MADAGASCAR imetinga robo fainali ya Cosafa baada ya kufanikiwa kumaliza vinara wa kundi B wakiipiku Swaziland kwa idadi nzuri ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Timu hizo ambazo zilizokuwa zinachuana kusaka timu moja ya kutinga robo fainali zimetoka sare ya 1-1 usiku huu.
Mechi ya kwanza ya kundi hilo, Madagascar walishinda 2-1 dhidi ya Lesotho, mechi ya pili wakaifumua 2-0 Tanzania 'Taifa Stars' na leo wametoka sare ya 1-1 na Swaziland.
Kwa matokeo hayo Madagascar wamefunga magoli 5 na kufungwa 2.
Kwa upande wa Swaziland wao walianza michuano kwa kuifunga 1-0 Taifa Stars, wakashinda 2-0 dhidi ya Lesotho na leo wametoka sare ya 1-1 na Madagascar, hivyo wamefunga magoli 4 na kufungwa 1.
Kwa matokeo hayo, mei 24 mwaka huu Madagascar watacheza mechi ya robo fainali dhidi ya Ghana uwanja wa Moruleng majira ya saa 9:00 kwa saa za Afrika kusini sawa na saa 10:00 kwa saa za Afrika mashariki.
Mechi nyingine ya robo fainali siku hiyo itawakutanisha Malawi na Msumbiji.
Kwa upande wa kundi A, Namibia walifuzu robo fainali na watachuana na Zambia mei 25 mwaka huu uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace majira ya saa 11:30 kwa saa za Sauzi sawa na saa 12:30 kwa saa za Tanzania.
Mechi nyingine ya robo fainali siku ya jumatatu itawakutanisha wenyeji Afrika kusini dhidi ya Botswana.
0 comments:
Post a Comment