MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga wanatarajia kupata vifaa vya nguvu kutoka katika klabu za Zesco ya Zambia na Benfica de Luanda ambao ni ndugu wa wababe wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika 2013, FC Libolo ya Kongo.
Libolo FC iliitoa Simba kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-0 katika michuano hiyo ya CAF, ikiwa ni baada ya Wekundu wa Msimbazi hao kulala bao 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kupigwa 4-0 ugenini.
Yanga imepania kusuka kikosi cha nguvu kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, ikiwa na malengo ya kufanya vyema katika michuano ya ndani na ile inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Msimu ujao kwenye anga ya kimataifa, Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni baada ya kutwaa ubingwa wa Bara msimu huu.
Kwa kufahamu ugumu wa michuano hiyo, Yanga imeona ni vema ikapiga hodi katika klabu kadhaa kubwa barani Afrika ambapo mbali ya hizo mbili, pia itachungulia katika kikosi cha APR ya Rwanda.
Tayari Yanga wamefanikiwa kumshawishi straika wa FC Platinum ya Zimbabwe, Donald Ngoma, ambaye anatarajiwa kutua nchini Jumatatu kumaliziana na klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Kati ya wachezaji inaowawania katika vikosi hivyo, yupo kiungo hatari wa Miguel na washambuliaji wa timu hiyo, Massinga na Fabricio wote wa Benfica Luanda.
Kwa upande wa Zesco iliyochafua sherehe za Tamasha la Simba Day 2014 kwa kuifunga timu hiyo mabao 3-0 na Wekundu wa Msimbazi hao kumtimua kocha wao, Zdravko Logarusic, Yanga wanataka kung’oa nyota wao wawili au zaidi ya hao.
Miongoni mwa nyota wa timu hiyo wenye uwezo wa kukipiga Yanga ni Innocent Mwaba, Winston Kalengo na Humphrey Maseneko.
Chanzo:Bingwa
0 comments:
Post a Comment