Na Ramadhani Ngoda.
Winga wa kimataifa wa Argentina na Manchester United, Angel
Di maria anayeitumikia Argentina katika michuano ya Copa America nchini Chile kwa
sasa, ameweka wazi kuwa kushinda taji akiwa na timu ya taifa ya Argentina
kutamfanya asahau mataji yote aliyoshinda akiwa na vilabu alivyowahi
kuvitumikia katika maisha yake.
Di maria aliyeibuka nyota wa mchezo katika fainali ya ligi
ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2013/2014 iliyoshuhudia Real madria ikitwaa
taji la 10 (La Decima) la michuano hiyo, bado anaona anahitaji kushinda taji
akiwa na jezi ya timu ya taifa kwani ni jambo la heshima na kubwa kwake kuliko
chochote katika soka.
Angel Di maria (kulia) akiwa na wachezaji wenzake Sergio Ramos (katikati) na Pepe (kushoto) wakiwa na 'ndoo' ya ligi ya mabingwa walioshinda msimu wa 2013/2014 jijini Lisbon |
“Nadhani ningeweka rehani kila kitu nilichoshinda katika
maisha yangu ya soka kwa ajili ya kushinda kitu nikiwa na timu yangu ya taifa,”
alisema Di maria.
Licha ya kushinda kombe la dunia kwa vijana chini ya miaka
20 (world cup U20) mwaka 2007 na kufunga goli la ushindi lililoipa Argentina
chini ya umri wa miaka 23 medali ya dhahabu katika michuano ya Olympic
iliyofanyika Beijing mwaka 2008, bado Angel Di maria hajaonja ladha ya taji
akiwa na timu ya taifa ya wakubwa ya Argentina.
“Hakuna ufananisho. Kila kitu unachoweza kushinda katika
klabu ni cha pekee. Kushinda ligi ya mabingwa ilikuwa ni jambo bora kuwahi
kutokea kwenye maisha yangu, lakini sidhani kama kuna kitu kinaweza kufanana na
mimi kushinda kitu na timu yangu ya taifa,” alisisitiza Di maria.
Di maria alikuwemo kwenye kikosi cha Argentina
kilichoshiriki kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014 na kuambulia nafasi ya
pili baada ya kuusaliti ubingwa kwa Ujerumani katika dakika za nyongeza licha ya yeye kutokuwepo kwenye mchezo huo wa fainali, lakini ilikuwa pigo kwake kama
ilivyokuwa kwa Waargentina wengine.
“Mamilioni ya Waargentina walifurika wengine wakilala kwenye mitaa Brazil. Wengi
walikosa tiketi lakini hawakujali. Waliacha mamilioni ya vitu kuja kutona sisi
na kutuunga mkono. Hatukuweza kushinda lakini tulionesha kila kitu uwanjani. Na
ndio maana sioni cha kufananisha,” aliongeza winga huyo.
Di maria akishangilia goli katika michuano ya kombe la dunia 2014 nchini Brazil |
Mbali na matamanio yake hayo, Di maria anajiona miongoni mwa
watu wenye bahati duniani hususani katika mchezo wa soka kwa kucheza pamoja na
miamba miwili ya soka duniani kwa sasa, Cristiano Ronaldo (Real Madrid) na
Lionel Messi (Argentina)
“Nakosa maneno sahihi ya kulielezea hili. Nimecheza na watu
wawili bora duniani kwa sasa, Leo (Lionel Messi) na Cristiano (Ronaldo). Nimekuwa
na bahati kucheza na wachezaji wawili ambao bado wanapigania kuwa bora duniani.
Ni kitu ambacho wachache wamekipata au asiwepo kabisa aliyekipata,” alimalizia
Di maria.
0 comments:
Post a Comment