KOCHA msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, amesikia kilio cha wachezaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars, kumtaka achukue mikoba ya Mholanzi, Mart Nooij, kukinoa kikosi hicho.
Mkwasa alisema kuwa yupo tayari kuvaa viatu vya Nooij kukinoa kikosi cha Stars ambacho hivi sasa kinapumulia mashine.
“Nimesikia kilio chao, kama mzawa na mzalendo wa nchi hii ni kilio chetu wote, ni janga la kitaifa, hata siku moja hakuna raia ambaye anapenda kuona taifa lake linafanya vibaya katika michezo,” alisema Mkwasa.
Aliongeza kuwa yupo tayari kuokoa jahazi endapo ataombwa kufanya hivyo kwani uwezo anao.
“Unajua hata kipindi ambacho sisi tulikuwa nje ya nchi tukifundisha soka, watu wengi walishangaa na kutuuliza kwanini mnashindwa kuisaidia nchi yenu kupiga hatua, lakini majibu tulikosa,” alisema Mkwasa.
Alisema ingawa Tanzania bado changa katika maendeleo kisoka lakini raia wa kigeni wanaifahamu nchi hii kupitia wao pindi wanapokuwa mabalozi wazuri huko nje wanapokwenda kufundisha soka.
Hivi karibuni wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ waliuwasha moto baada ya kumtaka Charles Boniface Mkwasa, kuwa kocha Kocha Mkuu wa timu hiyo badala ya Mart Nooij aliyepo sasa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Nooij na benchi lake zima la ufundi kushindwa kubadilisha kiwango cha Taifa Stars iliyotolewa kwa aibu kwenye michuano ya Kombe la Cosafa inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Taifa Stars imeondolewa katika hatua ya awali ya makundi baada ya kufungwa bao 1-0 na Swaziland, kisha mabao 2-0 na Madagascar na baadaye na bao 1-0 dhidi ya Lesotho.
Chanzo:Bingwa
0 comments:
Post a Comment