MOJA ya stori kubwa ambayo leo hii imeweka 'headline' kwenye mitandao ya kijamii ni wachezaji wawili muhimu wa Mbeya City fc kusaini Simba na Yanga.
Deus Kaseke amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga, huku Peter Mwalyanzi akisaini mkataba wa miaka miwili pia kuichezea Simba msimu ujao.
Uongozi wa Mbeya City kupitia kwa katibu mkuu wake, Emmanuel Kimbe umeheshimu maamuzi ya wachezaji hao kujiunga na klabu hizo kongwe nchini.
"Sijapata taarifa rasmi ya Kaseke (Deus) na Mwalyanzi (Peter) kusaini Yanga na Simba, lakini nimetumiwa picha kwenye mitandao ya kijamii leo zikionesha wamesaini mikataba". Kimbe ameiambia MPENJA BLOG na kuongeza: "Kama ni sahihi kwa picha nilizoziona kwenye mitandao, maana yake ndicho kimetokea kwamba wachezaji hao wamejiunga Yanga na Simba. Tumeheshimu uamuzi wao, wachezaji wetu hao kwa bahati mbaya mikataba imeisha, kabla ya mazungumzo kukamilika wameamua kuondoka. Tunaheshimu na kuwatakia kila la kheri"
"Lazima maisha yaendelee kama ilivyokuwa, tunakaa chini na kupanga mikakati ya kujenga timu ya ushindani zaidi msimu ujao kwa kutumia ripoti ya kocha Mwambusi (Juma)".
0 comments:
Post a Comment