Wednesday, May 20, 2015

Na Oswald Ngonyani
Tuna uchungu sana na Taifa letu, tuna shauku kubwa ya kutaka kuiona timu yetu ya Taifa ‘Taifa stars’ ikifikia rekodi ambazo kwa miaka nenda rudi imekuwa ndoto, ingawa makocha husika wamekuwa na kauli laghai za kutudanganya watanzania kila siku.
Tumechoshwa na mbwembwe za hawa makocha tunaowalipa mamilioni ya shilingi pasipo kutusaidia chochote. Ni wakati muafaka sasa kuamka na kusema Hapana inatosha! Ndiyo ni wakati wetu watanzania kumtimua Martinus Ignatius Nooij kama ilivyokuwa kwa makocha wengineo ambao tuliwaondoa baada ya kutoipata tija yoyote kutoka kwao.
Juzi Jumatatu, Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilipoteza kizembe mchezo wake wa kwanza wa michuano ya COSAFA Castel Cup dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland, baada ya kufungwa bao 1- 0 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Royal Bafokeng jijini Rustenburg.
Ninasema ilipoteza kizembe kutokana na ukweli kuwa Kikosi hicho kilikuwa na uwezo wa kuibuka na ushindi mnono katika mchezo ule lakini kwa sababu ya wachezaji fulani fulani kukosa umakini tukajikuta tukiambulia kipigo katika mchezo huo ambao katika kipindi cha kwanza Taifa stars ilionekana kutawala.
Katika mchezo huo Stars ya Nooij ilipoteza nafasi nyingi mno katika kipindi cha kwanza kupitia kwa washambuliaji wake Simon Msuva na nahodha John Bocco ambao walishindwa kabisa kukwamisha mpira wavuni.
Wenzao Swaziland ambao walicheza vizuri zaidi katika kipindi cha pili walipata bao lao la kwanza na la ushindi kunako dakika ya 42 ya mchezo, kupitia kwa mlinzi wa kulia Sifiso Mabila aliyepanda kuongeza nguvu ya mashambulizi na kuachia shuti lililomuacha mlinda mlango namba mbili wa Yanga Deogratias Munishi maarufu kwa jina la ‘Dida’ akikosa cha kufanya kuokoa mchomo huo.
Kipindi cha pili Stars ilionekana kuzidiwa kwani mashambulizi ya Stars hayakua na madhara langoni mwa Swaziland na kumuacha mlinda mlango Mphikeleli Dlamnini akiwa likizo kwa muda mrefu.
Mwisho wa siku mchezo ukamalizika na Stars ya Nooij kutoka dimbani ikiwa kichwa chini kama tulivyozoea baada ya uzembe wa wachezaji fulani fulani dimbani, lakini pia uzembe wa kocha wa kuwapanga wachezaji fulani kwa mazoea na hata kutowaita kikosini wachezaji ambao pengine wangeweza kuleta tija kwa kikosi hicho.
Kama kawaida yake mara baada ya mchezo Mart Nooij alisema, amepoteza mchezo huo ambao alitegemea kupata ushindi, vijana walicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini bao la mapema lilionekana kuwapoteza mchezoni.
Akiongelea michuano ya COSAFA aliweka bayana kuwa anashukuru kwa kupata mwaliko huu, kwani kwake anatumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika (AFCON, CHAN) mwezi Juni, huku akisema anaamini wachezaji aliowaacha majeruhi nyumbani pamoja na wachezaji wa kimataifa wanaochezea klabu ya TP Mazembe, wataongeza nguvu katika kikosi chake watakaporejea Tanzania.
Binafsi yake anaweza akafikiri kuwa maneno hayo machache yanaweza yakawapumbaza watanzania, kitu ambacho hakiwezi kikawezekana kwa sasa. Watanzania wa leo si wale wa enzi za akina Maximo, watanzania wa leo wanajua mengi na wala hawaogopi kuhoji kwa maslahi ya Taifa lao.
Hii ina maana kwamba, Mart Nooij asijidanganye kwa mbwembwe zake za maneno matamu yanayotoka kinywani mwake, badala yake anapaswa aelewe wazi kuwa kwa matokeo haya anayoyapata kila siku, watanzania tumemchoka.
Tangu ujio wake ameonekana kufanya uteuzi wa wachezaji wengi wasiopewa nafasi katika vilabu vyao wanavyovichezea lakini kila anapohojiwa na wanahabari ameonekana kuwa mkali kama mbogo huku akiitanguliza mbele hulka ya ukaidi kwa kushindwa kutoa majibu yanayostahiki kwa faida ya watanzania wengi.
Leo hii unamuachaje mlinda mlango nambari moja wa Yanga Ally Mustafa ‘Barthezi’ katika kikosi cha Stars na kumjumuisha mlinda mlango namba mbili wa timu hiyo? Leo hii unawezaje kumuacha beki kisiki na chipukizi wa Simba anayeonekana kuhusudiwa na makocha wengi wa Ligi ya Vodacom Hassan Ramadhan Kessy katika kikosi hiki chenye vijeba wengi?
Vipi kuhusu washambuliaji Rashid Mandawa au Andrew Vicent wa Mtibwa, ni kweli viwango vyao havikidhi vigezo vya kujumuishwa kikosini? Kama sivyo, kwanini kila tukihoji tunajibiwa majibu rahisi ya No comments! wakati ni wajibu wetu kujua?
Hpana shaka haya ni maamuzi ya kibinafsi yanayotia hasira sana. Kila siku tunazungumza na kuandika lakini kwa bahati mbaya sana hatuoni tofauti yoyote. Ni kama tunampigia mbuzi gitaa, sijui mwisho wake itakuwaje.
Ikumbukwe kuwa Taifa Stars hii iliyopo Afrika Kusini itacheza mchezo wake wa pili leo Jumatano saa 11 za jioni kwa saa za Afrika kusini, sawa na saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki dhidi ya Madagascar katika uwanja wa Royal Bafokeng., ambao katika mchezo wa awali wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lesotho.
Ni wazi kuwa hautakuwa mchezo wa lelemama, hautakuwa mchezo wa kuleta masihara tena kama tulivyozoea kuona. Utakuwa ni mchezo ambao kwa hali na mali Taifa stars itabidi ishinde ili kuweza kujiweka katika mazingira salama ya kuendelea na Mashindano hayo kinyume na hapo hakutakuwepo na matumaini ya kucheza robo fainali.
Kitu kikubwa ambacho kinakatisha tamaa zaidi ni rekodi ya Mwalimu huyu tangu alipokabidhiwa mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen mwaka uliopita ambapo katika michezo 14, Taifa stars imeshinda michezo mitatu pekee, sare sita na imefungwa mechi 5.
Pengine rekodi hiyo unaweza ikakufanya ufikiri kuwa kikosi hicho cha Nooij kilicheza timu ngumu za barani Ulaya na Amerika kama Ujerumani, Ufaransa, Argentina na Uholanzi, kitu ambacho si cha kweli. Taifa stars imepoteza michezo yake mitano dhidi ya timu tulizozizoea sana tena nyingi zinatoka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa hapa Stars yetu ilipofikia ni wazi kuwa Mart Nooij ametuudhi sana, sasa inatosha. Atuachie Stars yetu ili tuweze kujua cha kufanya kwa lengo la kuipa hadhi soka yetu. Soka ambayo kwa siku za usoni imetufanya tuzidi kusahaulika tena na tena huku wale tuliokuwa tumewapita kabla wakizidi kuchanja mbuga huku sisi tungali tukirudi nyuma.
(0767 57 32 87)

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video