SHIRIKISHO la soka Tanzania TFF leo limetuma taarifa kwa vyombo vya habari
kwamba timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuingia kambini
kesho jumatano katika hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani jijini Dar es
salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri kuwania kufuzu kwa AFCON.
TFF wamesema kwamba, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij, amewaita wachezaji 16 kuingia
kambini kesho kwa ajili ya kupimwa afya zao na kujua maendeleo yao kabla ya
kuwajumuisha katika kikosi cha pamoja kitakachokuwa kwenye maandalizi ya mchezo
dhidi ya Misri.
Wachezaji walioitwa kuingia kambini kesho
ni; Mohamed Hussein, Peter Manyika,
Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba SC), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub
(Yanga SC), Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Kelvin Friday (Azam
FC), Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand
United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).
Mara baada ya kurejea kutoka nchini Afrika
Kusini, kocha wa Stars, Nooij aliwapa mapumziko ya siku 10, wachezaji waliokua
kwenye michuano ya Cosafa mpaka Juni Mosi ambapo ndipo watajumuika na wachezaji
wengine waliopo kambini.
Ifikapo Juni Mosi, 2015 Taifa Stars itaanza
kambi ya moja kwa moja kujiandaa na mechi dhidi ya Misri itakayochezwa jijini
Alexandria katika uwanja wa Borg El Arab Juni 14, 2015 ikiwajumuisha pia
wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika
klabu ya TP Mazembe ya Congo DR.
Kabla ya kuelekea nchini Misri, Taifa Stars
inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe 4, Juni
2015 kwa muda wa wiki moja kabla ya kuelekea nchini Misri kwenye mchezo huo
dhidi ya Mafarao.
Juni 20, 2015 Taifa Stars itawakaribisha
Uganda kwenye uwanja wa Aman mjini Zanzibar katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa
Fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN, zitakazofanyika nchini Rwanda
2016, na mchezo wa marudiano kufanyika baada ya wiki mbili nchini Uganda.
Nimesoma vizuri taarifa hii ya Mart Nooij kuteua wachezaji
wengine wa Taifa Stars pamoja na program nzima ya timu kuelekea mechi za
mashindano, lakini bado nina mashaka juu ya hali ya kiafya ya Hassan Isihaka,
Nadir Haroub na Haruna Chonongo.
Asubuhi ya leo mtandao huu umeongea na Chonongo ambaye ni
majeruhi na anatarajia kuanza mazoezi mepesi jumatatu au jumanne ya wiki ijayo.
Kwa maana hiyo bado anahitaji muda ili kukaa sawa. Kwa
Cannavaro na Isihaka pia wanahitaji muda wa kurudi katika hali yao kwani
hawajacheza kwa muda mrefu kutokana na majeruhi.
Imeelezwa kuwa wachezaji 16 walioitwa watajumuishwa na
wenzao waliokuwepo Afrika kusinii kushiriki michuano ya Cosafa ambao ni: Deogratius Munish, Mwadini Ali, Shomari Kapombe,
Erasto Nyoni, Oscar Joshua, Haji Mwinyi, Salim Mbonde, Aggrey Moriss, Joram
Mgeveke, Said Juma, Hassan Dilunga, Said Ndemla, Abdi Banda, Mwinyi Kazimoto,
Ibhrami Ajib, Juma Luizio, John Bocco, Mrisho Ngasa na Saimon Msuva.
Taifa Stars ilitolewa hatua
ya awali ya makundi ikipoteza mechi zote za kundi B. Ilifungwa 1-0 na
Swaziland, ikafumuliwa 2-0 na Madagascar, mechi ya mwisho ikachapwa 1-0 dhidi
ya Lesotho.
Matokeo haya mabaya
yaliwashitua Watanzania wengi kwasababu timu ilicheza hovyo katika idara zote.
