Jerry Muro
MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young Africans
wamewasilisha mapendekezo Shirikisho la soka Tanzania TFF wakiomba kuongezewa
idadi ya wachezaji wa kigeni mpaka kufikia nane (8).
Kwa mujibu wa kanuni ya sasa, klabu inaruhusiwa kusajili
wachezaji watano (5) tu wa kimataifa, lakini klabu kubwa zinazowakilisha nchi
kwa muda wa miaka mitatu sasa, Yanga na Azam zinalalamika kwamba idadi hiyo ni
ndogo na imewanyima fursa ya kufanya vizuri kimataifa kwasababu ya kukosa wachezaji
wengi wa kiwango cha kimataifa.
Mkuu wa Idara ya habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro
amesema tayari wana majina ya wachezaji 12 wa kimataifa, hivyo wanasubiri
majibu ya mapendekezo yao kutoka TFF.
“Tunachelea kutaja idadi ya wachezaji wa kimataifa ambao
tutawachukua mpaka sasa kwasababu tayari tulishaandika mapendekezo yetu kwenda
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF yakijumuisha mambo mengi likiwemo
suala la usajili wa nyongeza ya wachezaji wa kimataifa’, Amesema Muro na
kuongeza: “TFF, ijaribu kutusaidia tuweze kupata nafasi ya kusajili wachezaji
nane wa kimataifa ili tuweze kujiandaa
vizuri katika ushiriki wetu wa michuano ya klabu bingwa Afrika ambayo Yanga
itawasikilisha nchi”.
Hata hivyo Yanga imesema kama itaambiwa iendelea na idadi
ile ile ya wachezaji wa kigeni (watano) itabidi ikae chini kuangali ni akina
nani watasajiliwa.
“Wakituambia tusajili wachezaji wale wale watano waliotupa
fursa, basi sisi kama klabu tutalazimika kujibana. Tunao wachezaji takribani 12
ambao wamekuja kwetu na wengine tumewafuata, wengine tulishakuwa nao kwasababu dirisha dogo
mwaka jana lilikuwa limeshafungwa. Tunaangalia kama tunaweza kuwasajili
wachezaji wote”. Amefafanua Muro .
Wakati huo huo, Muro ametamba kuwa: “Kwa mara ya kwanza
katika historia ya Yanga tutasajili wachezaji ambao ni kiwango cha dunia ‘World
Class Players’, wachezaji ambao hawatakuwa na shaka yoyote kuthibitisha ubora
wao kama tulivyofanya kwa wachezaji wa ndani mfano Kaseke (Deus). Yeye toka
ligi inaanza waandishi na wachambuzi wa michezo wamesema miongoni mwa wachezaji
ambao Tanzania tunao kama lulu na ni hazina kwa taifa ni Deus Kaseke pamoja na wengine ambao hivi punde tutamalizana nao”.
0 comments:
Post a Comment