KIUNGO tegemeo wa Simba, Jonas Mkude, amewaambia viongozi wake wasithubutu kumwacha kipa wao mzoefu Ivo Mapunda.
Mkude amesema: “Mapunda bado ana mchango mkubwa katika timu, kwanza katika msimu uliomalizika ameweza kuokoa hatari nyingi ambazo pengine kama si yeye timu ingemaliza ikiwa kwenye nafasi mbaya.”
Ingawa viongozi wa usajili wa Simba wanadaiwa kugawanyika kuhusu kumpa mkataba Ivo, Mkude alisema ni vizuri viongozi wake wakalitazama jambo hilo kwa jicho la mbali kwani uwepo wake ni muhimu kuliko kuwaacha makipa ambao bado hawana uzoefu wa kutosha.
“Ni kweli kuna makipa chipukizi, lakini bado wanahitaji msaada wa wakongwe kwani watawaongoza namna ya kufanya vizuri kuhakikisha wanakuwa manufaa kwa timu kwa miaka ijayo,” alisema.
“Ndio maana mpaka kesho nikuulizwa ni mkongwe gani arudishwe Simba, nitakutajia Mwinyi Kazimoto, kwani pengo lake bado linaloonekana.”
Mkude alisema mbali ya uwezo alionao Mapunda, lakini pia amekuwa mshauri mzuri kwa vijana katika kuwajenga namna ambavyo wanaweza kufika mbali zaidi katika maisha ya soka.
“Siingilii majukumu ya viongozi wangu, lakini kuhusu Mapunda wakimwacha pengo lake halitazibwa kwani ni muda mwafaka kwa makipa chipukizi kujifunza mambo mengi kwa Mapunda,” alisema.
Hakusita kutoa ya moyoni kwamba umakini wa hali ya juu unatakiwa kwenye kikosi chao ili kuwalinda wachezaji wenye mchango.
Chanzo:Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment