Brendan Rodgers amekiri kuwa kikosi chake kimekosa ubora na mtu sahihi wa kuongoza kikosi hicho ndani ya uwanja na kuongeza kuwa kuondoka kwa Gerrard ndio kunazidi kuacha pengo kubwa.
Liverpool walifungwa na Crystal Palace 3-1 katika mchezo ambao Gerrard ndio alikuwa anawaaga rasmi mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwa ndio ulikuwa mchezo wa mwisho kupigwa kwenye uwanja wa Anfield kwa msimu huu wa Ligi kabla ya kuelekea Marekani katika klabu ya LA Galax.
Japokuwa Liverpool walimaliza katika nafAsi ya pili msimu uliopita lakini Rodgers amesema kuwa kwa sasa kikosi hicho kinakosa ubora wa ushindani.
“Hicho ndicho tunachopaswa kukitafutia majibu,” alisema. “lazima utafute suluhisho, timu imekosa mbinu za kiutawala uwanjani na ubora pia, kitu ambacho ninatakiwa kukitizama kwa undani sana.
“Stevie ana hamasa kubwa sana uwanjani na katika vyumba vya kubadilishia nguo na hivyo kuipa ubora timu. Bila shaka ni kitu ambacho kitakosekana baada ya kuondoka kwake, lakini kama unataka kuwa mchezaji mkubwa katika timu kama hii ni lazima ujitume na utoe mchango mkubwa katika michezo mikubwa.
“Na huo ndio mpango wetu msimu ujao. Nina uhakika tutalifanyia kazi hilo.
0 comments:
Post a Comment