Wednesday, May 20, 2015

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imechapwa mabao 2-0 na Madagascar katika mechi ya pili ya kundi B ya michuano ya Cosafa iliyomalizika usiku huu.
Hiki ni kipigo cha pili kwa Stars kwani mechi ya ufunguzi iliyopigwa juzi walichapwa 1-0 na Swaziland.
Kwa matokeo hayo, Madagascar wanaendelea kuwa vinara wa kundi B kwa kupata pointi zote sita katika mechi mbili za kundi B, wakifuatiwa na Swaziland walioshinda 1-0 dhidi ya Stars.
Lesotho waliochapwa 2-1 na Madagascar mechi ya kwanza wanachuana na Swaziland usiku huu majira ya saa 2:30 kwa saa za Tanzania.
Stars wanaendelea kuburuza mkia kundi B,  juu yao wapo Lesotho ambao hawana pointi, lakini wamefunga angalau goli moja na Stars hawajafunga goli lolote katika mechi mbili walizocheza mpaka sasa.
Kwa matokeo hayo, Stars imetupwa nje ya michuano kwasababu hata wakishinda magoli 100-0 dhidi ya Lesotho mechi ya mwisho, tayari Madagascar  wamefikisha pointi 6 ambazo Stars hawezi kuzifikia na wana mchezo mmoja mkononi,
Timu pekee inayoweza kufikisha pointi 6 ni Swaziland ambayo inacheza leo na Lesotho.
Kama Swaziland watashinda leo, maana yake fainali ya kundi B itakuwa kati yake na Madagascar ili kupata mshindi mmoja wa kwenda robo fainali, wakati Stars na Lesotho watakuwa wanachoma ‘mahindi’ nyumbani.
Magascar walishindi 2-1 katika mechi ya kwanza ya kundi B dhidi ya Lesotho, kwahiyo waliingia katika mechi ya leo dhidi ya Stars wakijua nini cha kufanya.
Kwanza walikuwa na mpango wa kufunga magoli ya mapema ili kujiweka mazingira mazuri ya kushinda na kwa bahati nzuri walifanikiwa kufunga goli dakika ya 13 ambalo liliwaondoa mchezoni Taifa Stars.
Stars walifungwa goli hilo kwa shambulizi la kushitukiza (Counter-attack) wakipitia upande wa kushoto ambako amecheza Oscar Joshua.
Katika kipigo cha Stars cha 1-0 dhidi ya Swaziland, Oscar alichemsha mno upande wa kushoto, leo amerudia tena kucheza chini ya kiwango ingawa hastahili lawama zote kwasababu kuna wachezaji wengine walioshindwa kutekeleza majukumu yao.
Licha ya makosa kuanzia safu ya kiungo ambapo Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla na Salum Abubakar walishindwa kupunguza kasi ya shambulizi la kushitukiza la Madascar, Oscar alikuwa amepanda sana, lakini kurudi ikawa mtihani.
Winga wa Madagascar alikimbia kupiga krosi wakati Oscar ambaye hana kasi siku zote akishindwa kurudi kwenye eneo lake kwa haraka na kumpa urahisi mpigaji krosi.
Kwa bahati nzuri Salim Mbombe, Aggrey Morris, na Mwinyikazimoto walifika eneo lao haraka, lakini nao wakashindwa kuwa na utashi mzuri.
Badala ya mmoja kumwangalia mpiga krosi na wengine kufanya maarifa ya kumzuia mshambuliaji, wote wakapeleka akili kwa mpigaji krosi na mfungaji wa goli akakaa eneo zuri bila usumbufu, alipopata mpira wa krosi alifanya kazi rahisi kumfunga Deogratius Munishi ‘Dida’.
Mazingira yale yale ya goli la kwanza, Stars walifungwa goli la pili kwa aina ile ile ya shambulizi la kushitukiza.
Huwezi kumlaumu moja kwa moja Oscar,  kwasababu Stars imefanya vibaya safu ya kiungo hususani kiungo wa Ulinzi alipocheza Sure Boy.
Sijui Nooij aliingia na akili gani, lakini kwa kawaida Sure Boy hana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi. Yeye na Kazimoto walishindwa kuwasaidia mabeki wa kati, Mbonde na Aggrey, hivyo mashambulizi ya hatari ya kushutukiza ya Madagascar yamefanya kazi nzuri kipindi cha pili.
