Mkurugenzi mpya wa Bodi ya ligi kuu nchini, Boniface Wambura
BAADA ya Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kumteua
Boniface Wambura Mgoyo kuwa Mkurugenzi mpya wa Bodi ya ligi kuu nchini (TPLB), klabu
ya Yanga imepongeza uteuzi huo na kuahidi kutoa ushirikiano wote kwa kiongozi
huyo.
Kabla ya uteuzi huo, Wambura alikuwa mkurugenzi wa
mashindano wa TFF na sasa ataanza kazi
yake mpya kuanzia Juni mosi mwaka huu akirithi mikoba ya Silas Mwakibinga.
Wambura pia aliwahi kuwa Afisa habari wa TFF kabla ya kuwa
Mkurugenzi wa mashindao na alifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa akijenga imani
kubwa kwa TFF na wanamichezo kwa ujumla.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro
amesema Wambura ni mtu mwenye uwezo na weledi wa hali ya juu katika kuendesha
soka.
“Alipokuwa mkurugenzi wa mashindano wa TFF, alikuwa anaelewa maana ya mashindano,
alionesha uwezo na uweledi wa kutosha sana katika kuendesha mpira wetu wa miguu
kwa mtindo wa kisasa”. Amesema Muro na kufafanua zaidi: “Yanga kilicho chetu ni
bodi ya ligi, mpaka mimi nitundikwa faini ya milioni tano ni bodi ya ligi, kwa
muda mrefu tangu aondoke Silas Mwakibinga tumeshuhudia bodi ya ligi iliyokuwa
inaendeshwa kwa misingi ya ubabaishaji. Hili neno ubabaishaji ni miongoni mwa
maneno ambayo yamenipa adhabu, na mimi nitarudia tena, Bodi ya ligi ilikuwa
ikiendeshwa kwa misingi ya ubabaishaji, lakini sasa Bodi ya ligi imepata mtu makini, mtu muelewa.
Sisi kama Yanga tutaungana naye kwa jambo lolote ambalo atahitaji kutoka kwetu
ili tuweze kuendeleza mpira wetu na kufikia kiwango cha kimataifa.
Kwa upande wake Wambura amesema anaichukulia nafasi hiyo
mpya kama changamoto kwake, lakini anahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau wote
ili kuboresha utendaji wa chombo hicho muhimu.
“Kwanza nimeichukulia nafasi hiyo kama changamoto, lakini kikubwa ni
imani ambayo kamati ya utendaji ya TFF na Bodi ya ligi wameonesha juu yangu.
Niahidi kwamba kikubwa ni ushirikiano ili kuhakikisha ligi kuu ya Vodacom, ligi
daraja la kwanza zinakuwa bora zaidi, Pia ligi daraja la pili ipelekwe kwenye
bodi na kuwa moja ya vichocheo vya maendeleo ya mpira wa miguu nchino” Amesema
Wambura na kukiri. “Lazima tukubali kuwa huko tulikotoka tulikuwa nyuma zaidi
na kadri tutakavyokwenda tutaimarika, mwanga unaonekana mbele, kikubwa ni
uweledi tu, watu wanaamini zikiwemo hata klabu kuwa ligi ni mali ya bodi,
lakini klabu zitambue kuwa wao ni wadau wakubwa na ligi ni mali yao, TFF na
Bodi ni wasimamizi tu”.
0 comments:
Post a Comment