KUFUATIA kiwango kizuri walichokionyesha kwenye michuano ya kombe la Muungano Mufindi na mafanikio kwenye ziara ya michezo 8 ya kirafiki wilayani Sumbawanga, nyota 7 waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya vijana U20 ya Mbeya City Fc wamepandishwa kikosi cha kwanza.
Akizungumza mapema leo Kocha Mkuu wa City Juma Mwambusi amesema kuwa ameamua kuwapandisha wachezaji hao kikosi cha kwanza ili waweze kuitumikia timu yao kwenye msimu ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara inayotarajia kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi wa 8.
“Sina shaka na uwezo wao, ripoti yao kwenye michuano ya Muungano ilikuwa safi na pia uwezo mzuri waliouonyesha kwenye ziara ya michezo 8 ya kirafiki huko Sumbawanga inanipa imani kubwa ya kufanya vizuri kwenye ligi hasa ukizingatia vipaji vyao, ni wachezaji vijana ambao watakuja kuungana na vijana wengine kikosini kutengeneza nguvu ya pamoja na wakongwe wachache tulionao jambo ambalo naamini litaifanya City kuwa na kikosi kikubwa na bora msimu huu” alisema.
Wachezaji walipandishwa kikosi cha kwanza kutoka U20, ni Bakary Mwinyijuma, Aboubakary Shabani, Salvataory Rafael, Monti Stafano,Medson Mwakatundu, Hemed Omary, na Rajabu Seif huku pia Joshua Ibrahimu akipewa nafasi ya kufanya mazoezi na timu kubwa ili kuimarisha zaidi uwezo wake hasa baada ya kucheza vizuri kwenye ziara ya Sumbawanga.
Katika hatua nyingine Kocha Mwambusi amesema kuwa nyota wengine 27 waliokuwa kwenye ziara ya michezo ya kirafiki watasajiliwa kwenye kikosi cha Vijana cha City U20 tayari kwa michuano ya vijana huku pia wakiendelea kuimarishwa kwa ajili ya kuja kuitumikia timu kubwa siku za usoni.
“Tulikuwa na kundi kubwa la vijana zaidi ya 100 waliojitokeza kuja kufanya majaribio kati yao 50 walipita kwenye mchujo wa kwanza na kufanikiwa kusafiri hadi Sumbawanga, baada ya michezo nane 27 kati yao wamefaulu na watajumuishwa kwenye timu ya U20,hili ni jambo zuri linatufanya kuwa na hazina kubwa ya wachezaji ambao wataendelea kuimarishwa ili wawe kwenye kiwango bora siku za usoni” alimaliza Mwambusi
0 comments:
Post a Comment