John Bocco (kulia) ameshindwa kuonesha makeke kwenye michuano ya Cosafa
AWALI ya yote nianze kwa kumpongeza nahodha wa timu ya taifa
ya Tanzania, Taifa Stars katika michuano ya Cosafa inayoendelea huko Afrika
kusini, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
Bocco ameandika makala ndefu na kuiweka kwenye akaunti yake
ya facebook na mtandao huu imeichapisha kama ilivyo asubuhi ya leo, akijaribu kueleza masikitiko yake juu
ya soka la Tanzania linalozidi kuporomoka kila sekunde, hususani kuboronga kwa
Taifa Stars.
Nimeisoma makala hiyo kwa umakini na kurudia mara nyingi,
hatimaye nimeguswa na namna Bocco anavyojua sababu za soka la nchi hii kushuka
kila kukicha. Hata Swaziland na Madagascar hatuwawezi kwasasa? Hii ni fedheha.
Mshambuliaji huyo wa Azam fc ni miongoni mwa wahanga wa
matokeo mabovu ya Taifa Stars kule Afrika kusini, hawezi kukwepa lawama kutokana na kiwango
kibovu alichoonesha katika safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars.
Bocco hayuko fiti hata kwa asilimia 40, amesumbuliwa na
majeruhi kwa muda mrefu, hajacheza katika timu yake ya Azam fc, amefunga magoli
matatu tu. Hata kocha wake anajua hayuko fiti, lakini Mart Nooij ameona yuko
fiti, jiulize mwenyewe utapata jibu.
Wapenda michezo wengi wamemponda Bocco na bila shaka amekuwa
akisoma kwenye mitandao ya kijamii jinsi anavyoshambuliwa. Kwa binadamu yeyote
ambaye hana moyo wa chuma, lazima aumizwe na matusi, kejeli zinazotolewa na
mashabiki kuihusu Taifa Stars.
Ukiyapima maandishi ya Bocco, unagundua kwa haraka kwamba
kuna kitu kipo kichwani mwake. Matusi yamemuumiza sana na ili kujaribu
kupungumza mzigo uliopo moyoni mwake ameamua kueleza baadhi ya sababu
zinazoathiri soka la Tanzania, mathalani;
1.
Kutokuwa
na program za kuendesha mpira kisasa
2 .
Kutokuwa na misingi endelevu ya kuendesha
wachezaji wadogo kisasa
3.
kutokuwa na ligi kuu bora nchini .
4.
Kuwa
na uhaba wa wachezaji wanaocheza nje ya nchi ndani ya timu ya TAIFA
5.
Kutothamini
na kuheshimu wachezaji wakitanzania walio ndani ya ligi yetu na nje ya ligi
yetu etc.
Hizi ni sababu alizotaja Bocco na kuzielezea vizuri kwenye
makala yake (soma tena makala hiyo), lakini katika maelezo yake amegusia mambo mengi
ikiwemo kukosekana kwa mfumo wa soka la vijana, miundo mbinu mibovu ya mpira,
waamuzi wabovu, viongozi wa kizamani, makocha wa kizamani ndani ya soka la nchi
hii n.k.
Mengi aliyosema Bocco yanasemwa pia na makocha, wachambuzi
na waandishi wa habari. Elimu ya kutosha
kuhusu namna ya kutengeneza mfumo wa soka la vijana, falsafa ya nchi, namna ya
kutafuta makocha na wachezaji wa timu ya Taifa imeshatolewa sana , lakini kwa
bahati mbaya viongozi wanaohusika wamekuwa wakipuuza maoni hayo kwasababu wanaendesha soka
kwa maslahi binafasi.
Kutokana na makala ya Bocco, nimeamua kumpongeza kwa moyo
wote. Nimeona mara nyingi makala za wachambuzi na waandishi wenzangu na
ninaendelea kuziona, lakini makala za wachezaji waliopo kwenye mpira kwasasa
kama Bocco ni adimu mno.
Bocco ameniaminisha kuwa kuna wachezaji makini, wanajua vitu
vingi, lakini wanashindwa kusema kwasababu wanawaogopa viongozi wao ambao
hawapendi kuambiwa ukweli, wanaendekeza chuki, uzandiki na visilani. Je, kwa
viongozi hawa, mchezaji akisema ukweli atacheza mpira? Sina hakika!.
