UONGOZI wa Yanga umesema winga wake machachari na mfungaji bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015, Simon Happygod Msuva ataadhibiwa kwa kitendo chake cha kutoroka kwenda Afrika kusini kufanya majaribio katika klabu ya Bidvest Wits inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo.
Katibu mkuu wa Yanga, Dr. Jonas Tiboroa amesema Msuva aliyefunga magoli 17 msimu uliomalizika mei 9 mwaka huu bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu klabuni hapo, hivyo wameandika barua kwenda FIFA kuilalamikia Bidvest iliyozungumza na mchezaji mwenye mkataba kinyume na sheria za usajili.
"Mchezaji anatoroka kwenda kufanya majaribio, akirudi wewe utamfanyaje? kwanza timu ile haijaleta ofa wala chochote, sisi tunasikia kwenye magazeti kwamba bei yake ni dola laki moja, laki mbili mara laki tano, nani kasema? nani kaleta ofa? ofa iko wapi? au Msuva mwenyewe amewaambia kuwa kasajiliwa kule? ', Amehoji Tiboroa na kuongeza:"Tunazo sheria zinaongoza usajili wa mchezaji hususani mwenye mkataba, kama tunamzuia mchezaji mwenye mkataba kuongea na jirani zetu wa hapo karibu (Simba) kwanini isiwe Bidvest Wits ya kule Afrika kusini? tena mchezaji mwenye mkataba wa mwaka mmoja na nusu?
Je, Yanga wamechukua hatua gani dhidi ya Bidvest Wits?
Dr. Tiboroa amesema: "Sisi tumeandika barua kwenda FIFA tukilalamika kuwa Bidvest wameongea na mchezaji wetu bila ruhusa, sisi tunataka maendeleo ya klabu hii, mkifuata maneno ya mtaani kwamba Yanga wanawazuia wachezaji kutoka sio kweli".
Je, Msuva anaadhibiwa na Yanga?
Tiboroa amefafanua: "Suala la Msuva sisi kama klabu tumekaa, hivi ninavyosema ninaandika ripoti yake kwenda kamati ya utendaji na tutakaa kujadili adhabu yake, lakini hiyo adhabu haimzuii kuendelea na mchakato wa kuendelea kujiunga na hiyo timu endapo timu ya Bidvest italeta ofa, Yanga haitamzuia mchezaji yeyote kwenda kokote anakotaka"
0 comments:
Post a Comment