Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
UONGOZI wa mabingwa wa msimu wa 2013/14 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC wameweka wazi kwamba wanahitaji huduma ya winga aliyeingia katika malumbano na klabu ya Simba, Ramadhani Singano 'Messi'.
Moja ya mitandao ya kimataifa ya michezo umemnukuuu Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrissa Nassor, akieleza kuwa wana mpango na winga huyo kwa ajili ya msimu ujao wa VPL na michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Idrissa amesema wameshafanya mazungumzo na mchezaji (Messi) na wanachokisubiri kwa sasa ni nyota huyo kumaliza malumbano na klabu yake ya Simba ili waweze kukamilisha taratibu za kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.
“Messi ni mchezaji mzuri na sisi kama Azam tungependa msimu ujao kuwa naye kwenye kikosi chetu, tumeshafanya mazungumzo naye tumekubaliana, lakini tunasubiri amalizane na viongozi wa timu aliyokuwa anaichezea ili tukamilishe mipango yetu ya kumsajili,” amesema Idrissa.
Messi amekuwa na malumbano makubwa na uongozi wa Simba ambao unadai mchezaji huyo bado amebakiwa na mwaka mmoja wa kuichezea klabu hiyo katika mkataba wake huku mwenyewe akisema amemaliza mkataba huo na kudai viongozi hao wamegushi mkataba huo unaoonyesha bado ana mwaka mmoja wa kuichezea Simba.
Nyota huyo aliyekulia Simba B amekuwa akiifunga Azam karibu katika mechi zote anazocheza dhidi ya matajiri hao wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment