na Ramadhani Ngoda.
Mlinda wa mlango wa
Manchester United, David De Gea ameshindwa kutegua kitendawili kilichotanda juu
ya mstakabali wake katika klabu hiyo na kuzipa nguvu tetesi za yeye kuhamia
Real Madrid anakohusishwa nako kwa muda mrefu sasa.
Real Mdrid
inayotazamiwa kumtangaza Rafa Benitez kama mrithi wa Carlo Anceloti katika
klabu hiyo yenye maskani yake Santiago Bernabeu, imekuwa ikihaha kunasa dole
gumba la mlinda lango huyo na kumrudisha katika jiji alilozaliwa na kuwa mrithi
wa Ika Cassilas anayeonekana kuhitaji mbadala katika klabu hiyo.
David De Gea
amebakisha mwaka mmoja katika kandarasi yake Old Trafford na ameshindwa kuweka
wazi iwapo atabakia United au ataelekea Madrid wanaohitaji huduma yake kwa udi
na uvumba katika kipindi hiki cha usajili.
“Tutaona nini
kitatokea juu ya mstakabali wangu,” De Gea aliliambia gazeti la AS la nchini
Hispania aliko mapumzikoni kwa sasa baada ya kwisha kwa msimu wa ligi na
kuisaidia United kushika nafasi ya nne na kurudi katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Licha ya sintofahamu
hiyo, kocha wa mashetani wekundu Manchester United bado ana matumaini kuwa De
Gea atabaki Old Trafford na kuisaidia United kushinda mataji katika msimu ujao.
De Gea(24) aliyejiunga
na United akitokea Atletico Madrid kwa ada ya uhamisho wa pauni million 17.8,
ameshaichezea Man United michezo 132 mpaka sasa na ameonekana kuzivaa vema ‘gloves’
za Mdachi Edwin Van De Sar aliyestaafu baada ya fainali ya ligi ya mabingwa
Ulaya mwaka 2008.
Kama De Gea ataondoka
United, itamlazimu Luis Van Gaal kuingia sokoni na kutafuta mlinda mlango
atakayechukua nafasi ya Mhispania huyo licha ya kuwepo kwa Mhispania mwingine
Victor Valdes aliyesajiliwa katikati ya msimu uliopita kutoka Fc Barcelona.
Tayari walinda lango
kama Hugo Loris (Spurs), Asmir Begovic(Stoke City) na Jasper Cillesen(Ajax)
wametajwa kama tazamio la Luis Van Gaal kama warithi wa mikoba ya De Gea kama
kweli atahamia kwa mabingwa hao mara 10 wa Ulaya.
0 comments:
Post a Comment