Kutokana na Stars kukosa kiungo wa ulinzi asilia, ndipo mawazo ya wengi kumtaka Jonas Mkude (Simba) yanaonekana kuwa ya maana.
Kipindi cha pili Nooij alimtoa Mrisho Ngassa na kumuingiza Simon Msuva, pia akamtoa Said Ndemla na kumuingiza Shomari Kapombe.
Pia alimtoa Juma Luizio na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Hajib Migomba.
Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kidogo kwa Stars, lakini bado hawakuweza kutengeneza mipango mizuri ya kufunga magoli.
Kapombe na Msuva mara kadhaa walijitahidi kulazimisha kuingia na kupiga mipira ndani, lakini ‘Uchovu’ wa John Bocco aliathiri mipango hiyo.
Madagascar waliingia kipindi cha pili kwa staili ile ile, walipanga mashambulizi ya kushitukiza, walikaba kitimu, walijua maeneo muhimu ya kuwazuia Stars yaani kiungo ili kutoshambuliwa.
Wataalamu wa mpira wa miguu wanasema wachezaji wanaishi kwenye kivuli cha kocha, wanacheza kuakisi mbinu na ufundi wa kocha wao na ndio maana timu inapoboronga, kocha ndiye mtu wa kwanza kuwajibika.
Kocha  anafukuzwa, wachezaji wote wanaweza kubaki, lakini kwa Bongo baadhi ya wachezaji pia wanaweza kupewa adhabu timu inapofanya vibaya ikiwemo kusimamishwa kama inavyotokea kwa Simba na Yanga.
Wachezaji wa Taifa Stars waliowengi hawako fiti na kwa bahati mbaya hawajaandaliwa vya kutosha, lakini inafika wakati unaweza kuhoji uwezo wa kocha Nooij kwa namna timu yake inavyocheza pamoja na uteuzi wake.
Mbinu  na ufundi wake umefeli kwa soka la Tanzania ingawa ni kocha mzuri, hana namna ya kukwepa lawama. 
Timu haina uwezo wa kukaba inapopoteza mpira, mipango ya upigaji wa mipira ya kutenga ni mibovu, wachezaji hawajui wakae wapi na wafanye nini inapotakiwa kufanya maamuzi ya haraka hususani safu ya kiungo na ulinzi.
Mtu kama Erasto Nyoni amekosa kasi kwasababu hajacheza mechi za mwisho za ligi kuu kutokana na majeruhi, nadhani kocha angeweza kuangalia wachezaji wengine kama akina Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), David Luhende (Mtibwa), Hassan Kessy (Simba), Juma Abdul (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City).
Hawa ni baadhi ya vijana waliocheza kwa kiwango kikubwa mno msimu uliomalizika mei 9 mwaka huu, lakini washambuliaji pia ni shida. Unamuachaje Rashid Mandawa aliyefunga magoli 10 na kumchukua John Bocco ambaye amefunga magoli matatu tena anasumbuliwa na majeruhi?
Naheshimu mtazamo wa Nooij, lakini ilikuwa nafasi nzuri ya kujaribu vipaji vipya katika  ‘Bonanza’ la Cosafa kwasababu baadaye timu inakabiliwa na michezo migumu zaidi ya kufuzu CHAN na AFCON.
Kama wachezaji hawa ambao wamezoeleka watacheza hivi hivi kwenye mechi za kufuzu michuano ya Afrika hapo baadaye, Nooij hatafika popote.
Hata kama atapata wachezaji wengine wanaopendekezwa na wataalamu wa soka,  muda wa maandalizi utatosha? Naamini hakukuwa na ulazima wa kuwaita baadhi ya wachezaji kama Oscar Joshua, Erasto Nyoni, John Bocco, Amri Kiemba na wengineo. Ni wachezaji wazuri, lakini kuna wengine waliochipukia na kufanya kazi zuri.
Mart Nooij anapaswa kupewa muda zaidi wa kuifundisha Taifa Stars au imefika wakati wa kumuondoa?
Nitumie maoni yako, kosoa mtazamo wangu

Na Baraka Adson Mpenja
Mtangazaji wa Mpira wa Miguu-Azam TV

Tel: 0712461976

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video