Hans Poppe |
UONGOZI wa Simba umethibitisha rasmi kuachana na aliyekuwa
kocha mkuu wake, Mserbia Goran Kopunovic baada ya kushindwa kufikia makubaliano
juu ya mkataba mpya.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans
Poppe amesema Kopunovic ameshuka kidogo mno kwenye dau alilotaka na Simba
wameshindwa kufikia uwezo huo.
“Amebaki palepale, ameshuka kidogo sana, tumeona atafute
maslahi ya namna hiyo kwenye timu nyingine, sisi hatuwezi kufikia. Unaweza
kusema hakushuka kabisa, yaani katika hela zote alizotaja ameshuka kwa dola
elfu tano tu”. Amesema Hans Poppe na kuongeza: “Tumeshaona makocha karibu sita
kutoka Serbia, Hungary, Bulgaria na Burundi pia tunaangalia, kuna kocha ambaye
CV zake ni nzuri”.
Goran Kopunovic
Hans Poppe ameongeza: “Hatudaiani na Kopunovic, mkataba wake
umekwisha. Mrithi wa Goran ndani ya wiki moja tutakuwa tumempata. Atakakuja
kocha tu, wasaidizi wataendelea walewale, hatukupenda kubadilisha, lakini
bahati mbaya tumeshindwa kuafikiana, amekwenda juu mno tofauti na matarajio yetu,
tungependa kuendelea na Kopunovic, ni kocha mzuri, ameifundisha timu vizuri”.
Kopunovic alitaka mshahara
mkubwa wa dola za Kimarekani elfu tisa (9,000) sawa na shiloingi milioni 18 za
Kitanzania.
Pia anataka dau la kusaini la
dola za kimarekani elfu hamsini (50,000) sawa na shilingi million 100 za
Kitanzania.
Taarifa zilizoripotiwa jana
ni kwamba kocha Mbelgiji, Piet de Mol atatua Dar es Salaam Mei 21,
mwaka huu kwa ajili ya mazungumzo ya kuifundisha Simba SC.
Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, De Mol mwenye umri wa miaka 60 ana uzoefu
mkubwa wa kufundisha soka Afrika, Asia na Ulaya na alikuwa nchini Ghana
akifanya kazi ya Mkurugenzi wa Ufundi wa akademi mjini Kumasi. Pia alifanya kazi na Asante
Kotoko. Pia alifundisha timu ya kwao Ubelgiji, Dubai, Qatar na China. Alikuwa
kocha Msaidizi wa AA Gent kuanzia mwaka 1997 hadi 2001.
Naye kopunovic leo akiwa Hungary amethibitisha
kushindwana na Simba, lakini amedai kuwa atakuwa shabiki mkubwa wa timu hiyo
kwani hakupenda kuondoka.
Simba imekosa kushiriki michuano ya kimataifa kwa miaka mitatu, kwa mara ya mwisho ni mwaka 2012 walipotwaa ubingwa wa Tanzania.
Moja ya sababu kubwa Simba kuchemsha katika michuano ya ligi kuu ni mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha.
Toka walipochukua ubingwa 2011/2012 chini ya kocha Maserbia Milovan Circovic, Simba imepitia mikononi mwa Mfaransa Patrick Liewig, Mzawa Abdallah Kibadeni, Mcroatia, Zdravko Logarusic, Mzambia Patrick Phiri na sasa wameachana na Mserbia, Goran Kopunovic.
0 comments:
Post a Comment