Stars haikuwa na muunganiko
wowote wa kiuchezaji, alionekana haijafundishwa chochote, ilijaa wachezaji
ambao hawakuwa na msimu mzuri katika klabu zao mfano, Deogratius Munish, Amri
Kiemba, Erasto Nyoni na wengineo.
Watanzania wengi walichukizwa
na kiwango duni cha Stars, lakini hasira zao zilichagizwa zaidi na uteuzi mbovu wa
kikosi . Kuna lundo la wachezaji ambao walifanya vizuri kwenye ligi lakini
wakaachwa, Mfano, Hassan Kessy (Simba),
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Juma Abdul (Yanga), Rashid Mandawa
(Kagera Sugar), Jonas Mkude (Simba) na wengine ambao wamejumuishwa kwenye
kikosi kilichotajwa leo.
Masikitiko ya wengi ni Hassan
Kessy kuachwa tena Taifa Stars kwasababu alikuwa na msimu mzuri mno akiichezea
Simba. Labda wengi wanaweza kutulia baada ya kuitwa kwa Juma Abdul wa Yanga
ambaye pia iliimudu vyema nafasi ya mlinzi wa kulia Yanga.
Stori kubwa baada ya Stars
kurejea nchini ilikuwa hatima ya kocha Mart Nooij ambaye alijadiliwa jumapili
iliyopita na kamati ya utendaji ya TFF . Maamuzi ya kikao hicho yalikuwa haya
hapa chini;
Kamati ya utendaji ya
TFF imesikitishwa na mwenendo mbovu wa Taifa Stars Rais wa TFF, Jamal Malinzi
kwa niaba ya kamati ya utendaji amewaomba radhi wapenzi wa mpira kwa matokeo
mabaya ya Taifa Stars kwenye michuano ya Cosafa.
Kikao cha kamati ya
utendaji kilipokea taarifa juu ya mwenendo wa timu ya Taifa.
Baada ya majadiliano
ya kina, ilikubaliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa, Mart Nooij apewe
changamoto maalumu ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN
na asipofanikisha jambo hilo mkataba wake utasitishwa mara moja.
Maamuzi haya
yamezingatia hali halisi ya timu ya Taifa ambayo inakabiliwa na michuano
mbalimbali ya kimataifa ndani ya kipindi kifupi.
Aidha katika
kuliimarisha benchi la ufundi la timu ya Taifa, Leopald Tasso Mkebezi
ameteuliwa kuwa meneja mpya wa timu ya Taifa.
Mkebezi amewahi kuwa
meneja wa timu ya Taifa katika kipindi cha mwaka 2006 – 2012.
Watanzania wengi walitegemea kumsikia Rais Malinzi akifikia
maamuzi magumu juu ya Mart Nooij, lakini akawa tofauti. Dhahiri Ma linzi
amehofia gharama za kuvunja mkataba kama alivyofanya bila sababu kwa Kim
Poulsen.
Siku mbili tu baada ya kikao cha kamati ya utendaji, leo
Mart Nooij anaita wachezaji 16, huku asilimia kubwa ndio wale wale waliokuwa
wanatajwa na wadau mbalimbali wa soka, lakini akawapuuza.
Nakumbuka kwenye mkutano mmoja na waandishi wa habari baada
ya kuwaita wachezaji wa kwenda nao Cosafa, Nooij aliulizwakwanini amewaacha baadhi
ya wachezaji walioonesha kiwango cha juu kwenye ligi akiwemo Jonas Mkude,
Hassan Kessy n.k lakini akajibu kwa ‘jeuri’
kuwa Tanzania ina wachezaji zaidi ya 300, kwanini waulizwe hao tu? Tena akasema
wachezaji wanaotajwa wanaweza kuwa wazuri kwa makocha wengine, lakini sio
kwake.
Wadau walikuwa na hoja kwamba wachezaji wengi waliong’ara
ligi kuu ni vijana, hivyo kocha Nooij angewajumuisha kwenda Cosafa ili wakapate uzoefu kabla ya kuzivaa Misri na
Uganda katika mechi za mashindano.
