Kocha wa Chelsea Jose Mourinho amekataa kuruhusu wala kujibu swali lolote kutoka kwa waandishi wa habari ambalo lilikuwa likimhusu kocha wa Arsenal, Arsene Wenger hasa baada ya Wenger kumwambia kuwa hana heshima.
Wenger alikasirishwa na kitendo cha Mourinho kutoa majibu ya kuudhi hasa baada timu hizo mbili mahasimu wa jiji la London kutoa suluhu katika dimba la Emirates kwa kusema “Kinachokera ni kukaa miaka 10 bila ya kombe na si mpira wanaocheza Chelsea”, wakati huo huo akiwakashifu namna Arsenal walivyotolewa na Monaco katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.
Wenger alimjia juu Mourinho na kusema kuwa baadhi ya makocha wahahitaji kuonesha heshima dhidi ya makocha wengine, huku kauli hiyo akiilenga moja kwa moja kwa Mourinho.
"Kitu kikubwa kabisa kwa makocha ni kuheshimiana, sasa baadhi yao nadhani wanatikiwa kujirekebisha kwa hilo," Wenger alisema.
"Kila mtu ana matatizo yake yanayomsibu, sasa mimi matatizo yangu yananitosha mwenyewe."
Mourinho alipoulizwa kuhusu maneno ya Wenger, alirusha mikono yake na kukatiza maswali yaliyolenga hiyo maada akimaanisha kuwa hakuwa na mpango wa kujibu chochote juu ya hilo.
Ikumbukwe kuwa Mourinho na Wenger wamekuwa mahasimu kwa muda mrefu na hata kufikia hatua ya kukunjana mashati katika mchezo baina ya timu zao uliopigwa Uwanja wa Stamford bridge mwezi wa kumi mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment