Beki wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza Rio Ferdinand ametangaza rasmi kutundiga daluga kusakata kabumbu.
Rio aliachwa na QPR baada ya klabu hiyo kuteremka daraja msimu huu.
QPR:imewaacha Joey Barton, Rio Ferdinand na Bobby Zamora.
Ferdinand, ambaye ni nahodha wa zamani wa Uingereza, kwa sasa ameamua rasmi kuachana na mchezo wa soka na kuanza maisha mapya uraiani.
Rio ameiambia BT Sport hivi“Baada ya miaka 18 ya kusakata kabumbu kama mchazaji wa kulipwa, sasa nimeona ni muda muafaka kwangu kustaafu mchezo huu ninaoupenda zaidi."
“Nikiwa kama mtoto wa miaka 12, niliweza kupiga mpira kule Friary Estate ambayo ipo Peckham, sikuwahi kuwa na ndoto ya kuichezea timu ya West Ham,timu ambayo ndio nilianzia maisha pale, nimewahi kuwa nahodha wa Leeds United, nimeshinda kombe la klabu bingwa Ulaya nikiwa na Manchester United, na kuungana kwa mara nyingine tena na kocha wangu wa kwanza Harry Redknapp hapa Queens Park Rangers.
“Siku zote nitaheshimu michezo 81 ambayo nimejumuika na timu ya taifa ya Uingereza, nikijivunia sana fahari hiyo. Hizi zote ni kumbukumbu ambazo kamwe hazitosahaulika katika maisha yangu.
“Ukianza taaluma yoyote ile, kila kijana anahitaji mtu wa karibu wa kumshauri. Nilijikuta niko mikononi mwa Dave Goodwin, Meneja wa Wilaya huko Blackheath, na Tony Carr, meneja wa timu ya vijana ya West Ham. Walinipa mafunzo mema ambayo yamedumu kwa takribani kipindi chote nilichokuwa katika mchezo wa soka. Nitaendelea kuwaheshimu daima.
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Chris Ramsey, Harry Redknapp, David O'Leary na David Moyes ambao waliniwezesha katika nyakati tofauti katika maisha yangu ya soka, bila ya kusahau wafanyakazi wengine katika timu ambao walionyesha kunijali kwa miaka yote, na pia wachezaji wote ambao nimewahi kucheza nao. Pia ningependa kutoa shukrani kwa timu iliyonisaidia wakati nikiwa nje ya mchezo huu, Jamie Moralee na kila mtu katika kipindi hiki kipya ninachokianza rasmi.
“Kushinda makombe kwa kipindi cha miaka 13 nikiwa na klabu ya Manchester United ilinifanya nifanikiwe kila kitu nilichokuwa nikikitamani katika tasnia ya soka. Tangu utotoni mpaka wakati huu, hicho ndicho nilichokuwa nikikiwaza mara zote.
“Vyote hivyo sidhani kama vingewezekana bila ya kiungo muhimu kabisa ambaye ni, Sir Alex Ferguson. Upeo wake mkubwa katika macho yangu utaendelea kudumu daima. Kwa mtazamo wangu yeye ndiye atabaki kuwa kocha bora kabisa katika historia ya mpira wa Uingereza.
“Pia ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa mke wangu Rebecca na familia yangu, akiwemo mama na baba yangu, kwa kujitolea maisha yote juu yangu, na pia faraja na ushauri wao waliokuwa wakinipa kwa kipindi chote nilichokuwa nikisakata soka.
“Na mwisho kabisa, ningependa kuwashukuru mashabiki wote katika klabu zote - kwani bila yao mpira huu uliojaa utaalamu wa hali juu usingekuwepo. Nitamkumbuka kila mmoja wenu kwenye jioni hii ya siku ya Jumamosi.”
0 comments:
Post a Comment