Kama Oscar Joshua ni mzuri zaidi ya Tshabalala, basi muite
Tshabalala Taifa Stars awe mbadala wake. Atajifunza mengi hata akikaa benchi kuliko
kukaa nje ya Taifa Stars. Unawezaje kumtumia Salum Abubakar nafasi ya kiungo
mkabaji, wakati umemuacha mchezaji kama Jonas Mkude wa Simba?
Hamu ya Watanzania ilikuwa ni kuona akina Malim Busungu,
Rashid Mandawa wakiwemo Taifa Stars iliyoshiriki ‘Bonanza’ la Cosafa kwasababu
walionesha kiwango cha kufunga magoli VPL 2014/2015, lakini kocha akamuita John
Bocco ambaye hayuko fiti kabisa na amefunga magoli matatu tu msimu mzima.
Binafsi naamini katika kikao cha TFF, Rais Malinzi
alimwambia Nooij kinachoendelea na namna Watanzania walivyochukia. Bila shaka
alimueleza kuwa wanaponda uteuzi wa kikosi chake na nadhani alipewa majina
mengi ya wachezaji ambao watu wanalalamikia, hivyo ameamua kuwaita leo baada ya
kuambiwa na bosi.
Kitendo cha Nooij kuwaita wachezaji hao ni kujaribu kuwazuga
Watanzania, muda mzuri ulikuwa kule Cosafa. Sahizi hata kama atataka kuwapima,
atapata wapi mechi za ‘Bonanza’ kama kule Afrika kusini?
Mimi naamini Nooij alichemsha toka mwanzo, siwezi kumuunga
mkono eti kwasababu kawaita wachezaji niliotarajia, kwanini hakufanya hivyo
wakati anakwenda Cosafa?
Wachezaji ambao amewaita leo, angeenda nao Cosafa wangepata
uzoefu mzuri kuliko sasa, hapa katikati watakosa mechi za kirafiki kabla ya
kuingia kwenye mechi za mashindano. Au anataka kuwatia kikaangoni ili waonekane
vimeo?
Wanaojua mpira wanaelewa kwamba mchezaji anapokwenda kwenye
mashindano ya kimataifa anatakiwa kuandaliwa, cosafa ilikuwa sehemu murua ya
kusuka kikosi kipya cha Stars.
Hivi kweli Nooij kawaita hawa wachezaji? au ameambiwa waite
hawa kwasababu tushachafua hali ya hewa?. Cha kuchekesha ni kwamba wachezaji wengi
aliowaita leo alisema ni bora kwa makocha wengine na sio kwake.
Bahati mbaya watanzania wanasahau, ishu ya Deus Kaseke na
Pater Mwalyanzi kusajiliwa Yanga na Simba imeondoa mjadala wa Taifa Stars,
lakini hili la leo sio njia ya kuwaridhisha Watanzania bali ni kuwadhihirishia
kuwa TFF wanafanya mambo kiujanja-ujanja, hiki ni kiini macho cha mchana
kweupe.
Mart Nooij hana mwelekeo, wachezaji aliowaita ni wazuri,
lakini siku zote kama kocha sio mzuri, wachezaji hawawezi kufanikia.
Wachezaji wa Stars wamekufa moyo kwa matusi ya Watanzania
kwasababu ya Mart Nooij, naamini ukimleta kocha mwingine akakaa hata na timu ile
ile iliyoenda Cosafa, wanandinga hao wanaweza kubadilika na kuonesha kiwango
tofauti na sasa.
Tuna matatizo mengi katika mpira, utawala si mzuri, mfumo si
mzuri, hayo tunaeleza kila siku, lakini kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij sio
mzuri katika soka letu hili la ‘kichwa cha mwenda wazimu”.
Halali yako kukosoa maoni haya binafasi!
Na Baraka Adson Mpenja
Mtangazaji wa mpira wa Miguu-Azam TV
Tel: 0712461976
0 comments:
Post a Comment