Kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed 'Nduda', amewaambia
Simba kuwa atakuwa tayari kusaini mkataba na klabu hiyo kama itatoa Sh milioni
50 na mshahara mnono wa Sh milioni 3 kwa mwezi, vinginevyo atakuwa tayari
kwenda kucheza bure Majimaji.
Huo unaonekana kuwa mtihani mkubwa kwa Simba ambayo ipo
katika harakati za kumsajili kipa bora huyo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi
iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu Zanzibar.
Mohamed amesema kuwa kwa sasa hiyo ndiyo thamani yake
kutokana na kuwa katika kiwango kizuri.
Alisema kama atajiweka sokoni kwa vijesenti vya mboga
ambavyo havitakuwa na msaada wowote maishani mwake, atakuwa hajitendei haki,
pia hajithamini mwenyewe .
“Bado naendelea na mazungumzo na viongozi wa Simba lakini
mpaka sasa bado hatujafikia makubaliano kwani dau wanalotaka kunipatia ni dogo,
halilingani na thamani yangu kwa sasa”. Mohamed amekaririwa na Salehjembe.
“Ukiangalia kazi niliyofanya msimu uliopita, kila mtu
anayejua soka atakuwa anaijua thamani yangu, nimewaambia wanipatie milioni 50
na mshahara wa milioni tatu kwa mwezi, lakini wanaonekana kutokuwa tayari kutoa
fedha hizo, hivyo kama watashindwa basi ni heri nikaendelea kubakia Mtibwa au
nikarudi katika timu yangu ya zamani ya Majimaji ambayo pia inanihitaji,”
alisema Mohamed.
Kipa huyo kwa sasa ni mchezaji huru, hana mkataba na timu
yoyote ile kwani muda wake wa kuitumikia Mtibwa Sugar umefikia tamati hivi
karibuni baada ya kumalizika kwa michuano ya Ligi Kuu Bara.
0 comments:
Post a Comment