Wakati vita ya usajili kuwania wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara ikiwa imepamba moto, timu ya African Sports ya jijini Tanga imefanikiwa kuwasajili wachezaji wawili kutoka timu ya Mgambo JKT.
Katibu wa ‘Wanakimanumanu’ Khatibu Enzi amesema, zoezi hilo limeendelea vizuri na wameanza mazoezi tangu wiki mbili zilizopita, lakini bado wanaendelea na mchakato wa kumtafuta mwalimu wa kuunganisha kikosi cha timu hiyo.
“Tumemnasa beki wa Mgambo, kadhalika tuna mchezaji anaitwa Mavuo na yeye anatokea Mgambo, sasahivi tupo kwenye mazungumzo ya mwishomwisho na Bakari Masoud ambaye aliwahi kuwa Yanga na Coastal Union, muda wowote tunaweza kumalizana nae". amesema Enzi.
“Hatutochukua mchezaji kutoka Simba wala Yanga kwasababu inakuwa ni tatizo tunavyoangalia katika upeo wetu, wachezaji kuwatoa katika timu hizo bado inakuwa ni tatizo, bado wana mapenzi. Simba ,.Yanga ni timu kubwa, nadhani asilimia kubwa ya wachezaji wanamapenzi na timu hizo kwahiyo wanakuwa ni wepesi kuihujumu timu,” amefafanua.
“Mpaka dakika hii kuna kijana anaitwa Ally Manyani ambaye ni kocha msaidizi ila tunatafuta mwalimu mkuu ambaye bado hatujakuwa na msimamo kama atakuwa ni nani, mchakato wa kumtafuta mwalimu ulianza na tayari tulikuwa kwenye mazungumzo na Shime lakini baada ya mwalimu Shime kukabidhiwa timu ya Taifa kidogo mazungumzo yamekwenda tofauti, kwahiyo tunaangalia wapi tena pakulenga ili tupate kocha ajekuwa mwalimu mkuu,” alimaliza.
0 comments:
Post a Comment