MSHAMBULIAJI mpya wa kikosi cha Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, amesema kuwa amerejea katika kikosi chake hicho cha zamani kwa kishindo huku akiwataka mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuwa na imani naye.
Mgosi ambaye aliwahi kuitumikia Simba kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa DC Motema Pembe ya DRC, ameingia kandarasi ya mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo katika msimu wa Ligi Kuu Tanzanai Bara unaokuja.
Mgosi amesema ameamua kurejea katika kikosi chake cha zamani baada ya kuona wanahitaji msaada wake na yeye hana matatizo nao.
“Ninarejea Simba kwa moyo wote na nina imani kama wataniamini basi naweza kuwafanyia kile wanachokihitaji, kikubwa ni ushirikiano wao na mimi,” Mgosi aliiambia BINGWA.
Akizumgumzia matarajio yake kwa timu hiyo, alisema ina nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kulingana na usajili unaofanywa.
“Nina imani kubwa ina uwezo wa kushiriki michuano ya kimataifa mwaka 2017 na hiyo ni kwa kumaliza nafasi ya pili au kutwaa ubingwa kwa kuwa hivi sasa inaonekana inafanya usajili makini huku ikiwekeza zaidi kuhakikisha haiji kutetereka,” alisema.
0 comments:
Post a Comment