Nigusie kidogo kuhusu makocha wazawa; inawezekana kabisa makocha hawa wamekuwa wagumu kujifunza vitu vipya. Kwa wanaotumia
‘Smartphone’ lazima wanakutana na jumbe za mara kwa mara zikiwataka ‘wa-update
programs’ mbalimbali ndani ya simu zao.
Unapoambiwa ‘update program’ maana yake kuna maboresho yamefanyika,
wataalamu wanahangaika usiku kucha kuboresha na kubuni vitu vipya. Hata katika soka, sheria
kwa asilimia karibu zote zimeendelea kuwa zile zile, lakini kadri mpira
unavyoendelea duniani, kumekuwa na maboresho ya sheria hizo ili kuendana na usasa.
Ndio maana waamuzi na makocha wa mbele wamekuwa wakijifunza
kila kukicha, je, wakwetu Wana-update akili zao? Au bado wapo kwenye uzamani unaosemwa na Bocco?
Binafsi naamini wapo wanaojifunza mbinu mpya kila siku na
kuna wengine wamebaki kwenye uzamani. Ukienda kwenye program za mazoezi ya timu
za ligi kuu, ligi daraja la kwanza utagundua kama makocha wetu wamebaki kwenye
uzamani au wana usasa.
Kuna wengine wanaendana na usasa, ila kuna wengine
wameendelea kufundisha mpira wa kizamani, kuna haja ya kubadilika katika hili.
Ishu nyingine niliyoguswa nayo ni waamuzi; Bocco anadai sio wazuri , wanachezesha kizamani na
wakienda kucheza mechi za kimataifa wanakutana na waamuzi wazuri na wakisasa na
ndio maana timu za Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa zinapata kadi
nyingi, offside nyingi, mwisho wa siku zinafungwa kwasababu walishazoeshwa
vibaya na marefa wa ligi yetu.
Bocco
anasisitiza kuwa huwezi kupata mchezaji mzuri wa Timu ya taifa kutoka kwenye ligi mbovu isiyo na viwanja bora,
mipira bora, uongozi bora, marefa bora wala mashabiki bora.
Amini usiamini!
Bocco anayo siri kubwa sana kuhusu waamuzi! Kiukweli kuna madudu mengi
yanayofanywa na waamuzi, wengine si kwa kupenda. Kuna rushwa inatembea vibaya
mno. Sio kweli kwamba waamuzi wetu hawajui sheria za kisasa, wanajua sana
kwasababu sheria hazibadiliki sana zaidi ya kuboreshwa.
Baadhi ya makosa
ya makusudi wanayofanya waamuzi ni maelekezo
ya watu fulani, kuna waamuzi wanaondolewa kwenye ratiba ya mechi kadhaa kwasababu
ya misimamo yao. Akikataa rushwa ili apange matokeo, basi utasikia wamefanya
mabadiliko. Kuna watu wanataka mambo yao yatimie kidhuluma.
Nimejifunza
mengi katika mechi za mwisho za ligi kuu soka Tanzania bara msimu 2014/2015
uliomalizika mei 9 mwaka huu. Waamuzi
wametumika mno, timu nyingine zimepata nafasi za juu kwasababu ya mipango, timu
nyingine zimeshushwa daraja kidhuluma.
Bocco anajua
haya, lakini hawezi kusema kiundani zaidi ya kusema waamuzi wanachezesha
kizamani. Waamuzi wengine wana mapenzi na timu za Simba, Yanga, wanachezesha
kiunazi, lakini waliowengi ni wala rushwa. Kinachouma zaidi ni kwamba; wanaohusika kupanga matokeo ni watu wanaoonekana makini mbele ya jamii.
Inashangaza
sana kuona kiongozi mkubwa wa soka anatoa maelekezo Ruvu Shooting ashuke
daraja kwa maslahi ya watu fulani, Yanga ipate ushindi, Azam ipate ushindi au Mgambo wapewe
pointi, Ndanda wabakishwe ligi kuu kwasababu za kisiasa.
Waamuzi wanaelekezwa nini cha kufanya, akijifanya
anapenda ‘Fair Play’ hapangwi kwenye mechi .
Waamuzi
wanavuna mamilioni kwasababu ya rushwa, wanapiga vimeo vingi vya ligi kuu na
kuendesha maisha. Wanajua wanachokifanya na wanaposoma hapa wanasutwa nafsi
zao.
Kuhusu viongozi
wa kizamani ni kweli kabisa. Kiongozi bora ni yule anayekubali kujifunza. Siku
zote wanaojifanya wanajua wana-feli vibaya mno. Ulimwengu unabadilika, mambo
yanabadilika kila siku, lazima ujifunze kwa wengine.
Kwa habati
mbaya viongozi wengi wa soka kuanzia ngazi za chini mpaka TFF wanajifanya
wataalamu wa soka, hawashauriki, wanaamini katika mawazo yao, hawajifunzi wala
kupokea maoni ya wengine, madhara yake wanafeli.
Hata kocha wa
Taifa Stars, Mart Nooij anajiamini kupita maelezo, anajiona ndiye bora kuliko
wote, lakini kama angekuwa bora angekuja kuganga maisha Bongo?
Kuna watu wa
maana wapo nchi hii, wanajua mpira mno, wana uzoefu mkubwa, lakini huyu mzungu hata
kuwasalimia na kubadilishana mawazo hataki, anaamini anaweza kuliko wote.
Hawezi hata
kumpigia simu Hans van der Pluijm wa Yanga kujua hali ya kiafya ya Said Makapu,
Nadir Haroub inaendeleaje. Matokeo yake
anachaguo hata wachezaji majeruhi kwenye kikosi cha timu ya taifa.
Nooij hawezi kuifikisha
Tanzania popote kwasababu ya kiburi chake, Kim Paulsen alikuwa mtu wa watu,
alipenda kujifunza, lakini Malinzi akamuondoa bila sababu za msingi.
Inawezekana
kweli makocha wa ndani ni wa kizamani, lakini si kwa kiwango hicho. Kila siku
tunasikia kozi za makocha na wakati mwingine wakufunzi wanatoka CAF na FIFA,
makocha wetu wanajua sana, lakini hawathaminiwi.
Mtu mweupe
ndiye bora, hivyo ndivyo tunaamini. Lakini ukweli ni kwamba Hans van der
Plujim, Goran Kopunovic akikutana na Juma Mwambusi, Bakari Shime uwanjani,
waamuzi wakawa ‘fair’ asilimia 100, utagundua kuwa hawana utofauti mkubwa
katika uwezo wa kufundisha mpira.
Vitabu vya
mpira ni vile vile, ndio maana hata mzungu mzaliwa wa Uingereza anaweza kufeli
somo la kiingereza licha ya kuwa lugha yake mama. Kwa waliosoma na wazungu wana
ushahidi wa kutosha, wanazidiwa na waafrika katika mambo mengi, lakini kwa
bahati mbaya waafrika hatujikubali na hatukubaliki na waafrika wenzetu.
Kuna kocha yeyote
mzungu amewahi kuja Tanzania katika ngazi ya klabu na kujaribu kusogelea rekodi
ya Mfalme Abdallah Kibadeni pale Simba na Tanzania hii?
Huyu nidye
kocha pekee aliyeifikisha Simba kwenye fainali ya kombe la CAF, siku hizi kombe
la Shirikisho. Rekodi hiyo haijawahi kufikiwa wala kusogelewa na kocha yeyote
awe mzungu au Mtanzania katika timu zote za Tanzania. Unaanzaje kumdharau Kibadeni? Ndiyo! Unaweza
kusema ana uzamani kwa mtazamo rahisi tu, lakini ni kwamba yule ni mtu muhimu
mno.
Bocco kaongea
mengi, sijataka kurudia wala kuongeza. Lengo langu ni kumpongeza tu na
kujaribu kugusia baadhi ya mambo aliyosema!
Hongera sana! John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ kwa kutueleza hisia zao na ukweli wa soka letu. Viongozi chukueni maoni yake, sio dhambi kuyafanyia kazi.
Ni halali yako
kutoa maoni, kukosoa mtazamo huu binafsi!
Na Baraka Adson
Mpenja
Mtangazaji wa
mpira wa Miguu-Azam TV
Tel: 0712461976
0 comments:
Post a Comment