MAAFANDE wa Tanzania Prisons ‘Wajelajela’ wameibuka na
ushindi wa goli 1-0 dhidi ya mahasimu wao wa jiji la Mbeya, Mbeya City fc
katika mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara iliyomalizika jioni hii uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya.
Goli la Prisons limefungwa dakika ya 90’ na Lugano Mwangama
kwa mkwaju wa penalti.
Kabla ya mchezo huu kulikuwa na stori nyingi kuwa Mbeya City
watawabeba Prisons ili wasishuke daraja, lakini uongozi wa Mbeya City
ulikanusha hilo mara kadhaa.
Leo baada ya Prisons kupata penalti katika hali isiyokuwa ya
kawaida, baadhi ya mashabiki wa Mbeya City walikuwa wanashangilia kuashiria
kufurahishwa na tukio, na hata lilipoingia goli walishangilia huku wengine
wakipiga ngoma na kutoka nje ya uwanja.
Lakini baada ya dakika 90’ kumalizika, baadhi ya mashabiki
wa ukweli wa Mbeya City walikuwa na hasira kutokana na matokeo hayo na walitaka
kumvamia kocha mkuu, Juma Mwambusi, lakini aliondoka haraka uwanjani hapo.
Mashabiki hao wanadai kocha huyo amekula njama ya kuwabeba
Prisons kama ilivyokuwa ikielezwa siku chache kabla ya mechi.
Hata hivyo timu zote zilicheza kwa nguvu na kutengeneza
nafasi, lakini Prisons walijikosa nafasi nyingi za wazi.
Kwa matokeo hayo, Prisons wamefikisha pointi 28 na kupanda
kutoka nafasi ya 12 mpaka nafasi ya 8 katika msimamo.
Mbeya City wanaendelea kushika nafasi ya nne wakiwa na
pointi 31 ambazo zimewaweka mikono salama ya kubaki ligi kuu na mechi ya mwisho
mei 9 mwaka huu wataikaribisha Polisi Morogoro uwanja wa Sokoine.
Prisons watasafiri mpaka CCM Kirumba Mwanza kuchuana na
Kagera Sugar na hii inatokana na Stand United kuwa na mchezo mei 9 CCM
Kambarage, uwanja ambao Kagera wanautumia kama wa nyumbani.
0 comments:
Post a Comment